HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN, KWENYE BARAZA
LA IDD EL HAJJ TAREHE 26 OKTOBA, 2012
Bismillah Rahman Rahim
Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, Subhanahu
Wataala, Aliyetupa uhai na uzima tulionao tukaweza kuitikia wito wake, alioutoa
tangu zama za Nabii Ibrahim (AS). Katika Kur-ani imeelezwa kwamba Nabii Ibrahim
ameamriwa kuwatangazia watu kwenda kuhiji na watakuja kutoka kila
upande wa dunia na kwa kila kipando. Mwenyezi Mungu ndie aliyewakirimu Waislamu
wenzetu kwa mamilioni, kuitikia wito huo na kuwapa uwezo wa kwenda kuizuru
nyumba tukufu ya Alkaaba huko Makka mwaka huu wakiwa wamoja, kwa wakati
mmoja kwa lengo la kumuabudu Yeye Mola wetu Mmoja.
Tunashuhudia kuwa hapana anaepaswa kuabudiwa kwa haki
isipokuwa Allah (SW), Ambaye ndiye Mmiliki wa vyote na Kwake vyote
vitarejea. Sala na salamu zimshukie Hashimu, Mtume wa Mwenyezi
Mungu, Bwana wetu Muhammad (SAW) na wafuasi wake walioshikamana na mwenendo
wake na mafundisho, na wakaongoka. Inshaalla Mwenyezi Mungu atujaaliye na sisi
tuwe miongoni mwao - Amin.
Makamu wa Kwanza wa Rais;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd,
Makamu wa Pili wa Rais;
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, na Mama
Shadya Karume,
Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho,
Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu,
Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
Othman Masoud;
Mheshimiwa Sheikh Khamis Haji Khamis,
Kadhi Mkuu;
Mheshimiwa Naibu Mufti
Sheikh Mahmoud Mussa Wadi
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Mabalozi,
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama Vya Siasa mbali mbali,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Assalamu Alaykum Warahmatullah Taala Wabarakatuhu
IDD MUBARAK
Namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema na Utukufu,
Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote viliomo na Mfalme wa siku ya Mwisho kwa
ukarimu wake kwetu; Ametukarimu neema ya uhai tukaweza kuhudhuria hafla hii
adhimu. Ni uwezo wake Yeye tu Subhanahu Wataala ndio uliotuwezesha kukutana
hapa kwa kujumuika na kuungana na Waislamu wenzetu walioko huko katika mji
Mtakatifu wa Makka ambao wanaitekeleza nguzo ya tano ya dini ya Kiislamu; Ibada
ya Hijja.
Kwa hakika, tuna wajibu wa kuwatakia kheri na baraka ndugu
zetu na Waislamu wote ambao Mwenyezi Mungu amewaruzuku uwezo wa kwenda Hijja
mwaka huu. Tumuombe Mola wetu azitakabalie ibada zao na awarudishe nyumbani kwa
salama ili waungane tena na familia zao, ndugu zao, jamaa zao na majirani zao
na huku wakiendeleza mafunzo waliyoyapata katika mkusanyiko huo wa kila mwaka
wa waislamu duniani.
Ndugu Wananchi,
Wakati huu ambao tumo katika furaha ya kusherehekea sikukuu
hii, tunapaswa tuzingatie mambo ambayo tunajifunza kutokana na sikukuu hii
muhimu kwa waislamu wote duniani. Ni dhahiri kuwa miongoni mwa
mafunzo muhimu tunayopata, ni kwa watu kuwa pamoja katika hali ya amani na
kutii amri ya Mola wetu bila ya kujali tofauti tulizonazo za utaifa, jinsia na
uwezo wa kiuchumi. Ni uwezo na utukufu wa Mola wetu kutuwekea mkusanyiko huu
mkubwa kwani anajua udhaifu wa wanadamu unaopelekea kuibuka kwa migogoro na
mivutano miongoni mwetu jambo ambalo tayari alikwishatuelekeza katika aya ya 13
ya Suratush-Shuura kwa kusema:
“Amekupeni Sharia ya Dini ile aliyomuusia Nuhu na
tuliyokufunulia wewe na tuliyowausia Ibrahim na Mussa na Issa, kwamba
simamisheni Dini wala msifarikiane kwayo, (kwa ajili ya dini); ni ngumu kwa
wenye kushirikisha (dini hii) unayowaitia; Mwenyezi Mungu humchagua Kwake
amtakaye na humuongoza Kwake aelekeaye (Kwake).
Ndugu Wananchi,
Mafunzo mengine tunayopata kupitia ibada ya Hijja ni utii wa
Waislamu kwa Mola wao katika kuzitumia neema za uwezo wa mali na siha kwa ajili
ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Watu ambao, wameahidiwa fadhila kubwa kama
inavyothibitika kwenye aya ya 69 ya Suratul An-nisaa
“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao
watakuwa pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu, Manabii na Masidiki na Mashahidi
na Masalih (watu wema)….. “
Sote ni mashahidi kuwa si kila mwenye uwezo wa mali au siha
hudiriki kutekeleza ibada hii. Wenzetu hawa Mwenyezi Mungu amewaafikishia
kutekeleza nia zao na wamefaulu kumshinda iblisi ambaye hupenda kuwazaini
wanadamu katika njia ya Mwenyezi Mungu ili watumie neema alizowapa katika
kumuasi.
Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie kuyatumia mafunzo yote
yanayopatikana kwenye ibada zetu katika kulikamilisha lengo la kuumbwa kwetu na
kuletwa duniani. Awajaalie mahujaji wote na sisi tuzitumie vyema neema alizoturuzuku
Allah.
Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mola wetu (SW) kwa neema
zisizomithilika alizoturuzuku sisi wanadamu na kutufanya tuwe viumbe bora na
Makhalifa wa dunia. Katika kuweza kumudu jukumu hilo, Allah
ameturuzuku akili tuitumie kupambanua utukufu wake katika kuiumba dunia na
viliomo na kuvitumia katika kumtukuza Yeye katika maisha yetu ya hapa duniani
ili tupate mafanikio mema huko Akhera.
Mwenyezi Mungu anatubainishia hayo katika aya ya 15 ya
Suratul Mulk kuhusu kuitumia vyema neema ya ardhi aliyotupa kwa kusema,
“Yeye ndiye aliyefanya ardhi iweze kutumika kwa ajili
yenu. Basi nendeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake, na
kwake Yeye ndiyo marejeo (yenu nyote)”.
Ndugu Wananchi,
Mwenyezi Mungu ametujaalia nchi ndogo yenye watu wenye
uhusiano wa karibu wa udugu, tuna watu wenye maarifa makubwa ya elimu mbali
mbali na afya za kiwiliwili. Kadhalika,
tuna rasilimali ya bahari, misitu, ardhi ya kilimo na
maliasili nyenginezo ambazo wenzetu wengine hawajabahatika kuwa nazo. Serikali
zote duniani hujiwekea mipango ambayo huwa ndiyo dira ya kufuata katika
matumizi ya rasilimali zake.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu Awamu ya Kwanza hadi
sasa imejitahidi kupanga mipango mbali mbali ya maendeleo katika vipindi
tofauti, ili kuweza kuzitumia vyema rasilimali ziliopo kwa lengo la kuinua
uchumi wetu na kuleta ustawi bora wa wananchi wa Zanzibar. Sote tunakiri kuwa
nchi yetu imepiga hatua ya kupigiwa mfano katika maendeleo kwenye nyanja za
uchumi na ustawi wa jamii tangu Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari,
1964.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilipoingia
madarakani miaka miwili iliyopita, iliahidi kuendeleza mipango hiyo na
kudumisha mafanikio yake. Miongoni mwa mpango mkuu wa Serikali ni DIRA 2020
ambayo sasa imeshatimia miaka 12 katika utekelezaji wake na kubakiwa na miaka
minane.
Dira hii ndiyo iliyotuwezesha kuandaa mikakati mbali mbali
ya kitaifa ya muda tofauti ukiwemo Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umasikini Zanzibar (MKUZA). Hivi sasa tuna mpango wa uchumi unaotokana na MKUZA
II uliotayarishwa kwa kipindi cha miaka 5 ulioanza mwaka 2010 hadi mwaka 2015,
na baada ya hapo utapangwa mpango mwengine wa miaka mitano utaokaoanza mwaka
2015 hadi kufikia mwaka 2020.
Ndugu Wananchi,
Ripoti ya mapitio ya Dira 2020 iliyotolewa hivi karibuni
imeonesha kwamba yapo mafanikio ya kutia moyo yaliyopatikana katika utekelezaji
wa Dira ya 2020, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kuyafikia
malengo yetu kwa muda uliobakia. Malengo hayo yatafikiwa iwapo kila mtu
atafahamu kuwa ushiriki wake katika utekelezaji ni sehemu ya mafanikio ya
utekelezaji wa mipango hiyo.
Kadhalika, kila mtu mahali alipo aongeze bidii ya kufanya
kazi kwa kuongeza uzalishaji na utoaji wa huduma. Wakulima, wavuvi na wafugaji
waongeze bidhaa wanazozizalisha kwa kutumia fursa zilizokwishaandaliwa na
Serikali. Wafanyakazi katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya elimu, afya,
biashara, mawasiliano, nishati, maji na nyenginezo waimarishe utoaji wa huduma
zao ili kwa pamoja ziwe kichocheo cha kuleta ustawi bora wa jamii na kupunguza
umasikini. Tutilie maanani usemi maarufu kuwa “juhudi ndiyo siri ya
mafanikio”.
Ndugu Wananchi,
Tunapozungumzia haja ya kushirikiana katika utekelezaji wa
mipango ya Serikali, tunapaswa pia tuzingatie matumizi bora ya rasilimali
tulizonazo ili ziwe endelevu. Nchi yetu ina ardhi ndogo isiyoongezeka lakini
idadi yetu inaongezeka kwa wastani wa asilimia 3.1 kila mwaka. Hali kama hii
inasababisha kuendelea kuwepo kwa mahitaji makubwa ya ardhi ya kujenga makaazi
na matumizi makubwa ya rasilimali ikiwemo misitu na rasilimali nyengine
zisizorejesheka.
Katika kukabiliana na changamoto kama hizi, ndipo Serikali
inapolazimika kuandaa taratibu, sheria na sera mbali mbali za kusimamia
matumizi bora ya rasilimali. Mathalan, Serikali imeandaa Sheria ya
matumizi ya Ardhi na pia Sheria ya Mipango Miji, ili ardhi yetu itumike kwa
utaratibu mzuri. Kadhalika, Sheria ya kuzuia uvuvi haramu ina
madhumuni ya kuifanya amali hiyo ambayo ni tegemeo la wananchi wengi hapa
Zanzibar iwe endelevu, yenye tija na itufae tuliopo na watakaokuja. Kwa
hakika, hii itakuwa namna bora ya kuzitumia neema hizi alizoturuzuku Mwenyezi Mungu.
Ndugu Wananchi,
Dini yetu ya Kiislamu inatufundisha kuwafikiria wengine hasa
katika mambo ya neema na kheri na kuwaepusha na matatizo. Ndiyo
maana tunaamrishwa kutoa sadaka ambayo siri yake kuu ni kujiepusha na ubinafsi
na kumkuza mja kuwa na roho ya imani kwa wengine. Sadaka huitakasa
nafsi ya mja na kumwelekeza mtu kwenye imani na kufanya ihsani. Mwenyezi
Mungu amesema kwenye kitabu kitukufu cha Kur-ani aya ya 90 ya Suratun Nahl:
“Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu, na
kufanya hisani na kuwapa jamaa (na wengineo); na anakataza uchafu na uovu, na
dhulma. Anakunasihini ili mupate kufahamu (mfuate).”
Katika kukamilisha sherehe ya Idd hii huwa tunahimizwa
kuchinja na kuwapa haki tuliowajibishwa wakiwemo masikini na marafiki. Suna hii
ikiwa ni kiashirio cha utii aliouonesha Nabii Ibrahim (AS) katika kumchinja
mwanawe Ismail kwa kuonesha utii kwa Mola wake. Basi katika kufikiria wenzetu,
tugawe nyama hiyo tunayochinja kama inavyoelezwa na kuwafikiria zaidi masikini.
Ndugu Wananchi,
Tuzitumie vizuri rasilimali ziliopo nchini kwa ajili ya
maendeleo yetu hivi sasa, lakini wakati huo huo tuoneshe imani zetu kwa
kuwafikiria wenzetu wengine watakaozihitaji rasilimali hizi katika miaka ijayo.
Kwa mfano tunapokata misitu ovyo, kukata miti kwenye vianzio vya maji, kuchimba
mchanga bila ya taratibu na kuchimba mawe na matofali ni baadhi tu ya shughuli
ambazo huharibu sana mazingira yetu na kuviachia vizazi vijavyo mazingira
yasiyo na ubora.
Serikali kupitia taasisi zake mbali mbali imeweka taratibu
na sheria za kukabiliana na vitendo vinavyosababisha uharibifu wa mazingira.
Hivyo, ni wajibu wa wananchi kufuata taratibu hizo na kuzingatia ushauri wa
kitaalamu ili mazingira yetu yawe endelevu kama ni njia moja ya kubainisha
imani zetu kwa kuwafikiria wengine.
Ndugu Wananchi,
Serikali itaendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kufuata
taratibu kama hatua muhimu ya kuimarisha utawala bora nchini. Hata
hivyo, suala la kusimamia taratibu na kuona kuwa Sheria zetu zinazingatiwa ni
la kila mwananchi na siyo la Serikali peke yake. Kwa mfano, Serikali imetumia
fedha nyingi katika kujenga miundombinu ya barabara, kuweka nguzo za kupitishia
umeme mkubwa na vifaa mbali mbali vya kupitishia mtandao wa “e-government”
katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu. Lakini taarifa nilizonazo ni kuwa kuna
baadhi ya wananchi wenye tamaa na wanaoweka mbele maslahi yao na kwa hivyo,
wameanza kuihujumu miundombinu hii kwa namna mbali mbali zikiwemo kuchimba
mchanga chini ya nguzo kuu za umeme na kukata waya za umeme kwa ajili ya kuuza
shaba. Kadhalika, viguzo na paipu zitakazotumika kupitishia waya za mtandao
zimeanza kuharibiwa kwa namna tofauti wakati huu ambao Serikali inakaribia
kuizindua miradi hiyo muhimu kwa maendeleo yetu.
Zaidi ya hayo, katika nyakati tofauti baina ya mwezi wa Mei,
Julai na Oktoba, 2012; tumeshuhudia barabara zetu kadhaa zimeharibiwa kwa
kuchomwa moto mipira mibovu ya gari katika mji wa Unguja. Vile vile,
miti iliyopandwa pembeni mwa barabara ilikatwa matawi na mengine kung’olewa kwa
hasira na jazba zisizo na tija. Mambo yote haya yaliyofanyika
yameitia hasara Serikali. Kwa upande wake, Serikali itaendelea
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaosababisha uharibifu na kuitia
hasara Serikali.
Ndugu Wananchi,
Wakati huu tunaposherehekea sikukuu ya Eid el Hajj tayari
tumo kwenye Msimu wa mvua za Vuli. Katika wiki chache zilizopita tulianza
kuziona mvua zikinyesha kwenye maeneo machache kwa kiwango kidogo na taarifa za
utabiri, zilisema kuwa tutarajie kupata mvua nyingi. Siri halisi anayejua ni
Mwenyezi Mungu (SW). Hata hivyo, ingawa mvua bado hazijaanza kwa kasi tunapaswa
kujitayarisha hasa katika shughuli za kilimo. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo
na Maliasili tayari imeshaanza kuwahudumia wakulima kwa kuwachimbulia mashamba
yao kote Unguja na Pemba.
Katika Msimu huu, lengo letu ni kulima hekta 40,000.
Serikali imeshaagiza tani 1500 za mbolea na lita 30,000 za dawa ya kuulia
magugu. Hivi sasa kuna idadi ya matrekta 37 na tayari Serikali imeshaagizia
matrekta mapya 20 ili kuimarisha upatikanaji wa huduma zake.
Nawasihi wakulima wote wazingatie taratibu zilizowekwa na
Serikali katika kuwapatia huduma za matrekta na pembejeo nyengine za kilimo.
Serikali itajitahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizo ndani ya uwezo wake
ili kuwasaidia wakulima na kuelekea katika lengo kuu la Serikali la kuimarisha
sekta ya kilimo kwa lengo la kuyafanikisha Mapinduzi ya Kilimo nchini.
Ndugu Wananchi,
Napenda kutoa pongezi na shukurani kwa wakulima wote nchini
kwa kuhamasika kuzitumia fursa zilizowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
za kutoa ruzuku katika huduma na pembejeo za kilimo.
Pamoja na kuwepo uchache wa mvua kwa msimu uliopita, baadhi
ya maeneo hapa nchini yameonesha kunufaika na azma hiyo njema iliyowekwa na
Serikali. Zaidi ya hayo, tumeweza kupata mafanikio kwenye uzalishaji
wa mazao ya chakula zikiwemo ndizi, muhogo, viazi vitamu na vyenginevyo, mazao
ambayo yalisaidia sana kupunguza mfumko wa bei za vyakula.
Natoa wito kwa wakulima na wananchi wote wazitumie mvua za
Vuli pale zitakapokuwa zinanyesha kwa ajili ya kilimo na pia kwa ajili ya
upandaji wa miti ya misitu, biashara na matunda. Naelewa kuwa tayari kuna miche
mingi ya aina mbali mbali ya miti, katika vitalu vinavyomilikiwa na Serikali na
vile vya watu binafsi inayosubiri ichukuliwe na ipandwe mashambani.
Tutakapozitumia mvua hizi za vuli kwa shughuli za kilimo na upandaji miti
tutakuwa tumeitumia vyema neema hii aliyoturuzuku Mwenyezi Mungu na pia
tutayaimarisha mazingira yetu yanayozidi kuharibiwa. Kila mwananchi aweke azma
ya kupanda miti kabla ya kukata mti.
Kadhalika, taarifa za uwezekano wa kuwepo mvua nyingi ni
kauli ya tahadhari kwa wananchi wanaoishi mabondeni yakiwemo mabonde ya mpunga.
Wenzetu hao wanapaswa kuzingatia usemi mashuhuri wa “Tahadhari kabla ya
athari” au “kinga ni bora kuliko tiba”. Vile
vile, napenda kuzikumbusha taasisi zetu zinazoshughulikia majanga ikiwemo Idara
ya Kukabiliana na Maafa na Kikosi chetu cha Zimamoto na Uokozi kufanya
matayarisho ili tuweze kukabiliana na hali hiyo itakapotokea pamoja na
kuendelea kuwaelimisha wananchi namna bora ya kupambana na maafa.
Ndugu Wananchi,
Napenda kuwanasihi wananchi wote juu ya umuhimu wa
kuimarisha umoja na mshikamano wetu ambao ndio msingi mkubwa wa amani na
utulivu tulionao. Ni wajibu wetu tuiendeleze amani yetu na
mshikamano ambao ndiyo siri kubwa ya mafanikio tunayoendelea kuyapata.
Tuna wajibu wa kumshukuru Mola wetu (SW) kwa kuturuzuku
neema hii ambayo tumeitafuta kwa muda mrefu. Mwenyezi Mungu anatupa
habari ya jambo kama hili katika aya ya 61 ya Suratul Anfal kwa kusema:
“Na kama, wakielekea katika amani, nawe pia elekea na
mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Asikiaye na Ajuaye”.
Na pia akasema katika aya ya 63 ya sura hio hio kwamba:
“Na akaziunga nyoyo zao; hata kama ungalitoa vyote
vilivyomo ardhini usingaliweza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye
aliyewaunganisha. Hakika Yeye ni Mbora na Mwenye hekima”.
Nasi Mola wetu kwa hekima zake ameshaziunganisha nyoyo zetu
na tunaishi kwa amani. Kwa hivyo, kuishukuru neema hii, ni kuilinda
na kuiendeleza na kujiepusha na vitendo vyote vitakavyoweza kuiondosha na
kuturudisha nyuma tulikotoka.
Ndugu Wananchi,
Katika hotuba yangu niliyoitoa katika Baraza la Idd el Fitr
mwezi Mosi Mfungo Mosi mwaka 1433 Hijriya sawa na tarehe 19 Agosti, 2012;
nililizungumza kwa urefu suala la kuilinda na kuiendeleza amani, utulivu na
mshikamano wetu. Nilielezea kuwa mambo haya ndio siri kubwa ya mafanikio
yetu tunayoendelea kuyapata. Nilielezea ukweli kuhusu jamii yetu kwa
kusema kuwa ni jamii ya watu waliochanganyika sana kwa mambo mbali mbali ya
kijamii na katika maisha yetu ya kila siku. Mwisho nilielezea kwamba
katika siku za hivi karibuni nchi yetu imekabiliwa na vitisho vya kuondoka kwa
amani, utulivu na mshikamano na niliyakumbusha matukio mawili makubwa.
Tukio la kwanza ni lile la tarehe 26, 27 na 28 mwezi wa Mei
na la pili ni lile la tarehe 20 Julai, 2012. Nilisema wazi kwamba
matukio haya yameitia doa jamii yetu na nchi yetu, ambayo imejijengea sifa
nzuri ya amani na utulivu. Hatimae, nilitoa wito kwa kuwataka wananchi
wote wajiepushe na vitendo vya uvunjaji wa amani na vinavyopelekea kuwaathiri
watu na mali zao. Nilisisitiza athari ya vitendo
hivi na shughuli zetu za maendeleo na ukuaji wa uchumi hasa katika kuimarisha
sekta ya utalii na kuwakimbiza wageni wetu.
Ndugu Wananchi,
Takriban miezi miwili baada ya hotuba yangu hiyo, kwa mara
nyengine tena, hapo tarehe 17 Oktoba limetokea tukio jengine la tatu la
kusikitisha la kutaka kuivunja amani yetu. Maeneo mbali mbali ya mji wetu wa
Zanzibar yalikumbwa na vitendo vya fujo na vurugu.
Taarifa rasmi ya Serikali iliyotolewa tarehe 17 Oktoba na 24
Oktoba na zile zilizotolewa na Jeshi la Polisi baina ya tarehe 17 hadi 19
Oktoba, kufuatia vitendo hivyo, zilielezea hatua za haraka zilizochukuliwa
katika kurejesha hali ya amani. Kadhalika, taarifa hizo zilielezea
sababu za kutokea fujo na vurugu hizo, uharibifu, hasara na madhara
yaliyojitokeza siku hiyo ya tarehe 17 Oktoba, 2012.
Fujo na vurugu hizo zilipelekea kuchomwa moto kwa maskani za
CCM, kuvunjwa maduka, kuporwa kwa mali za watu na kuharibu miundombinu ya
barabara na kadhalika. Vile vile, fujo na vurugu hizo zilipelekea
kuuliwa kwa askari wetu wa polisi wa kikosi cha FFU Namba F2105, Koplo Said
Abdulrahman. Nawapa pole wafiwa, ndugu na jamaa wa marehemu, Mungu amlaze
mahala pema Peponi. Waliohusika kufanya fujo na vurugu hizo
ilisadikiwa kuwa wafuasi wa Sheikh Farid Hadi, kiongozi wa UAMSHO, wakidai kuwa
Sheikh wao haonekani na hivyo kudhania kuwa anashikiliwa na vyombo vya dola.
Hata hivyo, madai hayo kama nyote mnavyojua hayakuwa ya kweli na yalikanushwa
na Jeshi la Polisi. Na kwa hivyo vyombo vya dola havikumteka Sheikh Farid.
Ndugu Wananchi,
Napenda kukuhakikishieni wananchi nyote kwamba Serikali
itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watakaotishia amani ya nchi
yetu. Jeshi letu la Polisi na vyombo vya Ulinzi na Usalama viko
imara katika kuvidhibiti vitendo vya fujo na vurugu. Serikali
itafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kwamba wanaohatarisha usalama na
amani yetu wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Tutazitumia
sheria na taratibu ziliopo ili kuvishughulikia vitendo vya uvunjaji wa amani
vitakavyofanywa au kuchochewa na kikundi chochote. Hapana hata mtu
mmoja alie juu ya sheria, kila mtu anapaswa kufuata sheria.
Nataka niwaeleze rasmin. Serikali haitowavumilia na kwamba
ustahamilivu na uvumilivu wa Serikali umefikia kiwango cha mwisho. Hapa
tulipofika basi tena. Ni jukumu letu sote tushirikiane na Serikali katika
kuwakana na kutoa tamko zito kila mmoja wetu kwa vikundi hivyo.
Tutamshughulikia ipasavyo mtu yo yote yule atakaevunja
sheria.
Nataka nirudie tena tutamshughulikia ipasavyo mtu yo yote
atakaevunja sheria. Ustahamilivu na utulivu sio udhaifu ni heshima kubwa ya
kutii amri ya MwenyeziMungu. Wanasema wazungu ‘enough is enough’.
Kama mjuavyo hivi sasa, hatua za kisheria zimeshaanza
kuchukuliwa. Viongozi wanane wa UAMSHO wamepelekwa mahakamani. Wengine
waliokamatwa na polisi kwa kufanya fujo nao pia wameshafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, Jeshi letu la Polisi na vyombo vya Ulinzi na Usalama
vinaendelea na doria katika mitaa mbali mbali ili kuhakikisha kuwa wananchi
wanaishi kwa amani. Mali za watu na maisha yao yataendelea kulindwa. Wageni
wetu wanahakikishiwa usalama wao na pia mazingira mazuri ya utalii yataendelea
kuwepo.
Ndugu Wananchi,
Ninakuombeni sana kwamba nyote muendelee kuwa wastahamilivu
na wenye subira ili kwa pamoja na Serikali yenu tuendelee kushirikiana katika
kuidumisha amani katika nchi yetu. Jeshi letu la Polisi na vyombo
vyetu vya Ulinzi na Usalama vitaendelea kuimarisha ulinzi. Kwa mara
nyengine tena nawasihi wale wananchi wachache wenye nia ya kufanya fujo na
vurugu, waache kujiingiza kwenye vitendo hivyo. Kwani kufanya
vitendo hivyo ni kufanya kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitowavumilia
kwani ina wajibu wa kusimamia sheria na kuwalinda wananchi wote.
Kwa dhati kabisa, ninakupongezeni wananchi wote kwa
uvumilivu na ustahamilivu wenu. Kadhalika, ninalipongeza Jeshi letu la Polisi
na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuilinda
amani ya nchi yetu.
Nachukua fursa hii kutoa pole kwa wananchi wote waliopoteza
mali zao au kupata athari ya aina yo yote ile kutokana na fujo na vurugu hizo.
Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia nasaha zangu, napenda kuipongeza Kamati ya
maandalizi kwa matayarisho na utaratibu mzuri wa sherehe hizi za Idd el Hajj.
Kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wananchi wote kwa
ushirikiano wenu, ihsani, mapenzi makubwa na insafu mnayoionesha katika
kuisherehekea sikukuu hii. Tumuombe Mwenyezi Mungu azidi kuulinda umoja wetu na
atuwezeshe kuisherehekea Idd hii na nyengine kwa salama na amani. Atuzidishie
neema za kila aina nchini mwetu na atujaaliye mvua zenye kheri na baraka ya
mazao mengi.
Kwa baraka ya siku hii, Allah awajaaliye afya njema wagonjwa
wetu na wazee wetu walioko majumbani na hospitalini. Tunamuomba Mwenyezi Mungu
awape safari njema ya kurudi nyumbani mahujaji wetu na wakubaliwe Hijja yao na
sisi aturejeshe majumbani kwa salama. Awarehemu na awasamehe makosa yao wazee,
ndugu, jamaa na waislamu wote waliotangulia mbele ya haki. Awape malazi mema
Peponi na sisi tulio hai atupe khatima njema na kwa pamoja tuwe miongoni mwa
waja wake wema siku ya Kiama - Amin.
Nawasihi watumiaji wa vyombo vya barabarani kuchukua hadhari
zaidi na kujali usalama. Aidha, wazazi wawe waangalifu kwa watoto
wao katika siku hizi za sikukuu.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Idd Mubarak
Kullu Aam Waantum Bikheir.
Imewekwa na MAPARA
No comments:
Post a Comment