WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, October 16, 2012

Maalim Seif Sharif Hamad ahutubia Nungwi


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara huko Nungwi.
  Maalim Seif akikabidhi jezi na mipira kwa timu za mpira wa miguu jimbo la Nungwi
 Wanachama, wapenzi na wananchi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa CUF alipokuwa akiwahutubia kwenye mkutano wa hadhara Nungwi


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema mamlaka kamili ya Zanzibar yatapatikana kwa kila Mzanzibari kuhakikisha anaweka mbele mapenzi yake kwa nchi yake na kuweka kando itikadi ya chama chake cha siasa.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara huko Nungwi, mwishoni mwa wiki iliyopita, Maalim Seif alisema vyama vya siasa huanzishwa na baadaye kuondoka, lakini Zanzibar itaendelea kuwepo, hivyo Wazanzibari wote waone ni jukumu lao kuhakikisha ni yenye mamlaka kamili iliyostawi kiuchumi na maendeleo ya watu wake. 
“Tulikuwa na ASP, Hizbu, Umma Party, ZPPP na vyenginevyo, leo vipo... Zanzibar ipo haipo? Zanzibar imekuwepo hata kabla ya Tanganyika, Uganda na Kenya na Inshaallah itaendelea kuwepo mpaka kiyama” alieleza.
Alisema hakuna mtu anayechukia Muungano, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba Muungano wetu ni wa ‘Mkubwa na Mdogo’, hali ambayo matokeo yake ni kila siku zinavyokwenda mbele Zanzibar ndiyo inayoathirika zaidi katika nyanja tafauti.
“Mimi ni mwanachama wa CUF, ni muasisi wa CUF, naipenda sana CUF, lakini ukinipasua moyoni damu yangu itajiandika ‘Zanzibar’. Sote tunatakiwa tuwe Wazalendo wa Zanzibar, nchi kwanza vyama baadaye”, alisema Maalim Seif. 
Maalim Seif alisema baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaodai Muungano huu uliopo sasa ni mzuri inawezekana wanasema hivyo kwa sababu wananufaika wao binafsi, lakini Muungano huo tokea mwaka 1964 umekuwa na matatizo mengi na makubwa, ambayo matokeo yake ni kudhorotesha uchumi na hadhi ya Zanzibar.
Alisema juhudi kubwa zimechukuliwa kutatua kasoro zilizopo na sasa ni zaidi ya miaka 48, lakini kama kwamba zimezidi kuongezeka, na kuhimiza wakati ndio huu wananchi wa Zanzibar kuweka kando itikadi zao za vyama vya siasa na kuhakikisha wanapata mfumo wa Muungano ambao hautaibana Zanzibar katika kujiamulia mambo yake kwa namna yoyote ile.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara huko katika viwanja vya Nungwi Sokoni, Maalim Seif alikagua miradi ya barabara za ndani katika jimbo la Nungwi zilizojengwa na viongozi wa jimbo hilo, wakiongozwa na Mwakilishi wa Nungwi, Haji Mwadini Makame na Mbunge Yussuf Haji Khamis.
Pia alikabidhi vifaa mbali mbali, vikiwemo kwa ajili ya miradi ya maji safi na salama katika vijiji vilivyopo ndani ya jimbo hilo pamoja na kukabidhi kadi kwa wanachama wapya waliojiunga na chama cha CUF.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisifu juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na viongozi wa jimbo la Nungwi kwa mashirikiano na wananchi, na kuzielezea hatua hizo kuwa ni mfano wa kuigwa na viongozi wa wananchi katika maeneo mengine.
“Viongozi wa jimbo hili wanatekeleza kikamilifu sera za Chama cha Wananchi CUF za kuwaondolea shida wananchi, ni imani yangu kuwa iwapo watapata mashirikiano mazuri kutoka Wilayani, Mkoani na Halmashauri watafanya mambo makubwa zaidi na matatizo mengi ya wananchi wa Nungwi yataondoka kabisa”, alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.
Mapema wananchi wa kijiji cha Mvuleni jimboni humo, walimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa wamefarajika sana kupata barabara hiyo inayokwenda hadi kijijini kwao, kwa sababu kwa muda wote tokea kuwepo kijiji hicho walikabiliwa na shida kubwa ya usafiri, ikiwemo pale inapotokea haja ya kuwawahisha wagonjwa kupatiwa matibabu. 

Source Vijimambo Blog

No comments:

Post a Comment