WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, October 16, 2012

Walimu watoboa mahusiano ya mwenzao, RPC Barlow



 *Viapo vya kisasi vyatawala
 *Mwili wapelekwa Dar

Aliyekuwa RPC wa Mwanza, Leberatus Barlow
Baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Nyamagana wamevunja ukimya na kueleza kile kinachodaiwa ni mahusiano kati ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Leberatus Barlow, na mwalimu mwenzao, Dororth Moses.

Wakizungumza na NIPASHE shuleni hapo jana, pia walielezea kusikitishwa kwao na jinsi tukio hilo la mauaji ya RPC lilivyotokea mbele ya mwalimu mwenzao, Doroth Moses aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi eneo la Kitangiri, jijini Mwanza.

Mwalimu Doroth ndiye aliyekuwa na RPC Barlow ndani ya gari wakati watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walipowavamia na kumuua kwa kumpiga risasi Kamanda huyo.

Katika mahojiano hayo Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Mary Ngalula, alisema wanamuonea huruma mwalimu mwenzao kutokana na kushuhudia tukio hilo la kutisha.

Alisema wanamsikitikia kwa sababu jamii imeanza kumfikiria vibaya kwa kudhani anahusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.
“Tunamuonea huruma mwalimu mwenzetu kutokana na maneno tunayoyasikia, lakini sisi tuko pamoja naye kwa sababu tunamfahamu ni mtu safi, na hivi tunajiandaa kwenda kumuona na kumtia moyo ili amudu kuilea familia yake kwani ni mjane,” alisema.
Mwalimu Baraka Magafu alisema tofauti na hisia za baadhi ya watu kuhusu uhusiano wa Mwalimu Doroth na Kamanda Barlow, wao (walimu) wanafahamu kuwa ni watu wa kabila moja wanaotoka kijiji kimoja huko Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Alibainisha kuwa Mwalimu Doroth amekuwa ni mtu anayejihusisha sana na shughuli mbalimbali za watu wa kabila lake (Wachaga), hivyo hakuna sababu ya kumfikiria vibaya kwa sababu tu mtu aliyekuwa amemsindikiza nyumbani wakitokea kwenye kikao cha maandalizi ya harusi aliuawa kwa kupigwa risasi.
“Ukifuatilia mwenendo wa tukio lote, utaona kwamba kilichotokea ni bahati mbaya na kingeweza kumtokea yeyote, kwani Barlow alikuwa akimsindikiza Mwalimu Doroth nyumbani kwake, na hata baada ya tukio, alipowapigia simu wenzao waliokuwa nao kwenye kikao walikuwa ndipo na wao wanafika majumbani mwao,” alisema.
Aliongeza kwamba katika mazingira kama hayo ni makosa kuwa na mtazamo hasi dhidi ya Mwalimu Doroth kama ambavyo baadhi ya watu wameanza kuvumisha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Wakati huo huo, majonzi, simanzi na kauli za kulipa kisasi ni miongoni mwa mambo yaliyogubika shughuli ya kuuaga mwili wa  Barlow.
Mwili wa Barlow uliagwa na wakazi wa Jiji la Mwanza wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, katika shughuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana jana.
Baada ya shughuli ya kuagwa mwili wa Barlow, ulisafirishwa baadaye jana jioni kwa ndege kuelekea jijini Dar es Salaam kabla ya leo kusafirishwa kwenda kijijini kwake Vunjo, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.

WAZIRI LUKUVI
Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wakazi wa Jiji la Mwanza waliojawa na majonzi, Waziri Lukuvi alisema Jeshi la Polisi halijafilisika kwani wapo makamanda wa kutosha ambao wataendeleza mapambano aliyoyaanzisha Kamanda Barlow.

RC MWANZA: TUKO VITANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alisema hivi sasa vyombo vyote vya dola vipo kazini vikifanya uchunguzi wa tukio la mauaji hayo na kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni haraka iwezekanavyo.
“Leo Kamanda na jemedari wetu katika mapambano dhidi ya uhalifu ameondoka, lakini nataka niwahakikishie kwamba tupo vitani, hatupaswi kuweka silaha chini, kama mkoa tuweke silaha zetu vizuri hadi ushindi utakapopatikana,” alisema.
Aliongeza kwamba jamii ya Mwanza na Tanzania kwa ujumla iwe na imani kuwa waliohusika na mauaji ya Barlow hawako salama, kwani lazima watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Naomba niwahakikishie kwamba vyombo vyote vya dola viko kazini, waliotenda mauaji haya hawako salama, watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na jambo hili litafikia tamati mapema iwezekanavyo,” alisisitiza Ndikilo.

DCI MANUMBA
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, aliwaambia waombolezaji kwamba taarifa ambazo Jeshi la Polisi limezipata kutoka kwa wananchi zimeongeza kasi ya upelelezi wa mauaji hayo. Aliwataka askari kuwa watulivu katika kipindi hiki cha majonzi lakini akawataka kulipa kisasi dhidi ya mauaji ya RPC Barlow kwa kuhakikisha wanawakamata wote waliohusika.
“Umma utambue kwamba hatutalala hadi tuwatie mbaroni wauaji, na hii inapaswa kuwa ndiyo kawaida yetu kuhakikisha uhalifu wa aina yoyote unashughulikiwa kwa uzito ule ule kama tunavyofanya hivi sasa katika mauaji ya RPC Barlow,” alisema Manumba.

RPC WA MARA
Akitoa salaam za rambirambi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema  kama kuna wananchi wenye taarifa za watu waliohusika na mauaji hayo wampelekee yeye na atazifanyia kazi.
“Ningependa kuwaambia wananchi wenye taarifa za mauji ya RPC Barlow kama wanaona shida kuzipeleka kwingine waniletee mimi tutazifanyia kazi,” alisema Mwakyoma ambaye alimfananisha Barlow sawa na kitabu cha marejeo (encyclopedia) kutokana na jinsi alivyokuwa akimsaidia kutatua masuala mbalimbali.

RPC KAGERA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, alisema idadi ya wahalifu ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya raia wema, hivyo ana imani wakiunganisha nguvu ushindi utapatikana.

RPC SIMIYU
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alisema Jeshi la Polisi halitakata tamaa kupambana na wahalifu licha ya Kamanda Barlow kuuawa.

RPC GEITA, TABORA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Lenard Paul na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Anthony Ruta, katika salaam zao za rambirambi walisema kwamba 
Jeshi la Polisi limepoteza Kamanda shupavu, mkweli, mweledi na mwalimu kwa makamanda wengine.

SALAMU ZA CCM
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, alisema Kamanda Barlow alizingatia sana sheria katika utendaji wake wa kazi na alikuwa tayari kuitika wito hata kama ni usiku wa manane.

SALAMU ZA CHADEMA
Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Carlos Majura, alisema kifo cha Barlow ni pigo kwa wapenda amani wote, hivyo wananchi watumie nguvu ya umma kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

POLISI WAFICHUA MAPYA
Wakati huo huo habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Kitengo cha Upelelezi zimeeleza kwamba simu ya upepo (radio call) ndiyo iliyomponza Kamanda Barlow na kumsababishia kifo. Mmoja wa maofisa upelelezi ambaye hata hivyo, hakupenda jina lake litajwe, alisema baada ya Kamanda Barlow kuwa amemfikisha Mwalimu Doroth nyumbani kwake, walitokea watu wawili waliokuwa na tochi ambao walimtaka azime taa za gari, lakini yeye (Barlow) akagoma.
 Alibainisha kuwa upelelezi zaidi unaonyesha kwamba walipomsogelea walimlazimisha azime taa za gari, lakini aliendelea kushikilia msimamo wake huku akiwaambia kuwa yeye ni RPC.
Aliendelea kusema kwamba ghafla walitokea watu wengine takribani watatu ambao inaonekana bado hawakuamini kama kweli huyo ni RPC, lakini alipotoa radio call ili kufanya mawasiliano ndipo walipomfyatulia risasi na kumuua.

JK ATUMA RAMBIRAMBI
Rais Jakaya Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa mno na mauaji ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, yaliyotokea usiku wa kuamkia Jumamosi jijini Mwanza.
Katika salamu za rambirambi alizompelekea Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspeka Jenerali Saidi Mwema, Rais Kikwete ameagiza jeshi hilo kuhakikisha linachukua hatua za lazima kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria watu wote wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji hayo.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ACP Liberatus Barlow kilichotokea usiku wa Ijumaa katika Jiji la Mwanza ambako watu wasiojulikana walimpiga risasi na kumwua ofisa huyo mwandamizi wa Jeshi letu la Polisi.
“Historia ya ACP Barlow ni historia ya mfano katika utumishi wa umma na hususan katika Jeshi la Polisi. Kwa hakika, Jeshi la Polisi limempoteza kamanda hodari na wananchi wa Tanzania, hususani wale wa Mkoa wa Mwanza, wamempoteza mlinzi shupavu wa usalama wao na mali zao,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:
“Nakutumia wewe IGP salamu zangu za rambirambi kufuatia mauaji hayo. Kupitia kwako nalitumia Jeshi zima la Polisi pole zangu kwa kuondokewa na mwenzao na katika mazingira yenye kutia uchungu sana. Aidha, kupitia kwako, naomba uniwasilishie salamu zangu za dhati kwa familia ya ACP Barlow ukiwajulisha kuwa niko nao katika wakati huu mgumu sana. Naungana nao katika kuomboleza kifo cha baba yako na mhimili wa familia yao na katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amen.”
Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kulitia moyo Jeshi la Polisi kwa kusema: “Kitendo hiki ni kazi ya watu waoga, lakini nawasihi kitendo hicho kisiwakatishe tamaa katika kutekeleza wajibu wenu na kufanya kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya katika nchi yetu ya kulinda usalama wetu na mali zetu.”
 Aliongeza: “ Badala yake kitendo hiki cha woga kiwahamasishe kuongeza kasi ya kudumisha usalama wa nchi yetu. Na kwa kuanzia, tuhakikishe kuwa wote walioshiriki katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.”

MWILI KUAGWA LEO DAR
Mwili wa marehemu Barlow utaagwa leo kuanzia saa tano asubuhi katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Augustine Ukonga, jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Kilema, Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho mchana kwa kufuata taratibu za kidini na kuhitimishwa na taratibu za kijeshi.
Taarifa iliyotolewa Jana na Jeshi la Polisi Makro makuu ilieleza kuwa taarifa zitaendelea kutolewa mara kwa mara kadiri ya mipango itakavyokuwa inaratibiwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment