HOTUBA
YA MKURUGENZI WA MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA OFISI YA ZANZIBAR, KWA
WAHARIRI NA WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR 03/10/2012
Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa NIDA. Vuai Mussa Suleiman.
Ndugu Wahariri na waandishi wa habari
Maafisa toka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
Mabibi na Mabwana,
Assalamu - alaykum
Utangulizi
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutuwezesha kukutana
hapa tukiwa na afya njema katika kushirikishana hatua muhimu katika utekelezaji
wa jambo muhimu la kihistoria katika mustakabali wa Nchi yetu, kwa kuanza
mchakato wa usajili na Utambuzi wa watu, unaolenga hatimaye kutoa vitambulisho
vya Taifa.
Ni wazi wazo la kuwa na Vitambulisho vya Taifa limechukua muda mrefu sasa na
kwa muda mrefu serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kuwa jambo hili
linakamilika na mchakato unaanza. Na leo ndugu wanahabari, naomba kuwajulisha
Usajili wa wananchi kwa upande wa Zanzibar unaanza rasmi 15/10/2012 baada ya
kukamilika kwa usajili wa watumishi wa Umma.
Kwa hakika tuna kila sababu ya kuipongeza serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kwa namna ya pekee, sekikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
chini ya Rais wetu Mheshimiwa Ali Mohamed Shein. Kwa hakika jitihada kubwa
mlizozifanya kuhakikisha mradi huu unafanikiwa na kutekelezeka mnapaswa
kupongezwa.
Ndugu Wanahabari,
Zanzibar tunakusudia kuanza shughuli ya usajili na utambuzi wa Watu rasmi kama
hakutakuwa na mabadiliko yeyote tarehe 15/10/2012 na utaratibu tuliojiwekea ni
kusajili kiwilaya na kila Wilaya imepangiwa siku 10 za usajili.
Ni imani yangu kubwa wananchi, Viongozi wa dini, masheha na wanasiasa kwa
jumla, tutatoa ushirikiano kwa maafisa wetu wasajili ambao watakuwa katika kila
shahia kufanya usajili, na kila mmoja wetu aone ana jukumu kubwa la kulipa
kipaumbele suala hili kwani ni kwa maendeleo yetu na kwa mstakabali wa Taifa
letu.
Ratiba ya wilaya itakayoanza mpaka kuhitimisha, tutaitoa katika vyombo vya
habari ili kila mtu kufahamu ratiba yake na kujiandaa kwa usajili.
UNGUJA
WILAYA
TAREHE
WILAYA
TAREHE
WILAYA
TAREHE
Kusini
15–26/10/2012
Kati
29/10 – 09/11/2012
Magharibi
12 – 23/11/2012
Mjini
26/11 – 07/12/2012
Kask B
10 – 21/12/2012
Kask A
24/12/2012 – 04/01/2013
PEMBA
Mkoani
07 -18/01/2013
Micheweni
21/01 – 01/02/2013
Wete
04 – 15/02/2013
Chake Chake
18/02 – 01/03/2013
Vitambulisho hivi vitatolewa kwa makundi makuu matatu, wananchi kwa ambao ni
raia, wageni na wakimbizi. Hapa kwetu Zanzibar tunaishi na wageni na hata
wakimbizi. Rai yangu wote wajitokeze kujisajili kwa kufuata taratibu na
sheria za nchi, na tusikubali kupindisha sheria kutoa kitambulisho
cha uraia kwa wageni kwani sote tunafahamu madhara yake, na umuhimu wa kila
kundi kupewa kitambulisho chake kwa kadiri ya stahiki zake.
Ndugu zangu tukifanya makosa katika hili la kitambulisho tutajikuta nchi yetu
kesho ikitawaliwa na wageni..tujifunze kwa yaliyotokea kwa wenzetu, Tanzania
yasitukute.
Ndugu Wanahabari,
Zipo faida nyingi sana za kuwa na kitambulisho cha Taifa, kama ilivyo kwa
kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.
Wengi wetu tutakuwa tukijiuliza mfumo huu wa Utambuzi na usajili wa watu
utakuwa na faida gani kwetu kama Taifa na kama wazanzibari?
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipata hasara nyingi kwa kushindwa
kuwatambua watu wanaishio nchini kutokana na kutokuwa na mfumo wa utambuzi na
usajili wa watu Kitaifa. Baadhi ya hasara hizo ni kama zifuatavyo:-
1. Wananchi kuendelea kuwa katika umasikini kwa kushindwa
kupata mikopo katika benki na taasisi za fedha. Faida ya zoezi
hili, ni kuwasaidia wananchikujikwamua kiuchumi. Aidha, baadhi ya benki
zimekuwa zinatoza riba kubwa kufidia hasara wanayoipata kutokana na baadhi
ya watu kutorudisha mikopo kwasababu hawatambuliki.
2. Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa inapata
matatizo na malalamiko mengi kwa kushindwa kumtambua mwanafunzi yupi
anastahili mkopo na kwa kiasi gani. Aidha, urudishwaji wa mikopo hii
umekuwa ni mgumu kwa kushindwa kuwapata wadaiwa mara baada ya kumaliza vyuo
na hivyo kuingizia hasara Serikali. Sasa kitambulisho cha Taifa
kitawezesha vijana wengi zaidi kupata mikopo ya elimu ya juu na hivyo kutoa
fursa kwa vijana wengi zaidi kuendelea kimasomo
3. Kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na hasa unaofanywa na raia
kutoka nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa
msamaha waRais. Ni wazi kuwa udhibiti wao umekuwa mgumu kutokana na
kushindwa kuwatambua.
4. Kuongezeka kwa mrundikano wa wafungwa katika magereza
mbalimbali kutokana na kutokuwepo kwa udhibiti wa wafungwa wa kifungo cha
nje.
5. Serikali imeendelea kubeba mzigo mkubwa wa gharama wakati
wa zoezi la kupiga kura. Kwakuwa na kitambulisho cha Taifa, kutapunguza
gharama kubwa za kuhuisha daftari la wapiga kura kila inapohitajika
6. Serikali imekuwa inapoteza fedha nyingi kila mwaka kwa
kulipa watumishi hewa katika mfumo wa mishahara ya watumishi wa Serikali.
Sasa kwa kuwa na daftari lenye kumbukumbu sahihi za watu, serikali itadhibiti
upotevu wa fedha nyingi ambazo wamekuwa wakilipwa watumishi hewa kwani
hawatambuliki
7. Pamoja na hayo, Serikali imekuwa inapata matatizo na
kuingia migogoro na wananchi wakati wa mazoezi ya kuwalipa fidia kutokana
na kuchukua ardhi au kubomolewa nyumba zao kwa sababu ya kushindwa
kumtambua mmiliki sahihi na anachokimiliki.
8. Mfumo huu pia utarahisisha na kuwawezesha vijana na watu
wengi zaidi kuweza kumiliki hati ya kusafiria (Passport) tofauti na hali ilivyo
sasa ambayo inalazimu mwombaji kuwa na vielelezo vingi kutokana na
kutotambuana. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha Mfumo
huu wa Vitambulisho vya Taifa kwa sababu mbali mbali ikiwa ni pamoja na hizi
zifuatazo:
1. Kuweza kuwatambua raia na wageni waishio Tanzania.
2. Kusaidia kumtambua mhusika anapohitaji kupatiwa huduma
katika Taasisi mbalimbali kama vile benki, taasisi za mikopo na huduma za
afya.
3. Kumtambua mtu pale anapofanya uhalifu wa aina fulani. Jambo
hili litasaidia sana katika kupambana na uhalifu.
4. Kuwatambua wakwepaji wa kurejesha mikopo kutoka kwenye
benki mbali mbali nchini.
5. Kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari.
6. Kumtambua mtu anapofanya biashara au shughuli nyingine kwa
kutumia majina tofauti.
7. Kuhakikisha kuwa mtu anapata stahili zake za jamii. Kwa
mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu, haki za kujiunga
na masomo ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo raia wa
Tanzania anastahili.
8. Kusaidia katika kuondoa watumishi hewa kwenye
"payroll" ya Serikali.
9. Kuimarisha utendaji kazi Serikalini kwa kuwa na kumbukumbu
sahihi za watumishi na malipo ya stahili zao, hasa pale wanapostaafu.
10. Kurahisisha zoezi la kuhesabu watu (sensa).
11. Kurahisisha zoezi la kutengeneza daftari la wapiga kura.
12. Kwakuwa kitambulisho hiki kitakuwa cha teknolojia ya hali ya juu
yaani (smart Card) na kuweza kuhifadhi taarifa nyingi za mtu binafsi zikiwemo
taarifa za kibailojia, Kitambulisho cha Taifa kitasaidia kutambua watu
panapotokea majanga kama vile ajali n.k na kurahisisha upatikanaji wa huduma
kwa haraka.
Ndugu wanahabari,
Shughuli hii ni mtambuka kwa maana ina mgusa kila mtu kwa nafasi yake, hivyo
sitegemea zoezi hili kuchukuliwa kuwa la kisiasa, kidini au kikabila, kwani
lina linda maslahi ya kila mmoja wetu. Huu sasa ni wakati wa kujenga umoja wa
Kitaifa. Na maamini Watanzania kwa hili tunaweza, na wazanzibari tutaonyesha
mfano.
Rai kwa Wananchi wote
Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Wananchi wote na wakazi wa
Zanzibar mnaoishi kihalali kujiandaa na kujitokeza katika shughuli
hii kwa kuhakikisha kuwa wale wote wenye umri wa miaka 18 na zaidi wanaandaa na
kutunza nyaraka zote muhimu zenye kumbukumbu zao binafsi ili kurahisisha
ushiriki wao katika zoezi hili kama watakavyoelekezwa.
Vyombo vya habari tunawaomba ushiriki wenu wa karibu
katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa
wakati ili wasipoteze fursa hii muhimu kwao ikiwa ni haki yao msingi kama raia.
Pia, napenda kutoa wito kwa Taasisi zote za serikali wakiwemo wadau wote muhimu
wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambao ni RGO, ZAN-ID,
UHAMIAJI na TAMISEMI tushirikiane kwa pamoja ili wananchi wote na wageni
wanaoshi nchini kihalali kusajiliwa.
Mwisho NIDA inawahakikishia wananchi wote, usiri mkubwa wa taarifa
zitakazotolewa na utunzaji wa taarifa hizo muhimu wakati wote wa zoezi hili,
mpaka kupatokana kwa Vitambulisho.
Asanteni sana kunisikiliza.
Vuai Mussa Suleiman,
Mkurugenzi
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
Zanzibar.
03/10/2012
Source: http://www.wavuti.com
WILAYA
|
TAREHE
|
WILAYA
|
TAREHE
|
WILAYA
|
TAREHE
|
Kusini
|
15–26/10/2012
|
Kati
|
29/10 – 09/11/2012
|
Magharibi
|
12 – 23/11/2012
|
Mjini
|
26/11 – 07/12/2012
|
Kask B
|
10 – 21/12/2012
|
Kask A
|
24/12/2012 – 04/01/2013
|
PEMBA
|
|||||
Mkoani
|
07 -18/01/2013
|
Micheweni
|
21/01 – 01/02/2013
|
Wete
|
04 – 15/02/2013
|
Chake Chake
|
18/02 – 01/03/2013
|
No comments:
Post a Comment