Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba (aliyesimama) akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliotishwa na Tume hiyo jana
jumapili tarehe 14. Oktoba, 2012 katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza hilo mjini
Zanzibar, uliolenga kukusanya maoni ya Wajumbe hao kuhusu mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba. Kutoka kulia ni Wajumbe wa Tume hiyo, Profesa Paramagamba
Kabudi, Suleiman Ali, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Abdalla
Ali, Mjumbe wa Tume Joseph Butiku, Katibu wa Tume Assaa Rashid na Naibu Katibu
Casmir Kyuki.
Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amembana Mwakilishi wa Jimbo
la Mji Mkongwe Mkongwe (CUF), Ismail Jussa aeleze kuhusu mfumo wa
uendeshaji wa Muungano wa mkataba unavyopaswa kuwa na mgawanyo wake wa madaraka
.
Jaji Warioba alichukua hatua hiyo baada ya Jussa kusimama
na kutoa maoni ya kutaka mfumo wa Muungano wa mkataba, wakati Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikichukua maoni ya Wawakilishi mjini Zanzibar
jana.
Alimtaka Jussa atoe mfano angalau mmoja au miwili ya uendeshaji wa
serikali ya mkataba ili Tume yake ipate ufahamu katika mapendekezo yake.
Jussa alisema anayo mifano zaidi ya 100 lakini akadai wakati ukifika
serikali zinazohusika zitakaa na kuja na fomula ya mgawanyo huo pamoja na
uendeshaji wake kimadaraka.
Hata hivyo, Jaji Warioba kwa upande wake akionekana kutoridhika
na maelezo hayo ya Jussa alimtaka kuiambia Tume alivyojiandaa na
Muungano wa mkataba kinyume na mfumo dola uliopo.
“Bwana Mwakilishi hebu tupe lau mfano mmoja au muundo wa uendeshaji wa Muungano
wa serikali ya mkataba ili uweze kukidhi haja yako na kutuonyesha njia” alisema
Jaji Warioba.
“Hebu tuweke wazi juu ya utashi wa mpango unaofikirika wa kuwa wa serikali
ya mkataba, nafikiri unachokusudia ni kutaka kuvunja Muungano uliopo”
alisemaWarioba.
Hata hivyo, Jussa alibaki katika msimamo wake huku akisisitiza kuhusu
kukaa kwa serikali mbili na kutoa mfumo wa uendeshaji wa serikali ya mktaba.
Akifafanua, Jaji Warioba alisema kimsingi kudai Zanzibar iwe na
mamlaka kamili, huku Tanganyika nayo ikiwa na mamlaka yake ni sawa na kuvunja
muungano kwa kuwa kila upande utalazimika kuwa na kiti Umoja wa Mataifa (UN).
“Tanganyika na Zanzibar zikiwa kila moja ina mamlaka yake hakutakuwa na neno
Muungano, ndiyo maana nasema nisaidiwe juu ya kupata mfumo wa kuendesha
Muungano unaotakiwa chini ya mkataba” alisema Jaji Warioba.
Akiwekea mkazo katika hoja iliyotolewa na Jaji Warioba, mmoja wa
Makamishna wa Tume hiyo, Paramagamba Kabudi, alisema inasikitisha kuona hadi
sasa wanaotaka Muungano wa mkataba wanashindwa kutoa rasimu ya mfano wa
serikali ya mkataba ili kuisaidia Tume juu ya kile wanachokitetea.
Wakitoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wa CCM na CUF waligawanyika pande mbili huku wale wa CCM wakitetea
mfumo wa serikali mbili na wa CUF wakitaka Muungano wa mkataba.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha alisema muundo
wa Muungano wa serikali mbili ndiyo muafaka kwa kuwa umeonyesha faida katika
masuala ya ulinzi na usalama lakini pia ukijenga umoja wa kitaifa.
Akishauri Nahodha alisema hata hivyo ni vyema ikafika mahali kukawa na mabunge
mawili , moja dogo litakaloshughulikia mambo ya Muungano na jingine
lishughulikie mambo ya Tanganyika.
Aidha alitaka nafasi ya Rais wa Muungano itolewe kwa zamu kila upande uwe na
kipindi cha miaka kumi.
“Mgawanyo wa mapato usiangalie idadi ya watu kwa vile hata kama Serikali moja
ikiwa na watu wawili bado ina jukumu la kuwapatia maisha bora na huduma
wananchi wake” alisema.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar Said Ali
Mbarouk alisema mfumo wa sasa wa Muungano una matatizo kwakuwa kuna mambo
ambayo si ya Muungano lakini yanasimamiwa na Muungano kinyume na makubaliano ya
mwaka 1964.
Aliyataja baadhi ya mambo aliyodai yanayoleta mkanganyiko kuwa ni utalii,
maliasili, habari na michezo ambayo alisema yanahitaji kuwekewa utaratibu na
kuzungumziwa kwake katika medani za kimatifa.
Waziri asie na Wizara Maalum Machano Othman Said alitaka mfumo wa Muungano wa
sasa uendelee na kutaka Rais wa Zanzibar kubaki kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamed Raza alitaka Rais wa Zanzibar awe na mamlaka
sawa na Rais wa Muungano pamoja na Zanzibar kupata nafasi ya kujiunga na
jumuiya ya OIC na nyingine za kiuchumi duniani.
Tume ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni inayoongozwa na
Jaji Warioba ipo visiwani Zanzibar na tayari imekutana na wananchi
katika mikoa ya Kaskazini Unguja na Pemba.
Source: http://www.wavuti.com/
No comments:
Post a Comment