WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, October 7, 2012

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR


HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI KATIKA UTARATIBU WA VIONGOZI KUKUTANA NA WAANDISHI KILA BAADA YA MIEZI MITATU KUZUNGUMZIA UTENDAJI SERIKALINI HUKO HOTELI YA GRAND PALACE MALINDI MJINI ZANZIBAR TAREHE 6 OKTOBA 2012


Waheshimiwa Waandishi wa habari
Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuweka katika hali ya uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia utendaji na majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika serikali yetu ya awamu ya saba ya uongozi ambayo imetimiza takriban miaka miwili sasa.
Pili natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari mliotenga muda wenu kuja kuhudhuria kwa wingi kuitikia wito wetu wa kutusikiliza, na baadaye kupata fursa ya kuomba ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii ya Wazanzibari kwa jumla.

Waheshimiwa Waandishi wa habari
Nianze sasa, kuzungumzia mafanikio kwa jumla tuliyoweza kuyapata na changamoto tunazokabiliana nazo katika kipindi hichi cha mwaka wa pili wa serikali ya awamu ya saba. Waheshimiwa katika nchi yetu tunaendelea kujivunia hali ya amani na utulivu katika nchi yetu ya Zanzibar. Wananchi wote wanapata fursa na uhuru wa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na kuendeleza mshikamano miongoni mwao. Hali hii hatuna budi kudumisha kwa kuenzi misingi ya maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Novemba 5, mwaka 2009 na baadaye kuwa msingi wa kupatikana serikali hii shirikishi yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Kutokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani, utulivu na maelewano, wananchi wamekuwa wakiitumia kikamilifu fursa na neema hiyo kushiriki katika shughuli za kujieletea maendeleo, ambapo pia serikali inaendelea kusimamia majukumu ya wananchi kikamilifu, ikiwemo kukuza uchumi wake kwa mintaarafu ya kuwapunguzia wananchi ugumu wa maisha yao.

Katika mwaka 2011 uchumi wetu ulikuwa kwa asilimia 6.8 huku matarajio katika mwaka huu wa 2012/2013 yakionesha dalili njema kutokana na tulivyojipanga, ambapo uchumi huo unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.5. Vile vile pato la Mzanzibari limekuwa kutoka T.SHS 782,000 kwa mwaka hadi kufikia TSHS 960,000 ambazo ni sawa na dola za Marekani 615 kutoka 560 mwaka 2010.

Kwa vyovyote vile, bila ya kuwepo hali ya amani na utulivu na maelewano miongoni mwetu tusingeweza kujenga imani kwa wawekezaji vitegauchumi ambao hadi sasa wanaendelea kujitokeza kwa wingi na kutuunga mkono kwa kuwekeza miradi yao. Bila shaka hali hiyo inatokana na kuridhishwa kwao na amani na utulivu uliopo.
Hata hivyo, lazima tukiri kuwa bado tunayo kazi nzito mbele yetu ya kuzidisha bidii kwa kila mmoja wetu, kuiunga mkono serikali katika kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu na kusaidia kukuza kasi ya kuimarika uchumi wetu.

Kwa kufanya hivyo ndipo tutaweza kuyafikia malengo ya Milenia, ambapo nchi zote zinatakiwa ifikapo mwaka 2015 pato la wananchi wake liwe limefikia T.SHS 884,000. Hata hivyo tunapaswa kuzidi kuwajengea matumaini wananchi wetu, ambao wanaamini hali ya kukua kwa uchumi wa nchi, haina budi kuambatane na fedha kuonekana mifukoni na sio kwenye makaratasi.

Sekta za Kilimo, Biashara na Huduma zimeendelea kupewa msukumo mkubwa na kuendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi na mapato ya wananchi wetu. Kwa mfano katika Huduma, utalii umeendelea kutoa mchango wa kipekee katika uchumi wa Zanzibar. Sekta hii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni na asilimia 70 ya wananchi wetu wanafaidika katika sekta hii kwa njia moja ama nyengine.

Mwelekeo wa Serikali yetu ni kuzidi kuiimarisha sekta hii ya Utalii, ili iendelee kutoa mchango mkubwa zaidi kwa wananchi. Na katika kuhakikisha lengo hilo tunalifikia, hivi sasa serikali imekuja na mkakati mpya wa “Utalii kwa Wote”. Mkakati huu tayari umezinduliwa rasmi, na lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kila mwananchi Mzanzibari popote pale alipo Unguja na Pemba ananufaika na sekta hii ya utalii.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari

Kama nilivyogusia hapo awali mafanikio ya mikakati na malengo yote hayo tuliyoyaeleza yatatokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani, utulivu na maelewano miongoni mwa wananchi wake.
Katika nchi yetu ni ukweli uliowazi kwamba wapo baadhi ya wananchi ama hawajaelewa, au wameamua kukataa hali hii ya maridhiano na maelewano miongoni mwetu. Watu hao wakiwemo miongoni mwa baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa na mwenendo ambao matokeo yake yanaweza kuleta mgawanyiko na kuvuruga hali hii ya mshikamano na amani tunayojivunia.

Serikali itaendelea kuchukua juhudi kubwa kuwaelimisha juu ya umuhimu wa maridhiano yetu na kuwafahamisha kwamba wananchi walio wengi hivi sasa hawako tayari kurudi nyuma tulikotoka kwenye hali ya mifarakano na chuki miongoni mwa jamii.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Katika mkutano kama huu na waandishi wa habari mwaka jana, nilijikita zaidi kuzungumzia changamoto za kiuchumi ambazo zimesababisha ugumu wa maisha kwa Wazanzibari walio wengi, zikiwemo mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu kama vile, mchele, sukari, unga wa ngano na nyenginezo na kueleza mipango tuliyokuwa tumejipangia. Leo nimepanga nizungumzie zaidi kwa kifupi changamoto za ndani zinazojitokeza katika utendaji wa kila siku serikalini.
Waheshimiwa
Katika utendaji wetu serikalini katika kipindi hiki cha miaka miwili, bado tunakabiliwa na changamoto nyingi. Kati ya hizo ni kudhibiti matumizi holela ya fedha za umma miongoni mwa watendaji wetu. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka 2010/2011 inaonesha bado kuna watendaji ambao wamedhamiria kujinufaisha binafsi kupitia fedha za serikali. Wanafanya hivyo, licha ya hatua na juhudi kubwa zinazochukuliwa kuwakataza na kuhimizana kujali misingi ya Utawala Bora.

Pamoja na marekebisho katika baadhi ya maeneo lakini bado kila zinapotoka ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, zinaonesha suala la matumizi yasiyofuata taratibu linaendelea kujitokeza.
Kuna udhaifu mkubwa wa kukosekana baadhi ya vielelezo muhimu katika ukusanyaji na matumizi ya mapato. Aidha, kumegundulika kujitokeza udanganyifu katika utayarishaji wa mafao ya baadhi ya wastaafu.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza utaratibu wa kukagua miradi ya maendeleo na kujiridhisha kuwa kazi iliyofanyika inalingana na thamani ya fedha zilizotumika. Imegundulika katika baadhi ya miradi, fedha zilizolipwa ni nyingi sana ikilinganishwa na kazi iliyofanyika pamoja na ubora wa kazi wenyewe kuwa haulingani kabisa na fedha zilizolipwa.

Napenda kutoa wito maalum kwa watendaji serikalini kuacha tabia ya udokozi wa fedha za wananchi, na wahakikishe wanafuata taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za umma. Aidha, serikali haitavumilia kuona baadhi ya watendaji wanaendelea kukiuka sheria zilizopo na kuchukua fedha za wananchi kujinufaisha wao binafsi.

Sote tunaelewa ni kwa kiasi gani serikali inavyojibana katika matumizi, ili kuhakikisha mapato hayo kidogo yanayopatikana yanatumika katika shughuli za maendeleo na za kijamii.
Hivi sasa serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inapata usafiri wa uhakika wa baharini, kwa azma ya kuwaondolea usumbufu wananchi na wageni wanaohitaji kusafiri kati ya Unguja na Pemba na Tanzania Bara. Jambo hilo linahitaji fedha nyingi katika kufanikiwa kwake; fedha ambazo zitatoka katika mfuko wa serikali. Sasa pale wanapojitokeza watendaji wa serikali kurudisha nyuma juhudi kama hizo kwa kufanya udanganyifu kwa kweli hilo si jambo zuri na si jambo la kuvumiliwa.

Serikali inachukua bidii kutafuta meli kubwa ya kisasa au za kisasa kwa kuamini kwamba hatua kama hiyo ndiyo itakayotuwezesha kuwa na usafiri wa uhakika na kuepuka maafa ya baharini, kama yaliyotokea mwezi Julai mwaka huu kwa kuzama meli ya MV. Skagit katika eneo la Chumbe na Septemba mwaka jana, yalipotokea maafa kama hayo ilipozama meli ya MV. Spice Islander katika eneo la Nungwi.
Changamoto nyengine ya muda mrefu inayotukabili ni baadhi ya watendaji wetu kulalamikiwa kuviza kwa makusudi haki za wananchi. Hali hiyo imejitokeza zaidi katika suala la utoaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZANID).

Pamoja na ahadi na kauli mbali mbali za watendaji na viongozi kuahidi kila mwananchi aliyefikia umri wa miaka 18 na mwenye sifa zote za kupata kitambulisho hicho kuwa atapatiwa, bado malakamiko ni mengi katika jamii kuwa kuna watu wananyimwa haki hiyo kwa makusudi kabisa.
Serikali inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka changamoto hii kwa kutambua kuwa vitambulisho hivyo ndio utambuzi wa Wazanzibari Wakaazi na vinahusika moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki mbali mbali za msingi.

Kuwa na kitambulisho hicho ni jambo la lazima la kisheria na kwamba kumkosesha mtu au mtu kushindwa kuwa nacho ni kosa ambalo mhusika anaweza kuhukumiwa kifungo na faini. Na kwa umuhimu huo huo, napenda kuwanasihi wananchi ambao vitambulisho vyao viko tayari, lakini bado wamekuwa na ajizi kwenda kuvichukua wakavichukue haraka.
Kwa upande mwengine kutokana na umuhimu wa kitambulisho hicho na kwa kuwa kimehusishwa moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki za msingi, kumejitokeza mahitaji makubwa ya watu kuvitafuta na hata wasiohusika, yaani baadhi ya wageni wanavitafuta kwa udi na uvumba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduizi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuendelea kuwasisitiza wahusika wanaolalamikiwa kuwanyima wananchi vitambulisho hivyo kuacha tabia hiyo. Kwa mara ya mwisho Rais Shein alitoa wito wiki iliyopita kule Pemba wakati wa semina maalum kwa watendaji wa Serikali za mitaa. Ni imani yangu kwamba watendaji na viongozi wa serikali za Mitaa, Wilaya na Afisi ya Msajili wa Vitambulisho, watatii agizo hilo la Rais.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari

Nimelazimika kulizungumza kwa kirefu kidogo suala hili la vitambulisho vya Ukaazi kutokana na umuhimu wake kwa wananchi. Lakini pia tumeona namna baadhi ya watu na vikundi wanavyoweza kutumia udhaifu wa utoaji vitambulisho hivyo kuuhusisha na masuala mengine muhimu ya Kitaifa.
Tumeona wakati wa zoezi la Sensa ya Kuhesabu watu na Makaazi hivi karibuni, baadhi ya watu walivyo tumia udhaifu wa utoaji vitambulisho hivyo kukaidi amri ya kuhesabiwa. Wamefanya hivyo, licha ya kuwa jambo la kuhesabiwa lina umuhimu wa kipekee katika maendeleo na ustawi wa wananchi. Hivyo basi ni vyema hatua zichukuliwe kila mwenye haki ya kitambulisho hicho asiwekewe kikwazo chochote, ili kuziba mianya kama hiyo inayotumiwa na baadhi ya watu kurejesha nyuma maendeleo na umoja wetu.
Waheshimiwa Waandishi

Jambo jengine ambalo napenda kuwahimiza tena wananchi, ni juu ya umuhimu wa kushiriki kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoendelea kufanya shughuli za kuratibu maoni ya wananchi nchi nzima tayari imefanya kazi hiyo katika mikoa ya Kusini Unguja na Kusini Pemba kwa hapa Zanzibar. Na katika mikoa hiyo wananchi waliweza kujitokeza vizuri kutoa maoni yao.
Nawasihi wananchi wote wa mikoa ya Kaskazini Unguja, Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi wajitokeze kwa wingi kwenda kutoa maoni yao, wakati tume hiyo itakapofika katika maeneo yao. Hatua hiyo ndiyo itakayotuwezesha kupata Katiba tunayoitaka yenye maslahi kwa Zanzibar.
Hii ni fursa adhimu ambayo tumekuwa tukiililia kwa siku nyingi juu ya haja ya Watanzania kupata fursa ya kutoa maoni yetu, juu ya masuala yote yanayohusiana na Muungano. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao kwa uwazi na pawepo na uvumilivu. Hata kama mtu hakubaliani na maoni, hoja zinazotolewa na mwengine, inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata fursa aseme yake kwa uwazi pia.
Na mwisho wa yote hayo, ni kama ambavyo tunatarajia, maoni ya wengi ndiyo yatakayo heshimiwe baada ya wale wachache kupewa haki yao ya kusikilizwa kwa kikamilifu. Na sisi viongozi tunawajibu wa kusimamia hilo.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari

Sasa naona tugusie masuala ambayo imekabidhiwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kama ambavyo mnafahamu ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na mambo mengine, imekabidhiwa majukumu mazito, majukumu ambayo kwa lugha ya siku hizi yanaitwa Masuala Mtambuka (Cross Cutting issues), yakiwemo; Masuala yanayohusu Watu Wenye Ulemavu, Mapambano dhidi ya Madawa ya Kulevya, Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Ugonjwa wa Ukimwi.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Katika suala la mapambano dhidi ya UKIMWI, Wazanzibari tunapaswa sote tufahamu kuwa ukimwi bado upo na unaendelea kuwaathiri watu wetu. UKIMWI ni tatizo linalotugusa sote, wanawake, wanaume, vijana na watoto na ni janga ambalo linasababisha matatizo makubwa katika ngazi za familia hadi serikali.
Serikali kwa ushirikiano na wadau mbali mbali inachukua hatua kubwa katika kuweka mazingira mazuri ya kupiga vita janga hili, lakini bado kuna maambukizi mapya ya UKIMWI yanatokea.

Pia wale walioathiriwa na maambukizi bado wanakabiliwa na vikwazo vingi, ikiwemo kunyanyapaliwa na baadhi ya wanajamii. Aidha wanakumbana na hali ya umasikini na uhaba wa dawa na huduma nyengine wanazozihitaji.
Kiwango cha maambukizi ya ukimwi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kimeendelea kusimama kwenye 0.6, ikiwa ni sawa na watu 7,200 wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI. Visiwani humu hali ya maambukizi ni mbaya zaidi kwa watu wa makundi maalum, ambayo inakadiriwa kupita kiwango kilichopo katika jamii nzima.

Kwa Zanzibar makundi maalum yanajumuisha; Watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, Wanawake wanaouza miili yao, Wanafunzi katika vyuo vya Mafunzo na Wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Hata hivyo, tafiti mbali mbali ndogo ndogo hivi sasa zinaendelea, ili kujua hali halisi ya maambukizi ya UKIMWI Zanzibar, pamoja na mwenendo mzima wa maradhi hayo na kuweza kuandaa mikakati thabiti kwa mujibu wa hali ilivyo katika kudhibiti maambukizi mapya, na kuwasaidia wale ambao tayari wameambukizwa.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeweza kufuatilia na kutathmini program mbali mbali za UKIMWI. Mwaka jana jumla ya vikundi 24 vyenye miradi 36 ya kujiongezea kipato vilifuatiliwa. Jumla ya shilingi milioni 15 kwa mfano walipatiwa jumuiya ya ZAPHA+ kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao mbali mbali zinazolenga utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari

Nadhani bado mnakumbuka Disemba Mosi mwaka jana tulizindua Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI wa Zanzibar. Mkakati huo umeandaliwa maalum kuongoza muitikio wa kitaifa wa mapambano dhidi ya ukimwi kwa mwaka 2011/2016. Lengo kuu ni kuzuia kuenea maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa Wazanzibari, kukabiliana na athari mbaya za kiafya, ustawi na za kiuchumi zinazompata mtu mmoja mmoja , familia zao, makundi maalum na Taifa kwa jumla.
Aidha, Sera ya Taifa ya UKIMWI ya 2005 imejenga msingi mzuri wa kufanikisha mapambano dhidi ya ukimwi. Sera hiyo imeweka mfumo wa utawala wa kisheria kwa ajili ya mipango na harakati zote zitakazofanywa, ikiwemo kuzuia maambukizi mapya, kutibu, kutunza na kuwasaidia walioambukizwa pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutayarisha na kutekeleza program za ukimwi kwa kuzingatia jinsia na haki za binaadamu wote.

Katika kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar tunaendelea kutoa wito kwa jamii, wakiwemo wazazi na viongozi wa kidini waendelee kutoa nasaha na kuwakataza vijana wetu na jamii kwa jumla, kuepuka matendo ambayo yatasababisha watu kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Vijana katika umri wao huiona dunia kama mahali pa uwezekano usiomalizika. Vijana waliopewa miongozo na malezi mazuri ndio wenye mwelekeo mzuri wa kusalimika na matatizo kama haya. Familia hazina budi kuwapa mawaidha vijana wao wa kike na kiume tena kwa uwazi mkubwa kabisa juu ya ukimwi, ili wajiepushe.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari

Kuhusu Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, katika jamii ya Wazanzibari kama zilivyo jamii nyengine, miongoni mwetu kuna Watu Wenye Ulemavu. Aidha, katika harakati za kimaisha za siku hadi siku kuna sababu tafauti zinazopelekea idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka. Kutokana na ukweli huo pamoja na wajibu wetu wa kibinaadamu, hatuna budi kuwa na mipango na mikakati imara ya kuwasaidia watu wenye ulemavu. Kujitolea kwetu kuwasaidia watu wenye ulemavu ndipo tutawawezesha wenzetu hawa kuishi kwa furaha na kuondokana na vikwazo vingi vinavyowakabili hivi sasa.

Watu wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine katika jamii. Wenzetu hawa wana kila haki ya kushirikishwa katika mipango yote ya kimaendeleo, pamoja na huduma za kijamii. Lakini kwa bahati mbaya sana hadi sasa watu wenye ulemavu wana kilio kikubwa cha kutopatiwa haki zao stahiki ipasavyo, pia wana malalamiko mengi ya kunyanyaswa na kudhalilishwa ikiwemo kijinsia.
Lakini pia katika jamii zetu tunaona ni namna gani hata mwamko juu ya watu wenye ulemavu ulivyo mdogo. Hadi leo kuna watu bado wanawaficha watoto na ndugu zao kwa sababu tu wana ulemavu. Kutokana na hali hiyo ndio maana tukaamua kuanzisha zoezi la makusudi kabisa kushajiisha jamii kuwafichua na kuwasajili watu wenye ulemavu.

Katika zoezi hilo linaloendelea ambalo lilitanguliwa na mafunzo kwa Masheha na wakusanyaji taarifa, tumeweza kusajili jumla ya watu 6,445 wenye ulemavu katika mikoa yote miwili kisiwani Pemba. Awali zoezi hilo lilifanyika kwa majaribio katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako jumla ya watu wenye ulemavu 3,002 walisajiliwa.
Aidha, katika kukuza na kuendeleza mwamko juu ya masuala ya watu wenye ulemavu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imefanya kazi kubwa kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanaingizwa katika mipango ya taasisi za za Serikali. Hadi sasa ofisi imeweza kusimamia uanzishwaji wa mpango huo na Maafisa Waratibu 16 tayari wapo katika wizara mbali mbali kwa ajili ya hatua hizo na tayari wamepatiwa mafunzo maalum.

Kwa upande mwengine, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imehakikisha inajenga uwezo kwa Idara ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, kwa kununua vifaa vya ofisini pamoja na vifaa vya utendaji kwa wafanyakazi wake. Vile vile jumuiya tisa za Watu wenye Ulemavu zimeweza kupatiwa ruzuku pamoja na visaidizi, yaani viti vyenye magurudumu mawili kwa watu 31 Unguja na Pemba, ili kuwasaidia katika harakati zao za kimaisha.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari

Wajibu wetu kwa watu wenye ulemavu ni mkubwa, lakini wakati ukweli ndio huo uwezo na nyenzo zetu hazitoshi kuweza kuwajengea uwezo kikamilifu kwa mujibu wa mahitaji yao. Lakini kwa kuthamini maisha na maendeleo yao, haki, fursa na usawa kwa watu wenye ulemavu, wajibu wetu wa kuwawezesha kukabilina na umasikini uliokithiri na upatikanaji mdogo wa huduma za afya tumeona kuna haja kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu.

Mfuko wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar umeanzishwa kama Sheria No. 9 ya mwaka 2006 inavyoagiza. Kama ambavyo waandishi wa habari ni mashihidi, Mfuko huo tayari umezinduliwa rasmi wiki iliyopita na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed na kwakweli naona fahari kusema tumeanza vizuri.
Tunawashukuru mwananchi mmoja mmoja, mashirika, jumuiya, taasisi za kiserikali na watu binafsi, kwa namna walivyojitokeza na kuonesha moyo wao wa dhati kuwasaidia watu wenye ulemavu Zanzibar. Moyo wao huo umewezesha mfuko huo kuanza na kiasi cha T.SHS milioni 285. Tunaendeela kukuhimizeni wananchi na taasisi mbali mbali kuendelea kuchangia mfuko huu kwani uchangiaji wa mfuko unaendelea.
Matumaini yetu Mfuko huu utaweza kutoa mchango mkubwa kusaidia utatuzi wa changamoto nyingi ambazo baadhi tumesha zianisha.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa upande wa Madawa ya Kulevya, Suala hili pia ni changamoto nyengine kubwa inayotukabali katika nchi yetu. Na ukweli ni kwamba tatizo hili sio tu kwa Zanzibar, bali kwa Dunia nzima. Kutokana na ukubwa wa tatizo la madawa ya kulevya mataifa yanaungana kupambana na wazalishaji, wafanyabiashara na walanguzi wa madawa haya ambao nao wamejidhatiti vilivyo. Katika baadhi ya nchi tunashuhudia hata nguvu za kijeshi zikitumika kukabiliana na tatizo hili.
Athari za madawa ya kulevya zipo wazi na Zanzibar tunashuhudia hilo. Maisha ya watu wetu hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa yamekuwa hatarini. Lakini kwa upande mwengine madawa ya kulevya yamekuwa chanzo kikuu cha maambukizi ya maradhi ya ukimwi, ambayo nayo yanachukua nafasi kubwa kuteketeza maisha ya binaadamu na kudhorotesha uchumi wa nchi.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuratibu na kudhibiti utumiaji, biashara na usafirishaji wa madawa hayo. Kazi hizo zimekuwa zikifanywa kwa karibu na wananchi pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, azma yetu ikiwa ni kuinusuru Zanzibar kuwa kituo cha madawa ya kulevya na wananchi wake kuathirika na madawa hayo.
Mikakati yetu juu ya jambo hili imelenga zaidi kuwa na sheria zinazokwenda na wakati ambazo zinakidhi haja ya kudhibiti madawa ya kulevya kwa wakati uliopo.
Katika utekelezaji wa hatua hiyo tayari sheria Nam. 9 ya mwaka 2009 ilipitiwa na wadau mbali mbali na baadaye kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi na kurekebishwa. Aidha, uandaaji wa Sera ya Madawa ya Kulevya Zanzibar inaendelea na hivi sasa kazi za kukusanya maoni ya wadau inafanyika.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Juhudi kubwa katika kudhibiti madawa ya kulevya Zanzibar tumezielekeza katika kutoa taaluma kwa jamii juu ya madhara yake, lakini pia kuwasaidia vijana walioingia kwenye matumizi ya madawa haya, kwa kuwanasihi waache, pamoja na kuwashauri na kuwasaidia njia zitakazowawezesha kupata kazi za kujiongezea vipato na kuondokana na tabia ya kukaa bila ya kazi, tabia ambayo huwapa msongo wa mawazo na kuwafanya waendelee kutumia madawa hayo.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika mwaka wa fedha uliomalizika, iliweza kutoa ushauri nasaha kwa familia 984 za watumiaji wa madawa ya kulevya, wakiwemo wanawake 510 na wanaume 474, ambapo kati yao, 97 walikuwa watumiaji wa madawa ya kulevya.
Aidha, ahadi ya kuzisaidia angalau fedha kidogo taasisi zinazotoa huduma za makaazi ya vijana wanaoacha kutumia madawa ya kulevya (Sober Houses) ilitekelezwa na shilingi 9,900,000 zilitolewa, pamoja na televisheni na redio Unguja na Pemba.
Rasimu ya muongozo wa nyumba za marekebisho za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya madawa hayo imekamilika. Aidha, suala la taaluma kwa jamii juu ya kupiga vita madawa ya kulevya limeendelea kupewa umuhimu wa kipekee kwa kuandaa vipindi mbali mbali vilivyoweza kurushwa hewani kupitia televisheni na redio. Vile vile Shehia mbali mbali zilifanyiwa ziara za uhamasishaji na taaluma juu ya athari za madawa hayo Unguja na Pemba.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kuhusu suala la Kuyahifadhi na kuyalinda mazingira yetu, pia hili nalo ni muhimu katika kudumisha Uhai na Ustawi wa nchi yoyote ile. Hata hivyo changamoto inayojitokeza katika nchi nyingi, ikiwemo Zanzibar ni uharibifu na uchafuzi mkubwa na wa makusudi wa mazingira yetu. Kasi tunayoishuhudia ya ukataji ovyo wa misitu na uchimbaji wa mchanga na mawe, kwa ajili ya kutengeneza matofali ni ya kutisha na iwapo haitadhibitiwa nchi yetu ya Zanzibar kipindi kifupi kijacho itakabiliwa na janga kubwa la kimazingira.
Aidha, upoteaji wa bioanuwai za nchi kavu na baharini kwa jumla, utupaji ovyo wa taka na maji machafu, uvunaji usioridhisha wa maliasili zisizojirejesha, hali inayosababisha kuachwa kwa mashimo mengi, pamoja na ile tabia ya kuingizwa kwa wingi nchini vifaa chakavu vya elektroniki, umeme na mifuko ya plastiki inaongeza ukubwa wa hatari hiyo ya kimazingira.
Kwa upande mwengine suala la mabadiliko ya tabianchi limekuwa ni tishio kubwa kwa dunia, na nchi zinazoathirika zaidi ni zile za visiwa vidogo kama vyetu vya Zanzibar. Hali inayojitokeza katika baadhi ya maeneo ya visiwa vyetu ambako maji ya bahari yamevamia mashamba ya kilimo cha mpunga inatosha kuwa onyo kali kwetu na kufanya kila linalowezekana kuyalinda mazingira.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira, ikiwemo suala la athari za mabadiliko ya tabianchi bado inaamini utoaji wa elimu na kuzidi kukumbushana ndio njia muafaka na yenye umuhimu wa kipekee.
Hata hivyo hatua za kisheria zimeendelea na zitaendelea kuchukuliwa kwa wananchi au miradi ya kiuchumi ambayo inaonekana kwa makusudi kupinga au kudharau sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Miongozi mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kutoa taaluma kwa njia ya semina, vipindi vya televisheni na redio, pamoja na kuandaa ziara za kimasomo katika maeneo mbali mbali, ili wananchi, viongozi wa maeneo na wanachama wa jumuiya zisizokuwa za kiserikali, waweze kujifunza na baadaye kusaidia jamii kukumbusha na kuhamasisha suala zima la kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira ya nchi yetu.
Hatua hizo zinajumuisha mafunzo juu ya mabadiliko ya Tabianchi na mwelekeo wa Zanzibar katika kusimamia jambo hilo, yalitolewa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Aidha wafanyakazi 12 kutoka Idara ya Mazingira, Baraza la Manispaa Zanzibar, Halmashauri za Wilaya ya Magharibi na Mabaraza ya Miji ya Chake Chake, Mkoani na Wete na baadhi ya wawakilishi wa Jumuiya zisizokuwa za kiserikali waliwezeshwa kufanya ziara za kujifunza huko Moshi na Arusha, ili waweze kupata uzoefu juu ya usimamizi wa taka.
Ziara za kujifunza za aina hii, pia ziliwahusisha viongozi 10 wa Kamati za Machimbo ya Uwandani waliokwenda Mjini Mombasa Kenya kujifunza njia bora za shughuli za uchimbaji na urejeshwaji wa maeneo yaliyochimbwa na kuepusha athari za kimazingira.
Hatua hizo zilichukuliwa kwa makusudi, ili kudhibiti kasi ya uchafuzi wa maeneo na kuyaweka katika hali ya usafi, pamoja na kudhibiti athari za uchimbaji mawe kwa ajili ya kazi za uchongaji matofali, maeneo ambayo yanahatarisha sana hali ya mazingira hapa Zanzibar.
Eneo jengine ambalo linaonekana ni sugu katika uharibifu wa mazingira yetu ni kwenye fukwe na miradi ya hoteli za kitalii. Katika siku za hivi karibuni miradi 110 ya kitalii ilifanyiwa ufuatiliaji kuona inavyozingatia masuala ya kimazingira. Taarifa ya ufuatiliaji huo si ya kufurahisha kwa sababu kati ya miradi mingi ambayo ilionekana kukiuka kanuni ya kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji ya mwaka 2006.
Miradi hiyo ilitakiwa kubomoa sehemu zilizojengwa kinyume na kanuni, lakini ni mradi mmoja tu wa hoteli ya Zanzibar Ocean View ambao umetii amri hiyo.

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ilichukua hatua ya kuwasilisha majina ya miradi hiyo iliyoshindwa kufuata agizo hilo, Idara ya Mipango Miji na Vijiji kwa ajili ya hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni.
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba ipo haja kubwa ya kuimarishwa Sheria na kanuni zetu za Mazingira, ili ziweze kukidhi haja kwa mujibu wa wakati.
Kuhusu usimamizi wa marufuku ya mifuko ya plastiki, baada ya Kanuni kufanyiwa marekebisho, mafanikio makubwa yameweza kupatikana ambapo hadi unakamilika mwaka wa fedha uliopita, watu 192 walikamatwa na kushitakiwa mahakamani na jumla ya shilingi 7,650,000 zilizotokana na faini ziliingia katika mfuko wa serikali.
Ni dhahiri changamoto ya kimazingira ni kubwa, hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake wa kulinda na kuyahifadhi Mazingira yetu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Baada ya kusema hayo natanguliza shukurani zangu nyingi, kwa viongozi na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwemo Waziri wangu wa Nchi mchapakazi na muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji.
Vile vile shukurani hizo ziende kwa Katibu Mkuu makini mwenye uzoefu na ujuzi wa taratibu za serikali ambaye ndiye anayenishauri mimi na Waziri wa Nchi kuhusu masuala ya kitaalamu, mbali kuwa Mtendaji Mkuu wa shughuli zote zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar Shajak akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii. Wote hao nawashukuru kwa msaada mkubwa wanaoendelea kunipa kwa muda wote huu.
Ahsanteni sana.

No comments:

Post a Comment