WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 8, 2012

Dk Ulimboka aibuka ajipanga kuanika waliomteka





Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka ameibuka na kusema yuko imara na anajiandaa kuanika waliomteka, kumtesa na kisha kumtupa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk Ulimboka alisema kamwe hajanunuliwa na kwamba ukimya wake wa muda mrefu umetokana na kufuatilia kwa karibu masharti ya matibabu yake na si vinginevyo.
“Sijanunuliwa, sijawaogopa watesi wangu, wala sijanyamazishwa kwa lolote lile. Hata hao wanaoeneza taarifa kuwa nimenunuliwa, wanajua kuwa hawana ubavu wa kuninunua,” alisema.
Dk Ulimboka amekiri kuwa amewahi kusikia taarifa za yeye kununuliwa na kusema amekuwa akijisikia vibaya kuona kundi la watu fulani likihaha kutaka kupotosha ukweli na kuchafua jina lake.
“Huo ni uzushi mtupu. Hata walionitesa wanajua kuwa hawawezi kuninyamazisha au kuninunua. Wanajua sina bei katika kutetea masilahi ya umma. Ndiyo maana wakaamua kutumia njia ile ya kinyama kutaka kunitoa roho yangu. Siwaogopi wanaodhuru mwili, bali yule awezaye kutoa roho. Nakuhakikishia, muda si mrefu nitaanika kila kitu juu ya kutekwa kwangu, kuteswa na kutupwa kwenye Msitu wa Pande,” alisema.

Dk Ulimboka alitekwa Juni 26, mwaka huu na kuteswa ikiwamo kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na kisha kutupwa katika msitu huo kabla ya kuokolewa asubuhi yake na wasamaria wema karibu na msitu huo.
Daktari huyo ambaye bado hajahojiwa na polisi juu ya aliowataja kuhusika na utekaji na utesaji huo, amesisitiza kuwa alipokamatwa alikuwa na akili timamu na kwamba anawafahamu wote waliopanga mkakati wa kumteka.
“Watanzania na wapendahaki duniani kote, wana haki ya kujua kwa kina yale yaliyonisibu pamoja na watu waliohusika katika kutekwa kwangu. Hivyo ninao wajibu mkubwa wa kueleza ukweli huo na bila kuuma maneno.”
Haya ni mahoajino ya kwanza ya ana kwa ana tangu Dk Ulimboka aliporejea nchini kutoka katika matibabu Afrika Kusini miezi miwili iliyopita.
“Huo ndiyo msimamo wangu na katika hili siwezi kutafuna maneno, mimi kama kiongozi ninao wajibu mkubwa wa kulieleza hili kwa Watanzania wenzangu.”
Tofauti na aliporejea, Agosti 12 mwaka huu, Dk Ulimboka ameonekana akiwa mwenye siha nzuri huku akisema mapambano ya kudai haki za madaktari bado hayajafikia tamati.
Alisema mapambano hayo ni muhimu kuendelezwa kwa kuwa ndiyo njia pekee itakayoifanya Serikali kuboresha huduma za afya nchini. Alisema ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa mamia ya wananchi wanakufa kutokana na kukosa huduma bora za afya.
Aliwataka madaktari kote nchini, kuzidisha mshikamano na kuendelea kupigania haki zao akisema wanachokidai ni haki yao.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment