WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 19, 2014

Warioba aanika machungu

  Asema serikali tatu haziepukiki
  Ni kilio cha miaka zaidi ya 30

 
Jaji Mstaafu Joseph Warioba, akiwasilisha bungeni Rasimu ya Katiba.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema tathmini ya Tume yake ilithibitisha kuwa Muundo wa Muungano wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa.
Alisema Muungano wa serikali mbili ulioachwa na waasisi siyo uliopo sasa kwani umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba.

“Waasisi walituachia Muungano wa serikali mbili, na siyo nchi mbili zenye serikali mbili. Muundo wa serikali mbili unaweza kubaki tu kama orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali itaongezwa,” alisema.

Katika hotuba yake aliyoanza kuisoma saa 3:30 asubuhi hadi saa 7: 10 mchana, wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge Maalumu la Katiba, Jaji Warioba alikuwa ikishangiliwa na wajumbe wengi kutoka Zanzibar na vyama vya upinzani. (soma hotuba yake uk. 10-14)

Alisema kwa kipindi cha miaka 30, kumekuwapo hoja za muundo wa serikali tatu.

 “Muungano, pamoja na matatizo yote tuliyonayo, umedumu kwa miaka hamsini. Kuna hofu kwamba muundo wa serikali tatu utavunja Muungano. Baada ya kutafakari kwa kina Tume inaamini hakuna msingi wa hofu hii,” alisema.

Alisema asilimia 61 ya wananchi walipendekeza serikali tatu na asilimia 60 walipendekeza Muungano wa mkataba wakati wa kukusanya maoni ya katiba mpya.

MIITO YA SERIKALI TATU

Alieleza kuwa baadhi ya migogoro iliyotokana na Muungano kuwa ni pamoja na wa mwaka 1984, kilitokea kile kilichoitwa “kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar,” Msingi wake ilikuwa ni mpango wa baadhi ya viongozi wa Zanzibar kutaka Serikali Tatu.

Ingawa jaribio hilo halikufanikiwa, lakini Zanzibar ilitunga Katiba Mpya mwaka huo na kujipa baadhi ya madaraka ya Katiba ya Muungano.

Alisema Katiba ya Zanzibar iliweka masharti kwamba sheria za Muungano zipelekwe kwenye Baraza la Wawakakilishi kabla ya kutumika Zanzibar.

Aliongeza kuwa mwaka 1991, Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza muundo wa serikali tatu.

Ingawa pendekezo hilo halikukubalika, mwaka 1992, Zanzibar ilijiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (IOC) na Bunge lilipitisha Azimio la kuzitaka serikali zote mbili kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na matatizo mengine ya Muungano na kutoa taarifa bungeni katika kipindi cha mwaka mmoja.

Alisema mwaka 1993, wakati wa mkutano wa Bajeti, Wabunge kutoka Tanzania Bara (G 55) walipeleka Bungeni hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika. Hoja hiyo ilipitishwa na kuwa Novemba mwaka 1993, kikao Maalum cha CCM na Serikali zote mbili kilifanyika Dodoma ili kutafuta maelewano kuhusu Azimio la Bunge. Jaji Warioba alisema kuwa mwafaka ulifikiwa kwamba Azimio hilo lisitekelezwe, yaani Serikali ya Tanganyika isiundwe.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, mwaka1994, Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha azimio kuhusu haja ya kuendelea na muundo wa Serikali mbili kwa lengo la kufikia Muundao wa serikali moja.

Alisema baada ya Tume ya Jaji Nyalali, serikali iliunda Kamati ya Shellukindo ikijumuisha wajumbe kutoka Serikali zote mbili na Serikali ya Zanzibar iliunda Kamati ya Amina Salum Ali.

Jaji Warioba aliongeza kuwa kwa kuwa mjadala juu ya muundo wa Muungano ulikuwa unaendelea wakati wote, Serikali ikaona ni busara kuunda tume ya Jaji Kisanga ambayo, pamoja na mambo mengine, ilitakiwa kupendekeza aina ya muundo wa Muungano na ilipendekeza serikali tatu.

MALALAMIKO DHIDI YA MUUNGANO
Alisema katika kipindi chote hicho, kulikuwa na malalamiko kutoka kila upande, baadhi ya malalamiko kwa Zanzibar ilikuwa ni suala la Serikali ya Muungano ambalo linaisaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar.

“Taswira hiyo imeifanya Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania na Watanganyika ndiyo wamekuwa Watanzania; na Wazanzibari wamebaki kuwa Wazanzibari,” alisema.

Kwa upande wa Tanzania Bara, baadhi ya malalamiko ni Zanzibar imetunga katiba ambayo imechukua madaraka ya Rais yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanayoeleza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano ana madaraka ya kugawa nchi katika maeneo ya kiutawala.
Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yameitambua Zanzibar kuwa ni nchi na yanampatia mamlaka Rais wa Zanzibar kuigawa nchi katika maeneo ya kiutawala.
“Tume iliamua kufanya uchambuzi wa kina kuhusu baadhi ya malalamiko, hasa malalamiko ya Zanzibar. Malalamiko ya Tanzania Bara yanatokana, kwa kiwango kikubwa, na hatua zilizochukuliwa kwa upande wa Zanzibar. Kama malalamiko ya Zanzibar yakipatiwa ufumbuzi, malalamiko ya Tanzania Bara nayo yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi,” alisema.
 
KUONGEZEKA KWA MAMBO YA MUUNGANO
Alisema kuwa kati ya mambo 22 ya Muungano, Tume imebaini kuwa siyo yote yanatekelezwa kikamilifu kimuungano. Mengi yamebadilishwa bila kubadili katiba, ama kwa makubaliano kati ya pande zote mbili za Muungano au kwa hatua zilizochukuliwa na upande mmoja.

HAYATEKELEZEKI

Mambo ambayo hayatekelezwi kimuungano ni bandari, leseni za viwanda, utafiti, takwimu, biashara ya nje na maliasili ya mafutana gesi.

“Lakini kuna mambo mengi ambayo hayatekelezwi kikamilifu. Kwa mfano, mambo yanayohusu uhusiano wa kimataifa, ulinzi, uchukuzi, mahakama ya rufani, usafiri wa anga, kodi, posta, simu na uraia,” alisema.
 
MGONGANO WA KATIBA
Alisema kuna mgongano kati ya Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar. Ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka masharti kwamba sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano hazitatumika Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.
 
MICHANGO, GHARAMA ZA MAPATO NA MGAWO WA MAPATO

Alifafanua kuwa matumizi ya fedha na rasilimali za Muungano, mchango wa pande zote mbili kwa shughuli za Muungano na mgawo wa mapato ya Muungano yamekuwa ni masuala yenye utata kwa muda mrefu.

Alisema katika kupata ufumbuzi wa tatizo hili, mwaka 1977 Halmashauri Kuu ya CCM ilitoa uamuzi kwamba mapato ya kodi za Muungano yabaki upande wa Muungano yanapokusanywa.

Kwa msingi huo, mapato ya kodi za Muungano yanayokusanywa Zanzibar yabaki kwenye Hazina ya Serikali ya Mapinduzi ya Jamhuri ya Muungano na yale mapato ya kodi za Muungano yanayokusaanywa Tanzania Bara yabaki kwenye Hazina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano na yatumike Tanzania Bara.

Halmashauri Kuu pia ilibadili utaratibu wa kuchangia. Hata hivyo, alisema uamuzi huo haukumaliza matatizo.

Jaji Warioba alisema katika muungano wa nchi mbili, serikali tatu haziepukiki.

MADARAKA YA RAIS

Katika hatua nyingine, Warioba alisema madaraka ya Rais yamepunguzwa kwa kiwango kikubwa kwenye Rasimu ya Katiba.

Jaji Warioba alisema Tume yake imeweka mapendekezo makubwa manne kwenye Rasimu ya Katiba ambayo kwa kiasi kikubwa yanapunguza madaraka ya rais tofauti na ilivyo kwenye katiba ya sasa.

Alisema pendekezo la kwanza ni kumwondoa Rais kutoka kwenye bunge, kwani kwa katiba ya sasa rais ni sehemu ya Bunge na mawaziri wake ni wabunge.

Alisema nia ya pendekezo hilo ni kutenganisha mamlaka na madaraka ya mihimili ya dola kwani kazi kubwa ya bunge ni kuisimamia serikali na kuwa bunge haliwezi kuisimamia serikali kwa uhuru kama nayo ni sehemu ya bunge.

RAIS KURA ZAIDI YA NUSU
Alisema Tume pia imependekeza kuwa mtu atachaguliwa kuwa rais kama atapata kura za wapiga kura zaidi ya nusu, badala ya utaratibu wa sasa wa kupata wingi wa kura.

Jaji Warioba alisema msingi wa pendekezo hilo ni kwamba rais si kwamba ni kiongozi wa serikali tu bali pia ni mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu na kwa sababu hiyo ndiye taswira ya nchi na watu wake na ndiye alama ya umoja na uhuru wa nchi na mamlaka ya nchi, hivyo ni muhimu kuonekana anakubalika na wengi.

Alisema pendekezo la tatu la Tume yake ni kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani, kwa sasa matokeo ya uchaguzi wa rais yakishatangazwa na Tume ya Uchaguzi hakuna ruhusa ya kuhoji matokeo hayo.

Pia Tume imependekeza rais kutabaki na madaraka ya msingi kama mkuu wa nchi, amiri jeshi mkuu na mkuu wa serikali.

Alisema rais amepunguziwa madaraka ya kuteua watumishi wa umma wa ngazi za kati na ngazi za chini, sasa watateuliwa kwenye madaraka ya Tume za Utumishi.

Alisema rais atabaki na madaraka ya kuteua viongozi wa kitaifa kama vile mawaziri, majaji, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, makatibu wakuu wa wizara na wenyeviti na wajumbe wa tume za kitaifa.

Hata hivyo, Jaji Warioba alisema kuwa pamoja na kubakiwa na madaraka hayo, rais amewekewa utaratibu wa uteuzi, baadhi ya viongozi watateuliwa moja kwa moja naye, baadhi ya kuteuliwa  na kuthibitishwa na bunge na wengine watateuliwa na kutokana na ushauri wa Tume ya Utumishi.

Baadaye ya watakaothibitishwa na bunge ni mawaziri, watakaopendekezwa kwanza na Tume ya Utumishi ni kama vile majaji na makatibu wakuu.

MAONI YA WAJUMBE
Baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo, baadhi ya wajumbe walitoa maoni huku baadhi yao wakionyesha kufurahishwa pendekezo la muundo wa serikali tatu na wengine wakiupinga.

MACHALI

Moses Machali alisema serikali tatu haziepukiki kwa namna yoyote kutokana na mapungufu aliyobainisha Jaji Warioba na kwamba wanaopinga wana ajenda yao ya siri.

Machali alisema kuwa maoni yaliyotolewa na Watanzania yanapaswa kuheshimiwa kwa kuwa Muungano umekuwa na mapungufu pamoja na kero mbalimbali, hivyo suluhisho ni serikali tatu.

OLUOCHI
Ezekia Oluoch alisema kuwa kulingana na Rasimu iliyowasilishwa na Jaji Warioba, hakuna namna nyingine ya kukwepa uanzishwaji wa serikali tatu.

Alisema Serikali mbili ambazo zinapigiwa debe na Chama Cha Mapinduzi  (CCM) hazitawezekana kutokana na miaka 50 ya Muungano kushindwa kushughulikia kero za Muungano hususani malalamiko kutoka Zanzibar.

MNYAA
Mohamed Mnyaa alisema amepokea Rasimu ya Jaji Warioba kwa furaha na mapendekezo ya uanzishwaji wa serikali tatu ambazo ni suluhisho la matatizo na kero za Muungano.

MBATIA
James Mbatia alisema kuwa iwapo wajumbe watazingatia maoni ya Watanzania yaliyotolewa katika Rasimu ya Katiba kuhusu uanzishwaji wa serikali tatu, yatajenga umoja wa kitaifa na kuondoa malalamiko mbalimbali ya kila upande.

CHAMBI
Hata hivyo, Suleiman Chambi alisema Jaji Wariomba hakuwatendea haki Watanzania kutokana na muda wake mrefu wa asilimia 90 kuzungumzia kutetea Serikali tatu na kuacha mambo mengine.

WASIRA
Stephen Wasira alisema kuwa suluhisho siyo uanzishwaji wa mfumo wa serikali tatu, bali kuondoa kero zilizojitokeza katika mfumo huo ili zipatiwe ufumbuzi.

VUAI

Vuai Ali Vuai alisema kuwa wajumbe wasilichukulie jambo hilo kwa wepesi kwa kuwa ni kubwa sana na siyo la kujadili kwa jaziba kwani wanapaswa kuangalia changamoto zilizopo katika mfumo wa sasa wa serikali mbili na ule wa serikali tatu.

Wakati huo huo, tofauti zilizojitokeza  juzi kati ya  wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta, kulazimisha kusitisha kikao cha Bunge, zilimalizika baada ya pande hizo mbili kufikia mwafaka na jana Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba.

Ukawa walitaka Rais Jakaya Kikwete azindue Bunge hilo na baadaye Jaji Warioba awasilishe Rasimu.

Imeandikwa na Beatrice Bandawe; Emmanuel Lengwa na Ashton Balaigwa, Dodoma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment