WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 12, 2014

Uwazi, faragha: Dhana mbili zinazotesa wajumbe Bunge la Katiba

  • Kifungu cha (57) kimependekeza vikao vya Kamati za Bunge hilo vifanyike kwa faragha wakati wa majadiliano ya kupitisha hoja na masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara.

Dar es Salaam. Bunge Maalumu la Katiba limekuwa likiendelea mjini Dodoma ambako hakuna shaka moto umewaka.
Vikao vya Bunge hilo katika baadhi ya nyakati vimewaka moto, hatua inayotafsiriwa kuwa ni afya au kukomaa kwa demokrasia nchini.
Ushindani wa hoja ambao umejitokeza katika mjadala wa kanuni zitakazotumika kuongoza Bunge hilo pia ni ushahidi kwamba ipo kazi.
Katika vikao hivyo, hoja mbalimbali zimeibuliwa na kuwekwa sawa au kupatiwa ufumbuzi kwenye vifungu vyenye utata katika rasimu hiyo ya kanuni.
Hata hivyo, vile vyenye utata vimepelekwa kwenye kamati ya watu makini, wenye busara ambayo imeundwa na mwenyekti wa muda, Pandu Ameir Kificho.
Baadhi ya vifungu vilivyoteka hisia katika mjadala huo ni pamoja na kifungu cha (57) kinachopendekeza vikao vya Kamati za Bunge hilo vifanyike kwa faragha wakati wa majadiliano ya kupitisha hoja na masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara.
Mvutano mwingine uliojitokeza kwa wajumbe hao, ulitokana na kifungu kingine kinachopendekeza kuwepo kwa kura ya uwazi wakati wa kupiga kura ya kuamua hoja mbalimbali za rasimu hiyo ya Katiba Mpya. 
Hata hivyo, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya siasa na utawala nchini wanasema vifungu  hivyo vimeonekana kuwa mfano wa sura mbili zinazojifitini kutokana na ukinzani uliopo kwa  waumini hao hao wa hoja ya uwazi.
Wanapendekeza kuwepo kwa vikao vya faragha wakati wa majadiliano ya kamati.
Katika mahojiano maalumu na wanasheria, wanahabari na wasomi mbalimbali nchini ili kupata ufafanuzi wa hoja hizo na tafsiri zinazoendelea kujitokeza.Wengi wanatoa hoja zinazokinzana.
Vikao vya faragha ni usaliti?
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Ruzuku kwa Vyombo vya habari Tanzania(TMF), Ernest Sungura anasema Bunge hilo limeanza kujenga kutokana na hatua ya kupitishwa kwa kifungu hicho cha faragha.
Aidha, anaongeza akisema pia kuwa pamoja na msingi wa uhuru wa habari kutambuliwa na Katiba iliyopo, ni dalili mbaya inayojitokeza katika kuandaa Katiba Mpya.
 “Wanachojadili kilitakiwa kuripotiwa kwa kila hatua kwa kuweka utaratibu mzuri ambao ungetoa nafasi kwa waandishi kwani wao ndiyo wana uwezo wa kuchuja habari zinazostahili kwa jamii. Kinachoripotiwa ni kwa manufaa ya Watanzania. Kwa hivyo ningeomba Bunge litafakari kwa busara jinsi ya kuruhusu waandishi kushiriki vikao hivyo,” anasema Sungura.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT), Kajubi Mukajanga ambaye ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba anasema walipendekeza waandishi wa habari washiriki vikao hivyo, lakini maombi yao yamekwama.
“Sikuona sababu za Bunge kufikia hatua hiyo. Bunge la Jamhuri ya Muungano wao wamekuwa wakiripoti bila masharti kwa nini Bunge hili?  Tuliopinga hatua hiyo wengi hatukupewa nafasi hata ya kuzungumza kwenye vikao na badala yake wanasiasa wakateka mjadala,” anasema Kajubi.
Anaongeza kuwa  hoja ya waandishi kuwa na tabia za upotoshaji katika kuripoti, haikuwa kigezo cha kuwafungia wasishiriki vikao hivyo.
“Ni kweli kuna matatizo katika vyombo vyetu vya habari katika kuripoti na binafsi sioni sababu ya kuingizwa kwenye kanuni kwani hatua hiyo imekaa kiutendaji,” anasema na kuongeza:
“Hata hivyo, nimezungumza na Ofisi ya Bunge  inayohusika na habari ili kuona ni jinsi gani wanaweza kuandaa semina kwa waandishi wote wa habari, kuwapatia maarifa, utaratibu ili waweze kushiriki katika vikao hivyo.
Msomi mmoja kutoka moja ya vyuo vikuu nchini anasema baadhi ya wajumbe walioshiriki kupitisha hoja ya vikao vya faragha ni mafanikio ya kukwepa aibu ambazo zingibuliwa na waandishi.
“Its not fair (si halali) kwa kweli na inasikitisha, hoja ya waandishi kupotosha haina mashiko. Kuna ushahidi gani wa habari za kupotoshwa na zisizopotoshwa?
Je,  kama hizo zinazoonekana kupotosha kwao ndiyo zikawa na ukweli kwa Watanzania? Waache habari za kuchezea akili za watu kwa propaganda chafu,” anasema msomi huyo.
Uwazi ni upotoshaji
Kupenyezwa kwa kifungu cha kura ya wazi ni moja kati ya siri kubwa inayopigiwa chapuo na wajumbe mbalimbali hususan kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkurugenzi  Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anasema pamoja na kukubaliana na mfumo wa kura ya wazi, anapinga uamuzi wa kura hiyo kutumika katika muundo wa Bunge hilo huku akibainisha kuwa ni upotoshaji.
Anatofautisha msingi wa kura hizo akisema: “Kuhusu kura ya wazi yenyewe hutumika katika majadala isiyokuwa na athari au mivutano ya kimasilahi. Kwa mfano katika kupitisha bajeti ndiyo kura inaweza kupigwa ya wazi ili kuona ni watu gani wanakubaliana kwa wakati huo, hatua hiyo haina  sababu. Anaongeza: “Lakini kura ya siri hutumika kwenye mazingira yenye utata na ukinzani wa kimitazamo  ili kuepuka ushawishi unaoweza kutolewa na kundi fulani lenye nguvu katika mazingira ya kifedha au kichama.”
Bisimba anasema mapendekezo ya kanuni hiyo yanatakiwa kupitisha kifungu cha kura ya siri ili kuepusha ushawishi kutoka ndani ya vyama na makundi mbalimbali yenye masilahi binafsi.
Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea kutoka Kampuni ya Sengalawe(Sengalawe Advocates), Sengalawe Charles anasema duniani kote demokrasia hukosa nguvu katika harakati za kufanya mabadiliko ya mfumo wa serikali iliyopo madarakani.
“Kuna Mtanzania gani ambaye mpaka sasa hajafahamu mbinu zinazoandaliwa na CCM katika mchakato huo? Ni vigumu kusimamia misingi ya demokrasia kwa sababu ni tofauti na mfumo wanaoutumia ambao unalalamikiwa muda mrefu, kwa hivyo tusitegemee mabadiliko yoyote,” anasema Sengalawe.
Msingi wa kura ya siri
Kutokana na mazingira hayo, Profesa Chris Maina Peter kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anafafanua msingi wa kura ya siri akisema kuna mataifa duniani yaliyoibua  mjadala wa kura ipi iweze kutumika katika wakati wa chaguzi.
“Nchi hizo ni Ugiriki na Roma katika miaka ya BC (Kabla ya Kuzaliwa Kristo), lakini baada ya mvutano mkali kura ya siri ikapitishwa  na mataifa mengine yakaanza kuitumia ikiwamo Ufaransa (1795), Uholanzi (1849), Australia(1856) na Uingereza (1872) ambayo tunaifuata,” anasema na kuongeza:
“Kwa upande wa Marekani ubishi uliendelea mpaka ilipofika mwaka 1891 jimbo la mwisho kukubaliana na utumiaji wa kura ya siri lilikuwa ni Kentucky.
Kule Uingereza, mfumo wa kura ya siri bado unapingwa kwa sababu unatumia namba za kuwatambua wapigakura, kitu ambacho bado haiwezi kuwa na azimio la kura ya siri.
Aidha, msomi huyo anasema endapo wajumbe hao watapisha kipengele hicho kutambua kura ya wazi, watakuwa wamevunja Katiba na Mikataba ya Umoja wa Kimataifa(International Covenant on Civil and Political Rights) ya mwaka 1966 inayofafanuliwa katika ibara ya 25(b) kifungu kinachosema:

“Kila raia atakuwa na uhuru na haki ya kupiga au kupigiwa kura katika mazingira ya usiri bila kubugudhiwa, bila kuathiri uhuru wake wa kujieleza kupitia utaratibu wa kumchagua mgombea ili kuepuka ushawishi na matakwa ya kisiasa.”

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment