WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 6, 2014

TUTARAJIE NINI KUTOKA BUNGE HILI MAALUMU LA KATIBA MPYA- TANZANIA. 
Prof. Shivji katika kongamano lilofanyika tarehe 15/1/2011 Dar es Salaam alisema kuwa: “ Katika nchi yoyote msingi wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba. Katiba ni sheria kuu au sheria mama katika nchi yoyote. Sheria nyingine zote zinategemea au zinatungwa kwa mujibu wa katiba, wakati mwingine katiba hutafsiriwa kuwa ni mkataba wa kijamii kati ya watawala na wananchi (watawaliwa). Ni makubalianao ya wananchi husika juu ya ni jinsi gani taratibu za kanuni za uendeshaji wa mambo mbali mbali katika nchi yao unapaswa kuwa.  Ni muafaka wa Kitaifa juu ya misingi mikuu ya kuendesha nchi.”

Swali ambalo mimi najiuliza leo hii tutaipataje hii katiba bora? Katiba bora itapatikana tu tutakuwa na bunge bora na imara ambalo litafanya shughuli zake kwa masilahi ya wananchi wake na sio kwa kulenga kikundi Fulani au itikadi za vyama au sehemu wanazotoka.

 

 Tunafahamu kuwa  Bunge ni muhimili mkubwa sana wa demokrasia katika nchi yeyote ile ambayo inajali maendeleo na demokrasia ya wananchi wake; Katiba ya Nchi ambayo ni sheria mama katika shughuli za serikali hupitishwa na bunge maalumu ambalo huitwa bunge la katiba; ni bunge ambalo linakuwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.

Wajumbe wa bunge hili ni wawakilishi wa wananchi; bunge hili ambalo linakutana kwa muda mfupi linakuwa na ajenda maalumu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa nchi inapata katiba iliyo bora kwa taifa kwa miaka mingi ijayo.
 

Jambo la kwanza katika bunge hili ambalo limeshitua wananchi wengi ni kwa wajumbe wa bunge hili maalumu kuanza kazi kwa kuangalia masilahi yao binafsi ya kudai Posho; kwa kweli tuache utani posho ya sh 300,000 kwa siku kweli haitoshi kwa wakilishi wa wananchi ambao wanajua wananchi wao wanaishi katika mazingira magumu sana? Kama wanazuoni wengi walivyoainidha kuwa agenda nyingine ni nje na lengo na madhumuni ya mkutano huo.Suala la posho sio ajenda lakini inashngaza kwa nini imetengenezewa  kamati na kuangalia na eti wampelekee mheshimiwa Rais mapendekezo ya mjadala huo wa ongezeko la posho.

Je mbunge ambaye ni makini na anauchungu na nchi yake na amekubali kwenda Dodoma kwa ajili ya kutoa mchango wake katika kuhakikisha kuwa taifa letu linapata katiba iliyo bora anaweza kweli kukubaliana na wazo hili la ongezeko la posho? Kwa kweli hii ni kuwapotezea watanzania raslimali zao.

Kwa nini wawakilishi hao wasifikirie kuiomba serikali kuwaongezea mishahara watumishi wake ili waweze kuishi maisha yaliyo bora zaidi?

 Mwanzo huu sio mwanzo mwema kwani wajumbe hao wanatupa wasiwasi sisi wananchi kweli wanataka kutupatia katiba bora au wako pale kwa masilahi binafsi?


Nioavyo mimi nafikiri kuwa waheshimiwa wabunge wa bunge maalumu ambao wamependekezwa na wananchi na hatimaye kuchaguliwa na Mheshimiwa Raisi wazingatie kuwa wanapojadili mstakabari wa sheria kuu ambayo itaongoza nchi ni vyema wajadili na kuona umuhimu  pia kuzingatia ukweli kwamba mabadiliko yoyote humpeleka mtu upande mmoja kati ya pande mbili zinazokinzana. Kumtoa katika hali mbaya na kumpeleka katika hali nzuri zaidi, au kutoka hali nzuri na kumpeleka katika hali mbaya zaidi. Katika hali ya kawaida na kwa binadamu makini, hofu ya kupoteza, yaani kutoka hali nzuri kwenda hali mbaya huwa kubwa kuliko hamu ya kupata, yaani kutoka hali mbaya kwenda nzuri. Hili tumeanza kuliona kwani wameanza kujadiliana kuhusu wao “posho” na pia wanaangalia zaidi itikadi ya vyama vyao vinataka nini?

 
Waheshimiwa wabunge  wa bunge maalumu wajue kuwa kazi sio ngumu sana kwani wana sehemu ya kulinganisha nini watanzania wanataka kwa miaka mingine 300 inayokuja; wanayo katiba ya sasa kama wamekuwa na muda wa kuielewa na kusikiliza maoni ya wananchi basi wasipoteze mazuri yaliyopo katika katiba ya sasa, ni vizuri mabadiliko hayo yafanyike kwa umakini mkubwa. Naendelea kukumbusha kuwa katiba ni Nguzo kubwa ya demokrasia katika

Jambo nyingine ambalo limejitokeza na kuchelewesha kuanza kwa bunge hilo ni utaratibu gani utumike katika kupitisha vipengele katiba mpya je watumie kura za siri au kura za wazi. Demokrasia ya kweli iko inatakiwa iwe wazi wajumbe wasiwe na hofu ya kuonekana wasaliti na wanafiki mbele ya wananchi wao na vyama vyao. Utaratibu wowote ambao utapitishwa na wengi ndio uwe msingi wa demokrasia; kwani demokrasia ni sauti ya wengi ; japo John Locke aliwahi kuhoji je wachache je hawana nafasi katika demokrasia hata kama mchango wao ambao wanatoa ni mzuri ukilinganisha na mchango walio wengi ambao pengine huishia kufuata mkumbo?

“For one, a defining characteristic of democracy must be the people's right to change the majority through elections. This right is the people's "supreme authority." The minority, therefore, must have the right to seek to become the majority and possess all the rights necessary to compete fairly in elections—speech, assembly, association, petition—since otherwise the majority would make itself permanent and become a dictatorship. For the majority, ensuring the minority's rights becomes a matter of self-interest, since it must utilize the same rights when it is in minority to seek to become a majority again”. John Locke.

Tunawaomba wajumbe wa bunge la katiba kuvumiliana kwani kila mwakilishi anauwezo tofauti katika kujieleza. Tukumbuke kuwa Uwezo wa kusema na kujenga hoja hutofautiana kati ya mtu na mtu,  na kwa wakati huo huo anasema kwa  ya kundi lililo mchagua. Lakini tumeshajionea wenyewe kuwa wawakilishi wetu wameamua kulitumia Bunge kukidhi matakwa yao na wala sio ya wananchi wao. 

Haya yote yametupelekea tuanze kuona kuwa kuna kitu kinakosekana kwa waheshimiwa wawakilishi wetu ndani ya bunge la katiba ni dhana ya uongozi bora. Hapa wabunge wetu wanaweza wakawa na mapungufu yanayotokana na  ufahamu, ubunifu, maadili, mfano bora kwa wengine; mwajibikaji; mwenye uwezo wa kutoa ushauri.

Je wabunge wetu ambao tunategemea watuletee katiba mpya  wanajifahamu mwenyewe. Pili je  wananfahamu itikadi, uwezo, mwelekeo na malengo ya wale anawaongoza. Na tatu  wanajua mazingira ya uongozi wao.


Kwa kweli hatutamani kabisa bunge letu liwe la kifisadi na kinafiki katika jambo hili muhimu kwa taifa; kwani kwa kufanya hivyo nchi itapoteza mwelekeo kwa kukosa Katiba iliyo bora. Uongozi wa kifisadi unawavutia sana watu wenye tamaa ya mali kuingia katika siasa ili wakaibe hivyo badala ya siasa inakuwa “matumizi ya nguvu ya udikiteta”; tukikaribisha ufisadi wakati wa matayarisho ya katiba hii mpya itatupelekea nchi kukosa katiba iliyobora kwa maisha bora ya Taifa na hivyo katiba hiyo mpya itatengeneza ombwe la uongozi na kuwa kikwazo kikuu cha maendeleo.
 

Maneno “siasa na uongozi” yana maana sawa kwa maudhui ya makala hii. Nimekumbuka alichokisema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipohutubia kilele cha maadhimisho ya miaka kumi ya CCM na miaka 20 ya Azimio la Arusha mwaka 1987.

Akizungumzia dhana ya uongozi, Mwalimu Nyerere lisema, “uongozi ni kuonyesha njia.” Kwa maana hiyo, viongozi shurti wafahamu vema matokeo ya uongozi wao. Wasome imani za wanaowaongoza na nyakati zilizopo ili kutambua matumaini ya umma kimaisha. Yapasa viongozi watambue kuwa siasa njema hutatua matatizo na shida za wananchi zikiwemo zinazokwamisha maendeleo ya uchumi wa nchi na wa familia mojamoja. Siasa mbaya huangusha huduma za jamii. Kwa kuwa siasa ni uongozi, basi viongozi lazima waongoze kiadilifu, kizalendo na kwa kuzingatia hali halisi ya mambo. Wanapaswa pia kuwa wenye huruma na imani kwa wananchi.

Basi mwanasiasa yeyote katika nchi masikini kama Tanzania, anapochaguliwa kuongoza popote, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri. Atumie stadi za uongozi mwema kuonyesha njia. Tabia ya viongozi kuongoza kwa kufikiria zaidi maslahi binafsi mwiko. Viongozi wa nchi hizi masikini waangalie maisha ya Manabii ambao waliongoza karne za mwanzo za ulimwengu. Haya ni maneno muhimu sana hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba mpya.

Bunge la katiba mpya tutatamani kutowaona wajumbe wenye sura mbili, yaani waoga wa kupigania kitu bora kwa ajili ya taifa bila kujali Itikadi, dini au sehemu anayotoka na wale wanaotafuta masilahi binafsi ya  kujinufaisha wao wenyewe. Wajumbe wa Bunge maalum itakuwa vyema kama watabadilika.

 
 Bunge hili tunaomba lisiwe kama bunge la Bajeti ambalo likuwa limetawaliwa na misengwe na kulifanya lipoteze hadhi; bunge ambalo tulikuwa tunaona raha kuangalia sio hoja bali kuzomeana, kulaumiana, kunyosheana vidole; mpaka msanii mmoja akalitungia wimbo Bunge kama kariakoo,

Mambo kama haya  hayatalivusha Taifa letu  katika maisha bora tunayoyafikiria kwa faida ya Taifa letu, nafikiri itastusaidia sana kama wajumbe watakuwa wakishindana kwa hoja zitakazofanikiwa kulipatia Taifa Katiba ambayo tunahihitaji katika karne ya leo.

Bunge imara linajengwa katika msingi wa uwazi kwa kukosoana na kuheshimiana kihoja; ushindani na uchambuzi wa hoja ni sehemu muhimu sana katika kusaidia Taifa kusonga mbele; wabunge wote hawawezi kamwe kuwa na mtazamo wa pamoja; Mwenyezi Mungu ametujalia vipaji tofauti katika kufikiri na katika kutatua matatizo; Waheshimiwa wabunge wetu  ni lazima wajifunze kujenga bunge lenye ushindani wa hoja kama sehemu ya  kutatua matatizo mbalimbali. Tutaweza kushinda tu kama tutafanikiwa kujenge jamii inayotafakari na si jamii ya kulalamika kila wakati na kuishia kutukanana bila aibu.


Tunafahamu kuwa Bunge ndicho chombo cha kutunga sheria na muhimili mkuu sana wa uchumi kutokana na michango yao bungeni hasa wakati huu wa bunge la Bajeti. Bunge linatakiwa liwe na uwezo wa kuchangia na kuandaa mazingira yanayofaa kwa maendeleo yetu. Lakini Kama Bunge halina   uwezo wa kuyaangalia matatizo ya nchi hii na kuyatafutia ufumbuzi, basi, kuna tatizo kubwa katika jamii yetu, kuna tatizo kubwa ambalo kama tukibweteka, litatutafuna sisi na vizazi vijavyo.

Nafikiri linalowezekana leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina ya Muumba wetu tu;


Itafurahisha pale tunapowaona waheshimiwa wabunge wa Bunge hili maalum, bila kujali chama wakikubaliana hoja za msingi ambazo zinasaidia kujenga uzalendo wa kutetea maslahi ya  ya watanzania katika kutuletea Katiba mpya  ambayo haitafungamana na chama chochote cha siasa wala dini. Bunge letu Maalum likiweza kufanya kazi yake katika msingi huu kuondoa taswira ya BUNGE LENYE SURA MBILI NA MBAYA ZAIDI LINALOANGALIA MASALAHI BINAFSI YAKUWANUFAISHA WAO NA KUTOKUMJALI MTANZANIA WA KAWAIDA AMBAYE NDIYE WANAYEMWAKILISHA WATAKUWA WAMEWASALITI WANANCHI NA TAIFA LA TANZANIA.

 

MUNGU IBARIKI TANZANIA TUWEZE KUPATA KATIBA ILIYO BORA KABISA

No comments:

Post a Comment