WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 5, 2014

Sitta apiga jaramba kuongoza Bunge

sitta_fe8d2.jpg
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, akizungumza na mjumbe wa Bunge hilo, SamuelSitta (kushoto), ndani ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.
Dodoma. Siku moja baada ya kuteuliwa na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa Ushirikiano wa AfrikaMashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta alisema: "Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba."
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi Magharibi, AndrewChenge alisema: "Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu ndani ya CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta msuguano, basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua majina mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa kuniteua na kwa sasa najiandaa na uchaguzi."
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassanaliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi hiyo.
"Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote," alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa ushauri. Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana alisema: "Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba, angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili walionyesha nia; Sitta na Chenge.
"Wote hawa wana sifa kwa historia za maisha yao. Chenge aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sitta, Waziri wa Sheria na Katiba, halafu wote ni wanasheria. Hawa wote wakaanza kutafuta maoni kwa wenzao na kila mmoja akitafuta wenzake wa kumuunga mkono. Kwa sababu wote ni wanaCCM na kwa kuogopa makundi, tukaona tuwaite na kuwaambia jamani nyie wote ni wetu, tusingependa mkalumbane.
"Tukawaambia washauriane na kufikia mwafaka. Chenge akajitoa mwenyewe na jana (juzi), kwenye mkutano, WanaCCM wote wakaamua kumuunga mkono Sitta."
Mjadala moto bungeni.
Wakati huohuo; mjadala wa kanuni za Bunge la Katiba umeendelea kuwa moto baada ya baadhi ya wajumbe kutaka kanuni zitambue haki ya mwanamke katika nafasi hiyo ya juu ya uongozi.
Malumbano hayo yalizuka wakati wajumbe hao walipokuwa wakijadili kanuni ya saba inayohusu uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake. Mjumbe wa bunge hilo, Christine Mzava alishauri kuwa endapo mwenyekiti atakuwa mwanamume, makamu wake awe mwanamke.
Akijibu hoja hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, Magdalena Rwebangila alisema kwa kuwa sheria imetamka kuwa mwenyekiti akitoka Tanzania Bara, makamu atatoka Zanzibar, itakuwa vigumu kuweka uwiano mwingine wa kijinsia.
Baada ya ufafanuzi huo, Lediana Mng'ong'o alisimama na kusema: "Kwani mnaona ugumu gani wa kuongeza hicho kipengele? Mbona Rais katika uteuzi wa wajumbe 201 alizingatia uwiano wa kijinsia?"
Mjumbe mwingine wa Kamati ya Kanuni, George Simbachawene alisema haiwezekani kuwa na aina mbili za uwiano. Hali hiyo ilimfanya mjumbe mwingine, Dk Ave-Maria Semakafu kusimama na kuomba busara itumike na kutengua kanuni kwa kuweka nafasi sawa.
Hata hivyo, Mjumbe Ezikiah Wenje alisema itakuwa ajabu kumchagua mtu katika nafasi hizo kwa sababu tu ni mwanamke.
"Demokrasia inahitaji ushindani sawa na hao kinamama wanaamini tuko sawa. Mimi naomba kama kuna mtu ana sifa za kuwa mwenyekiti au makamu, wagombee washindane," alisema.
Maelezo hayo yaliwafanya wajumbe wanawake kusimama na kuanza kuimba: "Tunataka haki zetu, tunataka haki zetu." Kuona hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, Anna Abdallah alisimama na kuwataka wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waliopitisha sheria hiyo kujilaumu kwa sababu walipaswa kuliangalia hilo.
Chanzo, mwananchi

No comments:

Post a Comment