WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, March 18, 2014

Sitta: Pigo la kwanza

  Bunge Maalum la Katiba lavurugika
  Ni madai ya kuchakachua kanuni

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, akizungumza wakati akimkaribisha Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili ahutubie wajumbe wa Bunge hilo bungeni mjini Dodoma jana.Hata hivyo hotuba hiyo ilishindikana baada ya zomea zomea kutoka kwa baadhi ya wajumbe wakipinga Jaji Warioba kutoa hotuba hiyo hadi Rais azindue Bunge hilo kwanza.(Picha na Khalfan Said)
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, jana alianza vibaya kazi ya kuongoza hilo baada ya baadhi ya wajumbe kugoma kusikiliza taarifa ya Rasimu ya Katiba Mpya iliyokuwa iwasilishwe na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Hali hiyo ilitokea dakika chache tu baada ya Sitta kumtaka Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah kutangaza utaratibu unaofuata, akitangaza kuwasilishwa kwa Rasimu hiyo.

Hata hivyo, Bunge hilo liliahirishwa saa moja baadaye baada ya Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad, kutangaza kuahirishwa kwa Bunge hilo hadi hapo wajumbe watakapotangaziwa baadaye.

“Wajumbe Bunge limeahirishwa hadi hapo mtakapopewa taarifa baadaye, tunaomba muondoke ndani ya ukumbi huu,” alisema.

“Tutawatangazieni wakati tutakapokuja kuendelea na kikao cha Bunge. Waheshimiwa leo ninawaomba tutawanyike,” aliongeza.

Awali kabla ya kuahirishwa kwa Bunge hilo, Sitta alisimama na kumuomba Jaji Warioba kwenda mbele ya Bunge kuwasilisha taarifa yake.

Hata hivyo, baada ya tamko hilo la Mwenyekiti.  Profesa Ibrahim Lipumba, alisimama kuomba mwongozo akifuatiwa na Moses Machali, ambao hata hivyo, hawakusikilizwa na Mwenyekiti aliwataka kuketi kwa kuwa alisema hakuna mwongozo kwenye suala hilo.

Wengine waliosimama ni Freeman Mbowe, James Mbatia na Mchungaji  Christopher Mtikila.

 Hatua hiyo ilisababisha wajumbe wengine wa Umoja wa Wanaotetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimama na kugonga meza huku wakipasa sauti ya “Fuata kanuni mwenyekiti, tutaendelea hivi hadi utakapoacha kuvunja kununi.”

Inayodaiwa kuvunjwa ni kanuni ya 7 (1) h, ambayo inaelezea uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi ilitakiwa ianze, lakini ilitenguliwa ili kuruhusu Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo.

Wakati hayo yakiendelea Jaji Warioba alikuwa amesimama sehemu aliyotakiwa kuwasilisha taarifa yake kwa dakika tano bila kuanza kuisoma huku akiwa amepigwa butwaa kutokana na makelele yaliyotawala ndani ya ukumbi huo.

Licha ya makelele ya wajumbe hao, Sitta aliendelea kumsisitiza Jaji Warioba aendelee kuwasilisha taarifa yake, lakini ilishindikana kutokana kelele za zomea zomea kuongezeka na kumsababisha Jaji Warioba kuondoka mbele na kwenda kuketi sehemu maalumu waliyopangiwa  wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kufuatia hali hiyo, Sitta alisimama na kusema: “Katika mazingira haya hatuwezi kuendelea, naomba kutangaza kuahirisha Bunge kwa sasa hadi hapo tutakapotangaza baadaye.”

Baada ya kutamka hayo, Sitta alitoka nje ya ukumbi na baadaye kupita sehemu ya waandishi wa habari kuelekea kwenye chumba cha kikao.

Wakati akipita kwenye chumba cha waandishi wa habari akiwa ameongozana na Naibu Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, waandishi hao walimpa pole Sitta, naye alijibu: “ndiyo demokrasia yenyewe.”
Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wajumbe ndani ya ukumbi huo walionekana kurushiana maneno ya kushutumiana na kuonyeshana ishara za kudharauliana.
NIPASHE ilishuhudia mmoja wa wajumbe hao, Avemaria Semakafu, akirushiana maneno na mjumbe mwingine Abdallah Juma (CUF) ndani ya ukumbi.

Hata hivyo, walisuluhishwa na wajumbe wengine huku Juma akitolewa nje.

Awali kabla ya kuanza kwa kikao cha jioni, wabunge ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitishia kwamba wangesusia kuingia kwenye kikao hicho kwa ajili ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni.
Walisema kuwasilishwa kwa taarifa hiyo kabla ya Rais kulizindua Bunge hilo ni uvunjaji wa sheria na ukiukwaji wa kanuni za Bunge hilo.
LIPUMBA

Mwenyekiti wa Ukawa, Prof. Ibrahim Lipumba alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa kitendo cha Mwenyekiti kuruhusu Jaji Warioba awasilishe Rasimu ya Katiba bungeni kabla ya Rais kuzindua Bunge hilo ni uvunjwaji wa Sheria na Kanuni za Bunge hilo na kwamba wao hawawezi kuuvumilia.

Alisema waliamua kumwandikia barua Sitta kupinga ukiukwaji huo na kumtaka abadili ratiba hiyo kabla hawajaamua kuchukua hatua zaidi.

Prof. Lipumba alisema kuwa Ukawa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona kuwa kumekuwapo na mwendelezo wa matukio ya ukiukwaji wa kanuni wa makusudi tangu Sitta alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo.

“Tunapenda kukufahamisha kwamba hatuko tayari kuendelea kukaa kimya wakati unaendelea kuvunja kanuni za Bunge Maalum na kupelekea mkutano wa Bunge Maalum kuwa hatarini kuvunjika,” alisema Prof. Lipumba.

Alisema kuwa kwa sababu ya ukiukwaji huo wa kanuni za Bunge Maalum, wanachama wa Uwaka hawako tayari kuunga mkono na watapinga kwa kadri ya uwezo wao mambo makubwa manne.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba na Mwenyekiti Tume ya Madiliko ya Katiba kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais wa Zanzibar kufungua Bunge Maalum na semina yoyote itakayoongozwa na wataalamu wa ndani au nje ya nchi kama lilivyotangaziwa Bunge Maalum.

Mambo mengine ni hotuba ya mgeni rasmi kama itafuatia uwasilishwaji wa Rasimu na jambo lingine lolote linalokiuka kanuni za Bunge Maalum.

Alisema Ukawa wamekwisha kufanya jitihada mbalimbali za kufikisha msimamo wao kwa Mwenyekiti, ikiwa ni pamoja na kumfuata ofisini kwake, kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu (sms) kupitia simu yake ya mkononi pamoja na barua pepe kuhusiana na suala hilo, lakini pamoja na jitihada hizo bado hajataka kuwasikiliza.

MBATIA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kuwa kinachoonekana ni kwamba Sitta anakalia kiti cha Mwenyekiti wa Bunge siyo kwa kutimiza matakwa ya wananchi bali kwa kutetea maslahi ya Chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kuwa Bunge la Maalum la Katiba ni bunge kubwa zaidi ya lile la Jamhuri ya Muungano kwa kuwa ndilo linalojenga nchi, hivyo Sitta anapaswa kuachana na ujanja ujanja wa kukipendelea chama chake badala yake afanye kazi kwa maslahi ya taifa.

Alisema wananchi watambue na kuelewa kuwa chochote kibaya kitakachotokea ndani ya Bunge ikiwamo kuvunjwa kwa bunge hilo au wao kususia kuingia bungeni anayepaswa kulaumiwa ni Sitta na CCM.

Baada ya kusitishwa kwa shughuli za Bunge hilo, baadhi ya wabunge wakizungumza nje ya ukumbi wa Bunge wlikuwa na maoni tofauti, huku baadhi yao wakilaani kitendo kilichofanywa na wabunge wenzao na wengine wakiwaunga mkono.

MLAKI
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ritha Mlaki, alisema kitendo kilichofanywa na wenzao wa upinzani ni cha aibu kwa vile kinalidhalilisha Bunge kwa wananchi.

Alisema kuwa kwa kitendo hicho, Bunge linapaswa kumwomba radhi Jaji Warioba ambaye alikwenda bungeni akiwa tayari amejiandaa kuwasilisha rasimu hiyo, lakini wabunge wakaonyesha kutokuwa tayari kumsikiliza.

ANDUGULILE
Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Andugulile (CCM), alisema wabunge waliofanya kitendo hicho hawakutumia busara, kwa kuwa hata kama kanuni imekiukwa, lakini sheria inaruhusu rasimu hiyo kuwasilishwa bungeni hata kama Rais hajazindua Bunge hilo.

MNYAA
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF), alisema wabunge wanachohitaji ni kuona Bunge hilo linaendeleshwa kwa kufuata kanuni walizozitunga wenyewe na siyo kuburuzwa kama ambavyo Mwenyekiti wao anavyotaka kufanya.

Alisema kuwa tangu Sitta alipochaguliwa amekuwa akikiuka kanuni hizo na kuweka mambo yake licha ya kuwa wakati wa uandaaji wa kanuni hizo na yeye alikuwapo, lakini hakuwasilisha maoni yake.

MAKONDA
Paulo Makonda alisema kitendo hicho cha vurugu bungeni kinatokana na wabunge wa kambi ya upinzani kujawa na ushabiki wa kisiasa kuliko kufikiria utengenezaji wa Katiba.

MAHALU
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Prof. Costa Mahalu, alisema kuna haja ya kukaa wabunge wote kwa pamoja ili kupata maridhiano badala ya kuendelea kuvutana ndani ya ukumbi wa bunge.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusiana na nini kinastahili kuanza kati ya uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba na uzinduzi wa Bunge hilo, Prof. Mahalu alisema hawezi kuzungumzia suala hilo.

KANUNI ILIVYOTENGULIWA
Jana asubuhi, Sitta aliomba kutenguliwa kwa kanuni inayomruhusu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwasilisha taarifa yake kabla ya Bunge hilo kuzinduliwa rasmi na Rais.

Wakati akiomba kutenguliwa kwa kanuni, Sitta alisema:  “Kifungu cha 20 cha sheria ya Bunge Maalum kifungu kidogo cha 4 kinaturuhusu kumuita Mwenyekiti wa Tume au mjumbe yeyote wa Tume wakati wowote mwingine ili tukiendelea na mjadala hapa aje kutusaidia ama kwenye kamati au kwenye bunge zima.”

WEREMA AWASILISHA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema kwa kutumia kanuni ya 85, aliombwa kutengua kanuni husika  ili bunge liweze kupokea rasimu na kumpokea mgeni rasmi anayewasilisha Rasimu hiyo kuingia ndani ya ukumbi wa bunge.

Akitengua kanuni hiyo Jaji Werema alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  anawajibika kuwasilisha taarifa yake kwenye bunge kwa mujibu wa kanuni ya 7 fasiri ya 1 (h) uwasilishaji wa rasimu hiyo ungepaswa kufanyika baada ya hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi na kwa mujibu wa kanuni 85 fasiri ya 4 (d) Bunge laweza kutengua kanuni kwa kuongeza shughuli yoyote ambayo haiukuwapo kwenye mpangilio wa orodha hiyo.

Aliomba kanuni hiyo itenguliwe ili kuwahisha shughuli ya kupokea Rasimu ya Katiba hiyo ifanyike jana jioni, hoja ambayo iliungwa mkono na wajumbe wengi

Imeandikwa na Beatrice Bandawe, Emmanuel Lengwa na Ashton Balaigwa
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment