WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 12, 2014

Sitta:Nina jibu la kura ya siri

  Apata wapinzani watatu uenyekiti wa Bunge
  Hataudhuria vikao vya CCM akiwa M/kiti

 
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (kulia), akipokea fomu za kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo kutoka kwa Katibu Muhtasi wa Katibu wa Bunge, Lydia Mwaipyana, mjini Dodoma jana. Wengine ni Wajumbe wa Bunge hilo, Dk. Hamis Kigwangallah (wa pili kushoto) na Paul Makonda.PICHA: SELEMANI MPOCHI
Wajumbe  wanne wamechukua fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge Maalum la Katiba utakaofanyika leo, akiwamo Samwel Sitta, ambaye amesema ana ufumbuzi wa jinsi ya kupiga kura katika bunge hilo kati ya wazi na siri.
Pamoja na Sitta wengine waliochukua fomu hadi jana alasiri ni Hashim Rugwe, John Lifa Chipaka, na Dk. Theresia Huvisa huku Sitta akisambaza vipeperushi vinavyoelezea dira, elimu, uongozi, mafanikio na mtazamo binafsi.

Dk. Huvisa alichukua fomu saa 6:00 mchana wakati Sitta akichukua saa 7:15 mchana, akiwa amefuatana na wajumbe wa Bunge hilo, Dk. Hamis Kigwangala na Paul Makonda ambayo alikabidhiwa na ofisa wa Bunge, Lidya Mwaipiana.

Baada ya kuchukua fomu hiyo, Sitta alizungumza na waandishi wa habari na kuweka bayana msimamo wake na jinsi atakavyoongoza Bunge hilo iwapo atachaguliwa.

KURA YA SIRI

Alisema hadi sasa ana jibu la kanuni ya 37 na 38 na kwamba hawezi kulisema hadi hapo atakapokalia kiti hicho.

“Mara baada ya kushika kiti kama nikifanikiwa kutakuwa na kamati ya uongozi ambayo wajumbe wake ni wenyeviti wa kamati zote, mapema

tutashauriana ...tayari nina mawazo yangu jinsi ya kuondoka hapo (kura ya siri au wazi), siwezi kusema maana yanasubiri vikao,” alisema.

Sitta alisema jingine ni kuwa anaruhusiwa kuunda kamati ya mashauriano kwa mambo magumu, hivyo ataitumia.

Alisema Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho, aliwasikiliza wengi kwa kadri alivyoweza na kamati ya kanuni na kumshauri ina wajumbe ambao atawatumia kuendesha Bunge hilo.

Kama atachaguliwa leo, ataanza kukutana na kamati ya mashauriano na mwenyekiti wa muda ili waanze kushughulikia suala la kura ya siri au ya wazi mapema.

Alisema anatarajia kwamba mchakato utakwenda vizuri na atafanya vizuri zaidi kwa kuwa amejifunza tofauti na alivyokuwa Spika wa Bunge la Tisa.

“Ukiwa nje na kutazama unapata mengi ya kujifunza zaidi, umri umeongezeka, nitakuwa na subira zaidi... natambua ndani ya Bunge tunao ambao hawana uzoefu na mambo ya Bunge, tutawachukulia kwa kuwa wanawakilisha wananchi,” alisema.

Alisema kwa hali hiyo ni lazima kuendesha Bunge hilo kwa mtindo wa kuleana, vinginevyo mwenyekiki akiwa mkali sana wa kanuni, wajumbe 201 na wengine  watajisikia hawakupewa fursa na uhuru kamili.

Alisema matarajio yake ni kuwa na mjadala mzito na kwamba atatoa kipaumbele kwa wajumbe ambao hawajazungumza kutoka katika kundi la 201 kwa kuwa wamejifunza kwenye mchakato wa kanuni.

Sitta alisema anatarajia katiba itakayopatikana itakuwa ya mfano na nchi nyingine kuja kujifunza, na kwamba bunge hilo haliwezi kuvunjika kwa kuwa wengi wanadhamira ya kufika pazuri na kutoonekana wapuuzi waliotumia gharama kubwa, lakini wakashindwa kufika miezi mitatu na kuwapa wananchi katiba ya kuipigia kura.

“Nitahakikisha hatufiki huko, naelewa wapo wachache pande zote za Muungano hawautaki Muungano, baadhi yao nimewasikia wakisema, wana jitihada za kuvunja majadiliano, kanuni zipo tutahakikisha matakwa ovu ya wachache hayawezi kutushinda, tunataka katiba nzuri inayolinda Muungano na kuleta matumaini mapya kwa rika la vijana,” alisema.

Alisema ukishaweka msingi mzuri wa katiba ni dawa dhidi ya sheria mbovu na kwamba moja ya matatizo ya katiba iliyopo sasa inaachia mianya kwa watu kujifanyia watakalo, uwajibikaji mdogo na kwamba Rasimu ya Katiba inasisitiza utumishi kwa umma kwa kuwajali wanyonge.

“Tutapata baraka na mshikamano, ikiwa wanyonge wataona viongozi wao wanahangaikia matatizo halisi yaliyopo ya vijana, makundi maalum, wanawake wa vijijini na mijini, waone katiba mpya itakuwa na makali ya kutosha kuzuia uzembe na rushwa,” alifafanua.

Alisema pia katiba itakayosaidia mahakama iwe makini zaidi kwa kutoa adhabu stahiki kwa watu wanaofanya mambo ya ovyo.

MATAKWA YA CCM
Alisema yeye ni mwanachama wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, lakini kanuni hazimruhusu kuhudhuria vikao vya chama chake kwa kipindi chote nitakachokuwa Mwenyektii wa Bunge hilo.

“Watakayoamua huko watafute namna ya kunifikishia ... kama hayatendi haki, wajibu wa mwenyekiti ni kutenda haki tu, sitarajii kupindisha mambo kwa makusudi ili kusaidia chama changu, yenye hoja ndiyo yatapita kwa kuwa tunashindanisha hoja, kama hakuna dunia itanishangaa, nitatenda haki na kusimamia hoja,” alisema.

KAZI ZOTE KWA VIWANGO NA KASI

Alisema viwango na kasi ni sehemu ya maisha yake na kwamba Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayoiongoza anaisimamia kwa kwenda na viwango hivyo, hata Bunge ataliongoza kwa utaratibu huo.

MUUNDO WA MUUNGANO

Alisema ni muumini wa serikali mbili na kwamba  bila kutatua matatizo yaliyomo ndani yake, hazibebeki.

“CCM imekuja na hoja nane za kutetea serikali mbili... tusubiri yatazungumzwa ndani ya bunge... sitaki niseme hoja zao zitashinda bali tusubiri ndani ya bunge,” alisisitiza.
Sitta alisema wajumbe watashindana kwa hoja na wenye hoja nzito ndio watakaoshinda na kazi ya mwenyekiti ni kusimamia suala hilo liende vizuri.
 Alisema maoni yake yatakuwa ni sehemu ndogo ya mjadala na kwamba yeye hatoi maoni yoyote wakati wa uendeshaji wa vikao.

UCHAGUZI WA MWENYEKITI
Jana asubuhi mara baada ya azimio la kupitisha Kanuni kusomwa, Kificho alitangaza zoezi la uchukuaji fomu wa nafasi ya mwenyekiti.

 “Napenda kuwafahamisha kuwa kesho (leo) kutakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge Maalum, utafanyika baada ya wanaopenda kuwania nafasi hiyo kuchukua fomu za maombi ya nafasi hiyo,” alisema Kificho.

 Kificho aliwataka wenye nia kuchukua fomu na kuwa zitapashwa kurejeshwa leo saa 4:00 asubuhi na kufuatiwa na uchaguzi jioni.

WAJUMBE WAMFUNDA MWENYEKITI

Baadhi ya wajumbe wametoa maoni kuhusu sifa za mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo huku  Kangi Lugola akisema ana wasi wasi kama mwenyekiti huyo atatenda haki kwa kuwa mwenyekiti wa muda hakuwafikisha salama kwa kuwa vifungu muhimu vimewekwa kiporo.

NGELEJA
William Ngeleja, alisema ni vyema apatikane mwenyekiti ambaye atasimama juu ya itikadi za kivyama na kuendesha kwa mujibu wa kanuni, mzalendo, weledi na mwenye kusimamia maslahi ya taifa na kukidhi matarajio ya Watanzania kwa kuja na katiba itakayokidhi mahitaji ya sasa.

MPACHU

Amon Mpachu alisema mwenyekiti awe mwenye hekima na busara na atakayekuwa tayari kuendana na matakwa ya kanuni.

SARUNGI

Maria Sarungi alisema mwenyekiti aweke maslahi ya taifa mbele na kuweka nyuma ushabiki wa kisiasa na kuwaunganisha wajumbe na kufanya maamuzi magumu kwa wakati mwafaka.

NYAGWINE
Nyambari Nyagwine alisema mwenyekiti atambue kuwa ataongoza watu wenye fikra na akili timamu, hivyo wanapaswa kumpa changamoto ili yapitishwe maamuzi sahihi.

LISSU

Tundu Lissu alisema mwenyekiti ajaye anapaswa kutembea kwenye kanuni za kuongoza bunge hilo na kuwezesha Watanzania kupata katiba itakayokuwa na jibu la matatizo yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment