WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 13, 2014

Sitta aja na ‘falsafa’ ya chura

samwel-sitta1_1fadd.jpg

Dodoma. Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amechaguliwa kwa kishindo kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba, huku akisema kuchaguliwa kwake ni sawa na kumrudisha chura kwenye dimbwi la maji.
Jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata kura 487 na kumbwaga mpinzani wake, Hashimu Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma aliyepata kura 69.
Wajumbe wengine, Dk. Terezya Huvisa pia wa CCM na John Chipaka wa Tadea, walijitoa katika kinyang'anyiro hicho ambacho tangu awali Sitta alionyesha kujiandaa kwa kutengeneza vipeperushi alivyovisambaza kwa wajumbe kama sehemu ya kujinadi.
Akizungumza na wajumbe ambao muda mwingi walikuwa wakimshangilia, Sitta alionekana kujiamini kabla na baada ya uchaguzi. Pia alitumia misemo lugha ya picha ikiwamo ya chura kuishi majini, akimaanisha kuwa wajumbe wamemchagua mtu mwenye uwezo, uzoefu na weledi wa kuongoza shughuli za Bunge.
"Jamani kunichagua mimi ni kama kumrejesha chura kwenye dimbwi la maji alilolizoea. Msiwe na wasiwasi ataogelea tu na ninawaahidi kuwa ikiwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu, mtanichagua nitawatumikia kwa uaminifu, sitakubali upendeleo wa aina yoyote, nitasimamia kanuni tulizozipitisha hapa," alisema.
Aliongeza kusema: "Nitawaongoza kwa utumishi uliotukuka na uadilifu ili tupate Katiba bora, yenye viwango na kwa wakati. Nina hulka ya kuwapenda wale ninaowaongoza, kwa hiyo nitakuwa mtetezi wa shughuli mbalimbali...Ninawaahidi Watanzania kutenda haki na kuwapatia Katiba yenye viwango na kwa wakati.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiongozwa na falsafa yake ya Bunge la kasi na viwango. Pia anatajwa kufanikiwa kuliongoza Bunge hilo kwa weledi wa hali ya juu.
Kwa sababu ya mafanikio hayo, alipokuwa akiomba kura za wajumbe wa Bunge hilo, hakusita kujifananisha na chura kurudi majini.
Aidha, alisisitiza kuwa ataliongoza Bunge kwa kutumia falsafa yake ya kasi na viwango, huku akiahidi kulisimamia Bunge kwa haki na bila upendeleo kwa kundi lolote.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk. Thomas Kashillilah, alisema Sitta alipata kura hizo 487 ambazo ni sawa na asimilia 86.5, kati ya kura 563 zilizopigwa.
Dk Kashillilah alisema kwamba mpinzani wa Sittta, Hashim Rungwe ambaye jana tulimwandika kimakosa kuwa anatoka NCCR- Mageuzi alipata kura 69, sawa na asilimia 12.3 ya kura zote. Alisema kura saba ziliharibika.
Moja ya mambo yaliyovuta hisia za wajumbe wengi ni hatua ya Sitta kushikana mikono ya kupongezana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya kumaliza kuomba kura kutoka kwa wajumbe.
Sitta na Chenge
Akitoa shukurani zake baada ya kuchaguliwa, Sitta alisema hana uhasama wowote na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye naye awali alikuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo kabla ya kujitoa.
"Namshukuru pia ndugu yangu Andrew Chenge ambaye watu walivumisha kwamba tulikuwa na mchuano wa uhasama ndani ya chama, jambo ambalo siyo kweli, "alisema na kuongeza;
"Mheshimiwa Andrew Chenge tuna historia ndefu sana, nikiwa Waziri wa Katiba na Sheria mwaka 1993, mimi ndiye niliyependekeza jina kwa Rais wa Awamu ya Pili, Rais Ali Hassan Mwinyi ili ateuliwe kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali." alisema.
Kwa upande wake, Chenge alisema: "Mambo yote yaliyozungumzwa na Sitta ni mambo yaliyopita, kilichopo ni kutazama kazi iliyo mbele yetu.''
Nyongeza na Beatrice Moses, Dar es Salaam
chanzo: mwananchi

No comments:

Post a Comment