WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 28, 2014

Loga: Azam tishio Simba kuliko Yanga

Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Mcroatia,Zdravko Logarusic
Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Mcroatia, Zdravko Logarusic, amesema mechi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Azam itakayofanyika Jumapili ni ngumu na inampa mawazo kwa kuwa anaihofia timu hiyo kuliko hata Yanga.
Logarusic alisema Azam iko katika kiwango cha juu na ushindi mfululizo wanaoupata unawaongezea hali ya kujiamini tofauti na kikosi chake ambacho kimekuwa kikipoteza mara kwa mara.

Kocha huyo alisema pia umuhimu wa pointi tatu za kuamua hatma ya ubingwa kwa wapinzani wao ndicho kinampa wasiwasi zaidi wakati wachezaji wake wanatafuta heshima.

"Ni ukweli usiofichika kwamba mechi hii ni ngumu, ninawahofia zaidi Azam kuliko Yanga," alisema Logarusic.

Alieleza kwamba amekiandaa kikosi chake kukabiliana na ushindani wa kila aina katika mchezo huo na anaamini wapinzani wao pia wamejipanga.

Aliongeza kuwa bado Simba inahitaji kushinda licha ya kutokuwa na matumaini ya kumaliza kwenye nafasi mbili za juu msimu huu unaomalizika Aprili 19.

Naye Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongala, alisema kikosi chao kimejipanga kuendelea kufanya vizuri katika mechi za ligi zilizobakia ili waweze kutimiza malengo yao.

Ongala alisema wanaifahamu vyema timu ya Simba na wachezaji wake wanajua jinsi ya kuwakabili na hatimaye kupata ushindi katika mchezo wao wa Jumapili.

"Tumejipanga kufanya vizuri na kila siku tunaendelea kurekebisha makosa katika timu, lengo ni kuchukua ubingwa msimu huu," alisema kocha huyo msaidizi.

Simba itashuka dimbani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha  bao 1-0 dhidi ya Coastal Union wakati Azam wenyewe walipata ushindi wa mabao 2-0 ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani kwa kuifunga JKT Mgambo.

Wekundu wa Msimbazi wana pointi 36 na Azam ndiyo vinara wa ligi wakiwa na pointi 50 wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga wenye pointi 46 na mechi moja mkononi huku Mbeya City ikishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 42.

Simba bado inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kinesi ulioko Sinza, jijini Dar es Salaam na Azam ilirejea jana ikitokea Tanga.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment