WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 5, 2014

Wana-CCM wanahofia nini kura za siri?

bungeni_96a23.jpg
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza bungeni Dodoma juzi. Picha na Emmanuel Herman.
Suala la utaratibu upigaji kura kwenye Bunge la Katiba limeibua mjadala mkali na kugawa wajumbe kwa wale wanaotaka kura ya wazi na wale wanaotaka kura ya siri.
Dodoma. Kwa muda wa takriban siku 16 sasa, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamekuwa katika njiapanda kuhusu kupiga kura ya siri au ya wazi katika kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba.
Kiini cha mvutano huu ni hatua ya wajumbe wengi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutetea kwa nguvu zote, kura ya wazi huku makundi mengine yakitetea mfumo wa kura ya siri.
Wajumbe wengi wa CCM wanadai kuwa hakuna sababu ya kuwa na usiri katika upigaji kura huo na kwamba itakuwa demokrasia zaidi kwa kupiga kura ya wazi ili kila mwananchi ajue nani kapiga kura gani.
Wanachokitaka CCM sasa hakina tofauti na kile alichokifanya Rais Daniel Arap Moi mwaka 1988 alipoamua kuanzisha kura iliyojulikana kama 'Mlolongo Voting' au 'Mlolongo System'.
Chini ya utaratibu huo, wapiga kura walipanga foleni nyuma ya picha ya mgombea wanayemtaka na baadaye mtu alikwenda na kuhesabu idadi ya watu waliosimama nyuma ya picha na kuandika matokeo.
Utaratibu huo ulilaaniwa duniani kote kwamba ulikuwa una lengo la kuwatisha wapigakura na ulikuwa ukibana demokrasia katika taifa hilo ambalo wakati huo lilikuwa na watu milioni 20.
Kutokana na mfumo huo ambao uliwafunga wapigakura kutokutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi wanayemtaka kwa siri, ni asilimia 32 tu ya Wakenya waliojitokeza kupiga kura.
Leo miaka 26 baadaye, CCM inatumia nguvu kubwa kutaka mfumo kama huo.
CCM wameanzisha jambo hili kwa staili tofauti, tena katika jambo zito na la maridhiano kama la kupata Katiba Mpya.
Kwa akili ya kawaida kabisa ambayo haihitaji kuwa na Shahada ya Chuo Kikuu, mpango huo wa CCM, ni dalili za woga na vitisho ili wajumbe wake wenye mtazamo tofauti, wafyate mkia wasikiuke msimamo wa chama hicho.
Kwa wiki ya pili, imekuwa shida kuuelewa msimamo huo wa CCM, ambao unaweza kuufananisha na kinyonga ambaye hubadilikabadilika rangi kulingana na mazingira alipo.
Miaka 50 tangu Tanzania ijipatie uhuru wake, nathubutu kusema Serikali ya CCM imeendesha mambo yake kwa usiri mkubwa, lakini ghafla leo imebadilika inataka uwazi. Ina hofu gani?.
Nasema imeendesha mambo yake kwa usiri mkubwa kwa sababu mikataba yote iliyoiletea nchi hii matatizo ikiwamo ya rasilimali ya madini, imeingiwa kwa usiri mkubwa tena mingine nje ya nchi.
Hata hivyo, leo linapokuja suala la upigaji wa kura kupitisha katiba yetu, CCM 'wameokoka'; hawataki tena usiri bali uwazi. Waswahili wanasema: "Fumbo mfumbie mjinga mwerevu atagundua."
Tusidanganyane katika hili, CCM wanataka kuwashughulikia wajumbe wao ambao watakwenda kinyume na misimamo ya chama hicho ambayo tayari inafahamika kwa Watanzania wote.
Nani asiyejua kuwa viongozi wa CCM wanatoka hata 'mapovu' midomoni kupinga kwa nguvu zote muundo wa Serikali tatu, ambayo ndiyo mapendekezo ya Watanzania wengi.
Upo ushahidi wa wanachama 'walioshughulikiwa' na chama hicho kwa kile kinachodaiwa kutumia uhuru wao kuweka wazi misimamo yao ya kukataa kuburuzwa na CCM katika suala hilo.
Sawa, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 pamoja na kanuni zinazopendekezwa zinatoa kinga kwa mjumbe kwa kile atakachokisema ama kukifanya ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
Ukweli ulio wazi ni kuwa CCM wana mbinu nyingi za kuwashughulikia wale wanatofautiana nao kimtizamo.
Kubwa linalofanyika ni kukata jina lake anapogombea urais, ubunge na hata udiwani.
CCM wanalazimisha kwa nguvu zote utaratibu wa kura za wazi kwa kuwa ndani ya chama hicho, tayari kuna mgawanyiko mkubwa kuhusu muundo wa Muungano.
Baadhi ya wajumbe tayari wameonyesha misimamo ya kwenda kinyume na misimamo hiyo ya CCM. Walioamua kukitosa chama hicho wana sababu moja tu; wanataka kusimama na wananchi wao.
CCM wafahamu kuwa hata wakitumia wingi wao ndani ya bunge hili.
Kama ni chama kinachojiamini kwamba msimamo wake unakubalika ndani na nje ya Bunge hilo, kinahofia nini ikitumika kura za siri? Kwa nini inageuka kinyonga katika baadhi ya mambo?
Kama CCM wanaona wengi wanataka kura ya wazi, basi ushauri wa Anne Kilango Malecela wa kupiga kura za siri ili kuamua kama itumike kura za siri ama za wazi, ulikuwa mwafaka.
Kwa mwenendo huu wa CCM, nina mashaka kama chama hicho kina dhamira ya dhati ya kuwapatia Watanzania, Katiba bora na kwa wakati kwa sababu mvutano huu ukiendelea, Bunge linaweza kuvunjika.
Sitashangaa, kama CCM watafurahia kuvunjika kwa Bunge hili ili turudi kwenye muundo wa Serikali mbili ambao wao ndio wanautaka kwa sababu tu ya masilahi yao na si masilahi ya wananchi.
Hata hivyo, ikishindikana, wajumbe wa CCM wafanye uamuzi mgumu hata kama ni kura ya wazi. Wapige kura ya wazi kwa masilahi ya Watanzania kwa sababu wataingia kwenye vitabu vya kumbukumbu.
CCM inaweza kufutika katika historia ya nchi hii, lakini Utanzania utadumu milele na milele.
Chanzo, mwananchi

No comments:

Post a Comment