WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 28, 2014

Mwenendo huu Bunge la Katiba haufai,unawagawa Watanzania

Katuni
Hali  iliyopo sasa kwenye vikao vinavyoendelea vya Bunge Maalum la Katiba inatia shaka. Inawaogopesha Watanzania wengi, hasa wale waliojawa na shauku ya kuona kuwa taifa linapata katiba bora kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Sisi ni sehemu ya Watanzania tulioingiwa na hofu kubwa juu ya kile kinachoendelea kwenye vikao vya bunge hili.

Kauli zinazotolewa ndani na nje ya Bunge hilo haziashirii mwisho mzuri. Hakika, misukosuko ndani ya Bunge hilo inaonekana kuwa mingi kiasi cha kutoa ishara mbaya juu ya ufanisi wa chombo hicho ambacho kimsingi, kina wajibu wa kupitisha rasimu ya katiba mpya kabla ya kutoa nafasi ya kupigiwa kura na wananchi.

NIPASHE tunaona kuwa hivi sasa, badala ya kutumia muda mwingi wa kuijadili na kuipitisha rasimu ya katiba, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakipigana vijembe na kubishana kwa mambo yanayozidi kuwagawa wenyewe na taifa.

Tofauti kubwa za kimtazamo baina ya wajumbe zinapata nafasi kubwa zaidi. Ni dhahiri kuwa, kama hatua zisipochukuliwa mapema katika kumaliza mabishano ya mara kwa mara, ni wazi kwamba hakutakuwa na mafanikio. Katiba bora haitapatikana na badala yake, taifa litazidi kugawanyika kutokana na misimamo ya vyama.

Kwa bahati mbaya sana, badala ya wajumbe wa Bunge la katiba kujielekeza katika masuala yatakayoleta katiba bora, wengi wao wamekuwa wakionyesha waziwazi kuwa wanapigania zaidi maslahi ya vyama vyao.

Kwa mfano, kila uchao, wajumbe wa Bunge hili wamekuwa wakipeana vijembe baina yao, vingi vikionekana kujawa na mitazamo ya kisiasa. Upo ushahidi wa kutosha vilevile kuwa wajumbe wengi wamekuwa wazuri katika kuibuliana tuhuma.

Wengi miongoni mwa wale wanaopata nafasi ya kuzungumza wamekuwa wakimwaga tuhuma. Kiti pia kinaonekana kuyumba.
Nacho kimeanza kutuhumu. Hiyo ilidhihirika juzi baada ya Mwenyekiti wa Bunge kutoa yake ya moyoni, akisema kuwa wanaoyumbisha mwenendo wa bunge hilo ni baadhi ya watu waliodhamiria kuona kuwa mchakato wa kupitisha rasimu ya katiba mpya unakwama.
Na sasa, hali ya kutuhumiana huko imefika mbali zaidi.Ni baada ya Waziri Mkuu kueleza yake, akisema kuwa kutokana na mwenendo unaoonekana sasa, anafikiria kumuomba Rais aliyeunda Bunge hilo kuliahirisha hadi wakati mwingine ili kutoa fursa kwa masuala mengine ya Kiserikali kuendelea. Waziri Mkuu alikuwa akizungumzia mkutano wa Bunge la Bajeti ambao unapaswa kuanza baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba.

Sisi tunaona kuwa chanzo cha mkanganyiko unaoendelea sasa kwenye Bunge la Katiba ni kimoja tu, nacho ni hali ya kutoaminiana. Wajumbe wamekuwa hawaaminiani. Matokeo yake wanaishia kutuhumiana hata kwa mambo ya wazi na yasiyohitaji kubishana.

Ushauri wetu kwa wajumbe wa Bunge la Katiba ni kuwa, wajitahidi kutanguliza utaifa na wala siyo vyama vyao. Wakumbuke kuwa Watanzania waliwapa fursa ya kwenda kwenye Bunge hilo kwa nia ya kuwaandalia katiba bora na siyo kuimarisha vyama vyao.

Wajumbe wa Bunge la Katiba wakumbuke vilevile kuwa Watanzania wanawaangalia, teknolojia ya matangazo ya moja kwa moja ya televisheni inawaonyesha wote mbele ya umma ambao bila shaka, kuna siku utawahukumu kwa kuonyesdha mapenzi zaidi kwa vyama vyao kuliko taifa. Ni vyema wakaacha kufanya mambo yasiyokubalika.

Tunawasihi wajumbe wa Bunge la Katiba kuwa, mara zote wajitahidi kufanya kazi yao kwa umakini mkubwa ili mwisho wa siku waipatie Tanzania katiba bora. Kinyume chake, itakuwa ni janga kubwa kwa taifa.

Haipendezi hata kidogo kuona mchakato wa katiba ukiharibika baada ya taifa kutumia muda mwingi kuandaa rasimu na pia kupoteza mabilioni ya fedha kugharimia mchakato huo.

Tunawakumbusha wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwa ni vyema kwa kila mmoja kuwa na lengo la kuona kuwa katiba mpya yenye kukidhi matakwa ya Watanzania inapatikana. Na hii ni fursa ya kihistoria inayopaswa kutumiwa vyema kwa manufaa ya taifa.

Shime, Bunge Maalum la Katiba lilete katiba bora. Siyo kuwagwa Watanzania.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment