WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 14, 2014

Samuel Sitta: Kura ya siri


Mwenyekiti mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akizungumza na mwandishi wa Mwananchi, Fidelis Butahe nyumbani kwake mjini Dodoma juzi.
Dodoma. Mwenyekiti Mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano wa kutumia kura ya siri katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya Katiba.
Sitta aliyechaguliwa juzi kushika wadhifa huo, alisema atashirikiana na kamati ya uongozi itakayoundwa ya wenyeviti wa Kamati 15 za Bunge hilo na kamati ya ushauriano kupata jawabu la suala hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani kwake mjini Dodoma juzi, Sitta alisema: “Unajua kuna baadhi ya vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba ni vizuri vipigiwe kura ya wazi na vingine ambavyo ni nyeti zaidi vipigiwe kura ya siri.”
Alisema si vizuri vifungu vyote vipigiwe kura sawa, yaani si lazima zote ziwe za siri au ziwe za wazi.
Alitoa mfano wa ibara inayosema kutakuwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na kusema: “Hatuwezi kushindana katika suala la kuwapo kwa Mahakama na ni wazi kuwa jambo hilo mnaweza kupiga kura ya wazi. Nasema hivyo kwa sababu Katiba yoyote lazima ionyeshe mihimili yote ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.”
Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alishinda kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika juzi kwa kura 487 kati ya 563 (sawa na asilimia 85).
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki ambaye kaulimbiu yake ni ‘kasi na viwango’, alisema vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba vinavyoweka misingi ya Katiba, ni vizuri vikapigiwa kura ya siri.
“Unajua tuna viongozi wa dini na halitakuwa jambo la busara kama tukizijua hisia zao. Kama wewe uko karibu na imamu au askofu halafu anapiga kura ya wazi ya kutaka Serikali tatu wakati wewe muumini unataka Serikali mbili ni wazi kuwa jambo hilo linaweza kuleta hisia tofauti na kuwanyima watu haki na uhuru wa kuamua,” alisema Sitta.
Alitoa mfano wa Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba inayozungumzia Serikali na muundo wa madaraka katika Jamhuri ya Muungano na kufafanua kuwa katika sura hiyo atapendekeza ipigiwe kura ya siri.
Kuhusu suala hilo la muundo wa Serikali alisema: “Kikubwa ni wajumbe kujenga hoja, hatuwezi kwenda na misimamo isiyobadilika kwa sababu tunataka maridhiano. Nitatenda haki na nitatoa muda mrefu zaidi kwa wajumbe kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo zina uzito mkubwa kuliko sura nyingine ambazo ni za maelezo tu. Mfano suala la haki za binadamu ambazo wote tunakubaliana nazo.”
Alisema wakati wa kujadili muundo wa Serikali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifika, ataishauri kamati ya uongozi, kutenga muda wa ziada katika suala hilo na mengine yenye utata.
Mwenyekiti huyo alisema suala la upigaji kura linatakiwa kuamuliwa kwa busara na atatumia hekima zake na za wajumbe wa Bunge hilo, kutatua mgogoro wa kura ya siri au ya wazi
Wakati wa kujadili rasimu ya kanuni za Bunge hilo, kulizuka mvutano mkali katika vifungu vya 37 na 38 vinavyozungumzia aina ya kura itakayopigwa wakati wa kufanya uamuzi na kulazimika kuviweka kando. CCM kimekuwa kikinadi kura ya wazi kikisema ni ya haki huku wapinzani wakitaka kura ya siri.
Hata hivyo, kamati ya muda iliyoandaa kanuni za Bunge hilo, ilipendekeza kuwa Bunge Maalumu ndilo litakaloamua aina ya kura itakayopigwa.
Akizungumzia suala hilo Sitta alisema: “Pamoja na kuwapo kwa hali hiyo, lazima ifikie wakati tuamue. Hatuwezi kuwa na kanuni ambazo hazielekezi namna ya kupiga kura kwa sababu upigaji wa kura unaweza kuanza kufanyika wiki ya kwanza tu baada ya kuanza kujadili Rasimu ya Katiba.”
Samia Makamu Mwenyekiti
Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan jana alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo baada ya kumshinda mpinzani wake, Amina Abdallah Amour.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk Thomas Kashililah alisema kati ya kura 523 zilizopigwa, Suluhu alipata kura 390 sawa na asilimia 74.6, Amina kura 126 sawa na asilimia 24.1. Kura saba ziliharibika.
Kukamilika kwa uchaguzi huo kunafungua milango kwa Yahya Hamad Hamis kuapishwa kuwa Katibu wa Bunge la Katika na Dk Thomas Kashililah kuwa Naibu Katibu kwa mujibu wa sheria.
Makatibu hao wataapishwa leo saa nne asubuhi na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ndogo ya Dodoma. Baada ya kuapishwa, Katibu atawaapisha Sitta na Samia katika Ukumbi wa Bunge kuanzia saa 10 jioni leo.
Awali wakati wakijieleza Amina alizua gumzo baada ya kueleza kuwa licha ya kuwa na watoto watano, ameachika na kwa sasa hana mume.
“Mimi ni mama wa watoto watano, nina shahada ya uzamili ya masuala ya fedha, nina stashahada ya sheria na nimefanya kazi katika Benki ya Biashara kwa miaka 23 ila kwa bahati mbaya nimeachika,” alisema na kusababisha wajumbe kuangua kicheko.
Baada ya kuchaguliwa, Suluhu alisema: “Nitafanya naye (Sitta) kazi kwa ushirikiano na uadilifu mkubwa. Pia ninawaahidi wajumbe wote kuwa nitawapa ushirikiano.”
Mbowe amuonya Sitta
Wakati huohuo; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtumia salamu za pongezi Sitta huku akimtaka kuachana na masilahi ya chama chake.
“Ningependa kutuma salamu kwa Samuel Sitta ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, nataka aelewe kuwa alichokabidhiwa ni majukumu si cheo,” alisema na kuongeza:
“Mamilioni ya Watanzania watakuwa wanamfuatilia na kumtazama kwa makini mno... maana wananchi kwa sasa wanajua mchakato wa Katiba Mpya umebeba matumaini ya Taifa lao kwa miaka 50 hadi 100 ijayo

SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment