WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 7, 2014

Kufanya vurugu bungeni ni fedheha

Katuni
Jana mkutano wa Bunge Maalum la Katiba ambao unakwenda kwa sura ya semina katika kupitisha kanuni za bunge hilo uliahirishwa kabla ya muda uliopangwa kutokana na kuibuka kwa mtafaruku miongoni mwa wajumbe.
Mkutano huo uliahirishwa majira ya saa 6:15 mchana baada ya kuibuka zomeazomea na hata kufikia hatua ya baadhi ya wajumbe kutaka kukunjana masharti.
Hali hii haikubaliki na fedheha kubwa kwa bunge hili ambalo linatazamwa kwa macho makali na Watanzania wote kwa matumaini ya kupata katiba mpya.
Siyo nia ya tahariri hii kusema nani alikuwa chanzo cha vurugu hizi miongoni mwa wote waliosabaisha kuahirishwa kwa shughuli za kupitia kanuni kabla ya wakati wake, ila itose tu kusema kuwa kitendo cha mbunge yeyote kukosa uvumilivu na ukomavu wa kisiasa, ni kielelezo cha hali ya juu cha kutokujitambua na hivyo kujitumbukiza katika ulimbukeni wa vurugu.

Vurugu kamwe hazitatupa kanuni bora za kuendesha Bunge la Maalum la Katiba na wala hazitasaidia Watanzania kwa ujumla na umoja wao kupata katiba mpya.
Tunawaasa wabunge kuwa wavumlivu, na kutambua kuwa demokrasia ni pamoja na kujifunza kusikia ambayo hayapendezi masikioni mwako. Wabunge wajifunze kuwa wavumilivu.
 Nguvu itumike kuwahamisha wanaong’ang’ania mabondeni

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa hadhari kwamba ukanda wa pwani unaojumuisha mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba utapata mvua kubwa kwa kipindi cha siku mbili kuanzia juzi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mvua hizo zinatarajiwa kufikia milimita 50 katika kipindi cha saa 24 kiasi ambacho kinaweza kusababisha mafuriko.
Ni kwa kutambua ukubwa wa mvua hizo ndiyo maana TMA imewataka wakazi wote wa ukanda wa pwani kuwa na hadhari kubwa wakati wanakwenda maeneo ya baharini na hata wanaoishi maeneo ya mabondeni.
Hadhari hiyo pia imelenga vyombo vya umma vya kukabiliana na majanga kwa maana ya kujipanga kukabiliana na janga lolote litakalotokana na mvua hizo, hii itasaidia ama kupunguza madhara kwa waathirika au hata kuepusha kabisa kama watu wataitikia wito wa kuondoka katika maeneo hatarishi kama mabondeni kwa wakati.

Wakati TMA ikitoa hadhari hiyo juzi wakazi zaidi ya 200 wa jiji la Dar es Salaam mtaa wa Karakata, Ilala, nyumba zao ziliezuliwa mapaa na upepo mkali, sasa hawana makazi. Upepo huo unaelezwa kufuatana na mvua kubwa ambayo ilinyesha maeneo hayo na kusababisha mafuriko.

Miongoni mwa viongozi wa serikali waliofika eneo hilo kujionea madhara yaliyowakumbwa wananchi hao ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambaye pia ni kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Jordan Rugimbana, alisema wazi kuwa kulingana na  mvua zinazoendea kunyesha jijini Dar es Salaam na kama TMA ilivyobashiri ni dhahiri mafuriko yatatokea maeneo ya mabondeni. Kwa maana hiyo aliwataka wahame.

DC Rigumbana aliwaambia wakazi wa mabondeni kwamba safari hii serikali haitahusika na janga litakalowakuta kwa kutamka kuwa hakuna Mabwepande ya pili kwa maana ya kuwahamisha wakazi hao ambao wameendelea kukaidi amri ya serikali ya kuwataka wahame sehemu hizo hatarishi zisizofaa kwa makazi ya binadamu.

Siku moja baadaye yaani jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa wito kwa wakazi wa mabondeni kuhama kwa hiari yao kwa kuwa serikali haitahusika na madhara yatakayowakuta kutokana na mafuriko.

Tunaungana na viongozi wote waliozungumzia suala la wakazi wa mabondeni. Kwa hakika ni lazima watu hawa wahame kwenye maeneo hayo hatarishi.
Ni jambo lisilovumilika kwamba miaka na miaka watu hawa wameachwa kukaa katika maeneo hayo na mara nyingi kuisababishia serikali hasara kwa gharama za kuwaokoa kila wanapokumbwa na mafuriko.
Mwaka juzi serikali iliamua kukata mzizi wa fitina baada ya kutokea mafuriko makubwa ambayo yalisababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali kwa wakazi wa mabondeni.
Wakazi hao walipewa viwanja bure na serikali maeneo ya Mabwepande na wengine vifaa vya ujenzi; serikali ilipeleka huduma muhimu za kijamii huko kama barabara, maji na hata umeme.
Pamoja na juhudi hizi za serikali na ikizingatiwa kuwa gharama hizo zinabebwa na kodi za wananchi, watu hao walirejea tena mabondeni.
Tunaungana na viongozi hawa kuwataka wakazi hao kuhama mabondeni siyo kwa sasa kwa sababu ya hatari ya mafuriko tu, bali moja kwa moja.
Tunaiasa serikali kuwa kuendelea kubembelezana na watu wanaoishi mabondeni ndiko kunawapa kiburi cha kuendelea kung’ang’ania maeneo hayo hatarishi kwa maisha yao.
Kitendo chochote cha mtu kuhatarisha uhai wa mtu mwingine au wa kwake mwenyewe ni uhalifu, ni jinai, kwa maana hiyo hatuoni kwa nini serikali inashindwa kupambana na watu wanaong’ang’ania mabondeni kwa mkono wa chuma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment