WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, March 31, 2014

Sitta ampa barua Mtikila aende kwa JK


Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,Samuel Sitta.PICHA|MAKTABA 

Dodoma. Ombi la Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Christopher la kutaka Bunge hilo livunjwe, limekuwa zito kwa Mwenyekiti Samuel Sitta.
Kutokana na ugumu huo, Sitta amelazimika kumpatia barua Mtikila ili awasilishe hoja yake kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye kisheria ana mamlaka hayo ya kuvunja Bunge la Katiba, ambalo limekuwa likionekana kwenda mrama.
Mtikila, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia na mjumbe wa Bunge la Katiba aliwasilisha barua yenye hoja binafsi akitaka bunge hilo livunjwe na wajumbe warejee makwao kwa madai kuwa chombo hicho cha kutunga Katiba mpya hakijali maslahi ya umma na uongozi umekuwa haumtendei haki.
Majibu ya barua hiyo yalikuwa hivi: “Nimeagizwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu nikujulishe kwamba Bunge Maalumu halina uwezo wala mamlaka ya kujitangaza kwamba ni haramu na hivyo livunjwe ; na kwamba hoja hiyo haistahili kuwa hoja ya Bunge Maalumu,” inasomeka barua hiyo iliyoandikwa na katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad.
Akizungumza na Mwananchi jana, Sitta alikiri kumpatia barua hiyo Mtikila ili aende kwa Rais Kikwete kwa sababu hoja yake kutaka kuvunjwa Bunge haiwezi kusikilizwa na chombo hicho kwa kuwa mwenye madaraka ya kuvunja Bunge ni Rais pekee.
“Ni kweli ametuletea hoja ya kuvunja Bunge. Ameandika mambo mengi, akitumia lugha ya uchochezi, kama kudai kwamba ‘Tanganyika imekuwa koloni la Zanzibar kwa muda mrefu’, lugha ya namna hii hatuwezi kuikubali,” alisema Sitta.
Sitta alisema siyo kila kitu ambacho mjumbe anasema, ni lazima kifuatwe katika mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya.
“Mtu akija anasema anataka Bunge livunjwe amfuate aliyetuteua, siyo sisi wenyewe kujivunja,” alisema Sitta.
Alisema hoja ya Mtikila, ambaye alitishia kufungua kesi ya kuzuia Bunge la Katiba kufanya kazi, ya kutaka Bunge kuvunjwa imekwenda kinyume kabisa na taratibu za Bunge.
“Hoja hii imekwenda nyuzi 180 kwa sababu aliyetuteua alitaka sisi tutunge katiba kutokana na rasimu, ili sisi tupeleke kwa wananchi rasimu iliyopendekezwa,” alisema.
Mchungaji Mtikila alikiri kupokea barua kutoka Ofisi ya Bunge ikimweleza jambo moja; apeleke hoja yake kwa Rais Kikwete aliyeteua Bunge la Katiba.
Hata hivyo, alisema hakusudii kwenda kumuona Rais Kikwete baada ya kushauriwa kupitia barua ya Bunge kutokana na kutoa hoja ya kutaka kuvunjwa kwa bunge hilo.

“Sitakwenda kumuona Kikwete, bali ninajua kwamba tukishindwa kuipata Tanganyika kwenye Bunge hili nitakwenda mahakama za kimataifa,” alisema Mtikila ambaye amekuwa akihubiri Utanganyika tangu nchi ilipoingia kwenye siasa za vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya tisini.
Alisema kwa sasa anasubiri kumaliza majadiliano juu ya sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba kuona mwelekeo na suala la muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu litakwamishwa, ataondoka Dodoma na kurejea Dar es Salaam kuandaa kesi.
Hoja kubwa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya iko kwenye muundo wa Muungano baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha rasimu inayoonyesha kuwa wengine wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo linaonekana kupingwa na wajumbe kutoka chama tawala cha CCM.
Bunge hilo linaundwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wawakilishi wa Baraza la wawakilishi wa Zanzibar na wawakilishi wa makundi mbalimbali wapatao 201 ambao walitangazwa na Rais Kikwete.
Lakini Mchungaji Mtikila anapingana na muundo wa Bunge la Katiba.
“Nitakwenda mahakamani kupinga sheria yote ya Mabadiliko ya Katiba kwani waliopaswa kushiriki Bunge la Katiba ni wajumbe waliochaguliwa na wananchi kwa ajili ya Bunge la Katiba, na siyo hawa wabunge na wengine wa kuteuliwa,” alisema.
Hoja ya Mtikila
Pamoja na mambo mengine katika hoja yake, Mtikila analalamika kuwa amezuiwa kuchangia katika Bunge hilo baada ya kuandikiwa barua na Ofisi ya Bunge.
Hata hivyo, katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Khamis Hamad alisema: “Hili kwangu ni jipya na sidhani kuwa linawezekana.”
Mtikila alisisitiza kuwa alipewa barua hiyo Jumatano iliyopita ikiwa ni majibu ya barua yake aliyoiandika kwa ofisi hiyo wiki iliyopita.
“Nilianza kuhisi baada ya kuona ninanyimwa kuchangia; nikaandika barua kuomba maelezo kwa nini ninakosa nafasi ya kuchangia bungeni,” alisema na kuongeza:
“Lakini juzi nilipokea barua kutoka kwa katibu wa Bunge ikinikataza kuchangia tena bungeni kutokana na kauli zangu za kukosoa mchakato.”

Alisema kuwa alipomuuliza katibu sababu za uamuzi za kukatazwa kuchangia, alijibiwa kuwa ni maagizo kutoka kwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta.
“Hii imeniathiri sana mimi. Bunge hili limepotoka kwa kuwa wanachoangalia ni maslahi yao na si ya nchi,” alisema.
Alisema mchakato wote umekosewa kwa kuwaweka wabunge na wawakilishi kuwa sehemu ya Bunge badala ya wananchi kuchagua wajumbe wa Bunge.
“Hakuna nchi yoyote ambayo imefanya hivyo. Wanaharibu mabilioni ya fedha ambayo hayataleta Katiba yenye uhalali wowote,” alisema.
Alisema endapo Sitta atashindwa kutatua jambo hilo, anakusudia kuunganisha katika ushahidi wake kwenye kesi inayopinga mchakato wa Katiba.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment