WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 12, 2014

Kanuni hizi zisaidie kumaliza malumbano Bunge la Katiba

Katuni
Hatimaye Bunge Maalum la Katiba limepitisha kanuni zitakazotumika kuwaongoza wajumbe katika mijadala yao mbalimbali. Vifungu 87 vya kanuni hizo viliridhiwa kwa pamoja jana asubuhi, huku kukiwa na makubaliano ya kuwa na nafasi ya kuviboresha zaidi vifungu vya 37 na 38 vinavyozungumzia upigaji kura wakati wa kupitisha rasimu ya katiba hiyo mpya.
Kabla ya kupitishwa kwa kanuni hizo, tayari Bunge hilo lilishatumia takriban siku 21 bila ya kuanza rasmi kwa shughuli kuu ya kujadili rasimu ya katiba mpya na kuipitisha. Muda huo, ambao kwa kiasi kikubwa ulitumika kujadili vifungu vya kanuni kabla ya kuvipitisha jana, ni sawa na asilimia 26 ya siku 70 za uhai wa Bunge hilo. Idadi hiyo haihusishi siku nyingine 20 zinazoweza kuongezwa ikiwa siku zilizokadiriwa awali hazitatosha.

Sisi tunawapongeza wajumbe wote wa Bunge hili. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kama busara isingetumika na wajumbe hao wakaendelea kulumbana kutokana na mgongano kuhusu upitishwaji wa rasimu kuwa wa siri au wazi, ni dhahiri kuwa siku nyingine zaidi zingepotea.

Hivyo, kitendo cha kupitisha vifungu vingine na kuahirisha walau kwa muda malumbano kuhusu namna ya kupigia kura rasimu ni cha kuungwa mkono kwani sasa kinatoa fursa ya kuendelea kwa shughuli nyingine za Bunge hilo.

Kwa mfano, NIPASHE tunaona kuwa fedha za walipa kodi zingeendelea kupotea zaidi kupitia posho za vikao zinazolipwa kwa wajumbe kila uchao ikiwa wasingefikia muafaka kuhusiana na kanuni za kuwaongoza.
Na tayari baadhi ya wananchi walishaanza kuingiwa hofu juu ya mwenendo wa bunge hilo, wakihisi kwamba pengine, malumbano ya muda mrefu miongoni mwa wajumbe ni njia mojawapo ya baadhi yao kutaka kuongeza siku za kukaa kwao Dodoma ili waendelee kuvuna malipo yatokanayo na posho.
Hisia hizi zilianza pia kuwagusa wajumbe wenyewe na baadhi yao walikuwa jasiri kiasi cha kutaka bunge hilo lisitishwe kwa muda na kutoa fursa zaidi ya majadiliano kwa pande zinazovutana ili kutafuta suluhu nje ya Bunge na ndipo wakutane tena; lengo likiwa ni kuokoa mamilioni ya pesa za walipa kodi yanayopotea kupitia malipo ya posho.

Kuna wananchi pia walioanza kuingiwa hofu kuwa pengine, malumbano ya wajumbe kuhusu kanuni yangesababisha Bunge hilo kuvunjika kabla hata ya kuanza kwa kazi yenyewe ya kujadili rasimu na kuipitisha. Ni wazi kwamba hali hiyo ingewasononesha Watanzania ambao wengi wao wamekuwa na shauku ya kuona kuwa taifa linapata katiba mpya.

Jambo muhimu kwa wajumbe wote ni kutambua kuwa hadi kufikia jana, tayari wameshatumia muda mwingi kwa sababu tu ya kupitisha kanuni za kuwaongoza.
Kwa sababu hiyo, tunaamini kuwa kuanzia sasa, wataendelea kutekeleza majukumu yaliyowapeleka Dodoma kwa kasi mpya ili mwishowe wafanikishe kazi waliyotumwa kwa asilimia 100 na kutimiza ndoto za Watanzania.
NIPASHE tunaamini kuwa mabishano yatokanayo na hisia za kutetea misimamo ya vyama au makundi yoyote yale katika bunge hilo hayatapewa nafasi kubwa kulinganisha na taifa. Wajumbe wajadili hoja zao huku wakiwa na fikra za kuwa na taifa imara, lenye watu walioshikamana zaidi na kuwa kitu kimoja kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Baada ya kanuni kupitishwa na wajumbe wengi jana, ni matarajio yetu kuona kuwa sasa wabunge watazingatia kila walichokubaliana na kutumia muda mwingi katika kujadili rasimu kabla ya kuipitisha na wala siyo kuwa na migongano isiyokuwa na tija kwa taifa.
Haipendezi kwa mfano kuona kuwa bado kuna mwendelezo wa vitendo vya baadhi ya wabunge kuvunjiana heshima kwa kupeana maneno ya vijembe, kejeli na kashfa kwani mambo yote hayo hayana faida kwa mustakabali wa taifa la Tanzania.
Ni imani yetu kuwa baada ya kanuni kupitishwa, wajumbe wote watakuwa tayari kuziheshimu na mwenyekiti watakayemchagua atakuwa makini katika kuzisimamia.
Kwa kufanya hivyo, wote watatoa fursa nzuri ya kuwapo kwa majadiliano yenye tija na mwishowe taifa kupata katiba nzuri kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment