WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 12, 2014

Kura ya siri ngoma nzito

  Wabunge bado wakwama kupata suluhu
  Sasa kusubiri majaliwa ya Kamati ya Kanuni

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kabla ya kuanza kwa kikao jana asubuhi. Kutoka kushoto ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Kingunge Ngombale-Mwiru, James Mapalala, James Mbatia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka. Picha/Selemani Mpochi
Wasiwasi wa kufikiwa mwafaka baina ya pande mbili zinazovutana kuhusu utaratibu utakaotumiwa kupata uamuzi kwa kupiga kura ama ya wazi au ya siri, umezidi kuligubika Bunge Maalumu la Katiba, baada ya wajumbe wake kutaka livunjwe ili kuepuka kupoteza muda na kulaumiwa na wananchi kwamba, wanakula posho bila kufanya kazi.
Ushauri huo ulitolewa na baadhi ya wajumbe wakipinga uamuzi wa Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho, wa kutaka Bunge lipitishe azimio la kuridhia kupitishwa kwa baadhi ya vifungu vya Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, huku vingine vikiwa havijapatiwa mwafaka.

Vifungu, ambavyo Kificho aliamua jana Bunge lipitishe azimio la kuviridhia ni 85, huku pande mbili zinazovutana kuhusu vifungu viwili vinavyohusu utaratibu wa kupata uamuzi wa kupiga kura, wakiendelea kuvitafutia mwafaka kupitia kamati ya mashauriano.

Ushauri wa kuvunjwa kwa Bunge hilo, lilitolewa bungeni jana na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.

 Kafulila alisema kwa namna Bunge hilo linavyokwenda, hakuna kinachoendelea kutokana na pande mbili za wajumbe kuvutana.

 Alisema mvutano huo unasababisha masuala ya kanuni kukwama kwa sababu yana athari kwenye maamuzi ya baadaye.

“Kwa hiyo, ushauri wangu…lazima tukubaliane kwamba kama tukikutana jioni na bado tunaletewa taarifa za aina hii nusu nusu, ambazo hazina makubaliano, hazina mwafaka kuhusu jambo hili la kanuni, tukubaliane kwamba, Bunge hili, semina hii tukubaliane i-brake kwa kipindi, ambacho watu watarudi majumbani kwao ili kusudi wakafanye consultation (ushauri) huko nje, tukakubaliane huko nje,” alisema Kafulila. 

Alisema msingi wa hoja yake ni kwamba, wanaendelea kuvuta muda bungeni bila kukubaliana, huku wakiendelea kula posho.

“Huko nje wanatuona tunakula posho ya bure bila kazi kwa sababu maamuzi hayafanyiki,” alisema Kafulila

Aliongeza: “Kwa hiyo, kama tunakubaliana … naomba nipendekeze hoja kwamba tukikutana jioni kama hakuna mwafaka, Bunge hili liazimie kuvunjwa, tukajadiliane huko nje, ambako tutakuwa hatuchukui posho mpaka hapo mwafaka utakapopatikana.”

KIFICHO

Hata hivyo, ushauri wa Kafulila ulipingwa na Kificho, ambaye alisema kuanzishwa kwa Bunge hilo kulitokana na tangazo la Rais, hivyo kama ni kuvunjwa basi pia kutafanywa naye na si mtu mwingine yeyote.

OLUOCH

Mjumbe wa Bunge hilo kutoka vyama vya wafanyakazi, Ezekiah Oluoch, alisema Mwenyezi Mungu ameagiza katika vitabu vyake vitakatifu akisisitiza Biblia, kuwa panapokuwa na shida, kura ifanye kazi, hivyo alishauri wapige kura kwanza ya kuamua aina ya kura watakayoamua.

 “Asubuhi hii, wala hatuhitaji ku-brake. Wala hatuhitaji mashauriano kwa sababu watu wa kushauriana wameshashindwa kushauriana,” alisema Oluoch.

Aliongeza: “Sasa kama watu wa kushauriana wameshashindwa kushauriana, wamekaa tangu juzi, wanashauriana, sasa kilichopo Mheshimiwa Mwenyekiti mimi ninaomba sasa hivi sekretarieti watuandalie karatasi, na kwamba sisi tulikuchagua hapa kwa kutumia kura ya siri, tupige kura ya siri inayoamua juu ya aina ya kura tunayotaka.”

Alisema ikiwa wakipelekewa rasimu ya kanuni, ambayo haina vifungu vya 37 na 38, Kificho atakuwa hajawatendea haki kupitisha vitu nusu.

Vifungu hivyo vinazungumzia jinsi ya kufikia maamuzi katika Bunge Maalum la Katiba. Ingawa inatajwa kuwa ni kwa kupiga kura, havifafanui ni upigaji kura wa namba gani kati ya wazi na siri ambazo zimekuwa mwiba kwenye Bunge hilo.

 Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni, Profesa Costa Mahalu, alisema kanuni ya 37 na 38, ambazo zinaeleza utaratibu wa kufanya maamuzi, baada ya marekebisho sasa zitaeleza kuwa utaratibu wa uamuzi utakuwa ni wa kura.

Alisema kamati imeona ni vizuri ikaweka fasili nyingine kwenye kanuni ya 38, ambayo sasa itaeleza wazi aina ya kura itakayotumika na kwamba, hilo litakuwa kama itakavyoamualiwa na Bunge hilo.

Akizungumzia hilo, Kificho alisema kamati ya mashauriano pamoja na kila upande bado wanaendelea na mashauriano kuhusiana na jambo hilo na kwamba, ndivyo  walivyokubaliana.
 
DIANA CHILOLO

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), ambaye ni Mjumbe wa Bunge hilo, Diana Chilolo, alisema haelewi kinapotoka kigugumizi cha kukubali utaratibu wa kura ya wazi kwa kuwa kila mjumbe ametumwa na wananchi kwenda katika Bunge hilo kusikika.

“Tunavyotaka kusema vitu kisirisiri tunataka iwe nini. Wananchi wanasubiri kusikia tunasema nini. Tuna kipi tunaficha. Mimi naomba kwa kuwa hii kamati imekwama, tuendelee na mambo mengine,” alisema Chilolo.

Kauli ya Chilolo iliwafanya wajumbe kuanza kuzomea na yeye kusema: “Habari ya kuzomea ni tabia mbaya hata Mwenyezi Mungu haimfurahishi.” lakini wajumbe waliendelea kuzomea, hali iliyomfanya Kificho kuingilia kati na kuwataka wampe nafasi na haki ya kuzungumza na kumsikiliza.”

Chilolo aliendelea kusema kuwa iwapo zitapigwa kura kwa sasa, haitaondoa mvutano uliopo baina ya pande mbili hizo.

“Tatizo liko palepale tutapiga kura za aina gani. Kura ya siri ama kura ya wazi?” alihoji Chilolo na kujibiwa na wajumbe, ambao baadhi walisema kwa kupaza sauti: “Ya wazi” na wengine “Ya siri.”

Zogo la watu kuzomea na kuzungumza bila utaratibu, liliongezeka baada ya Kificho kumruhusu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuzungumza.

Zomea hiyo iliongezeka mara dufu baada ya Lukuvi kutamka kwamba, vifungu 85 vimeshapitishwa na wajumbe katika rasimu ya kanuni, vimebaki viwili, ambavyo ni cha 37 na 38 na kusema kwa uwiano wowote haiwezekani kusema kwamba, kanuni imeshindwa.

Hali hiyo ilimfanya Lukuvi kusema: “Inawezekana tulikutana kabla kwamba, tufanye mkakati wa kuzomea na nini, lakini mimi ni sugu wa kuzomewa. Nimeshazoea. Sasa kama mnafikiri wengine wasisikilizwe, ila watu fulani tu ndiyo wasikilizwe, endeleeni kuzomea, lakini mimi nitasema tu.”

Alisema semina ya wajumbe wa Bunge hilo siyo ya mwisho wa kupitisha kanuni, kwani kwenye rasimu ya kanuni kuna kamati pia ya kudumu ya kanuni.

Lukuvi alisema baada ya kanuni kupitishwa, utaratibu uliowekwa kwenye kanuni hiyo, umempa nafasi mbunge yeyote kupeleka marekebisho ya kifungu chochote cha kanuni wakati wowote.

“Hatuwezi kujihakikishia kwamba hata hivyo vifungu 85 tukivipitisha leo (jana) hatutakuwa na mawazo mbadala kwa kipindi chote cha miezi miwili. Haiwezekani, haiwezi kuwa,” alisema Lukuvi.  Alisema wao wameishi kwa kutumia kanuni hizo kwa zaidi ya miaka 15, ambazo leo wanaweza kupitisha, lakini kesho yanatokea mahitaji mengine zinapitishwa.

Lukuvi alisema ndiyo maana wajumbe wa Bunge hilo wamekubali kuweka kamati ya kudumu ya kanuni, ambayo itakuwa inazingatia mwenendo wa mijadala na Bunge hilo na mahitaji yake.

“Hivyo ninaposikia kwamba lazima kila kitu kiishe leo, basi futeni na ile kamati ya kanuni. Ina kazi gani? Kwa nini kila kitu kiishe leo? Mnataka kuniambia yaliyoandikwa leo yatawaongozeni kwa miezi yote mitatu bila mabadiliko. Haiwezekani.” alihoji Lukuvi.

Hata hivyo, alisema ili kamati ya kanuni ipate mamlaka ya kufanya marekebisho yoyote, lazima rasimu hiyo ipite ili kamati hiyo iundwe kwa ajili ya kushughulikia masuala hayo siku hadi siku.

Alisema anaunga mkono kamati ya kumshauri mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo na kuwaomba wajumbe kupitisha vifungu 85 vya rasimu ya kanuni hizo akisema matumizi ya vifungu vya 37 na 38 siyo ya leo wala ya kesho. Kauli hiyo iliwafanya wajumbe waendelee kuzomea. 

SIMBACHAWENE Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, George Simbachawene, alisema si kweli kanuni hizo zinapitishwa bila vifungu vya 37 na 38, bali wanapitisha kanuni kama ilivyo. Alisema utaratibu wa kura ya siri au ya wazi siyo suala na kwamba, suala ni kupiga kura na kwamba, kamati ya kanuni inaendelea vizuri na inafanya kazi kwa matakwa ya wajumbe wa Bunge hilo.  
Kificho aliahirisha kikao hicho na kusema kuwa wangekutana kama Bunge, saa 10:00 jioni kupitisha kanuni, lakini ulipofika muda huo aliahirisha tena hadi saa 12:00 baada ya wajumbe wengi kusema hawajapata nakala za kanuni ambazo zimefanyiwa masahihisho kabla ya kutolewa azimio la kuzipitisha.    

MBOWE ATOBOA SIRI 
Wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, wamekilalamikia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuingilia maamuzi ya kamati hiyo na kufanya kikao cha Bunge Maalum kushindwa kusonga mbele kwa maridhiano.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, mjumbe wa Kamati hiyo, Freeman Mbowe, alisema  Kamati imeshindwa kuafikiana kutokana na kukosekana kwa uwezo wa kufanya maamuzi ni udhaifu mkubwa. 
“Tulizungumza na kukubalina, mara ya mwisho tumekutana Jumamosi wenzetu (CCM) wakasema tusubiri wakawasiliane na chama chao, jana (juzi) wakasema wanakutana na Mwenyekiti wao (Jakaya Kikwete) washauriane na kutoa nafasi yao (maamuzi) katika jambo hilo, hadi sasa hatujafanya kikao kingine cha maridhiano,” alisema. 

Mbowe alisema wameshangazwa na maamuzi ndani ya Bunge hilo na kwamba ni kamati gani ambayo haipeani mrejesho wa waliyoyazungumza kwa upande wa CCM. 

“Kikao kinavyoendesha bila maamuzi maalum au kikifanya maamuzi fulani wakienda kwenye vikao vyao vya chama maamuzi yanabadilishwa, hata ile busara tuliyokubaliana wakija inapindishwa ikionekana inakuwa mbaya hawatuiti kwenye vikao hadi tunakutana na mazingira tunayokutana nayo leo, tunakuwa tunaviziana na haitatujenga kama taifa,” alisema.  Alisema kinachotakiwa ni maridhiano na si CCM kutumia nguvu na idadi kubwa ya wajumbe iliyonao ndani ya Bunge hilo. 

“Tukienda hivi katika Bunge hili kwa kujaribu kulazimisha bila maridhiano siamini pendekezo la tupige kura tuamue ya wazi au ya siri, maridhiano yanahitaji busara ya kujua nini kitakuwa faida kwa mwingine,” alisema.  Alisema ni vyema CCM ikaliacha Bunge liwe la kushauriana na kujenga hoja na kushawishiana ili watu wapige kura kwa dhamira zao na si shinikizo. 

“Kama tuna Bunge ambalo haliwezi kufanya maamuzi kwa sababu ya msukumo wa makundi na vyama ambavyo viko nje ya Bunge kinyume na kifungu cha nne cha Kanuni, hakuna maana ya kukaa humu kwa kuwa tutakaa halafu maagizo yanatoka kwenye vikao vinavyofanyika nje,” alisema Mbowe. 

Alisema juzi kilifanyika kikao cha Kamati Kuu ya CCM jambo hilo (kura ya siri au wazi) limejadiliwa na Mwenyekiti wa CCM alikutana na Kamati ya uongozi ya wabunge wa CCM.
“Wasitulazimishe maelekezo ya chama kulazimisha kuwa maelekezo ya Bunge la Katiba,” alisema Mbowe. 
Alisema mchakato wa Katiba ni tendo la maridhiano ya kuweka mustakabali wa nchi mbele na haki ya mtu kupiga kura. 

“Tunaona wabunge wa CCM wanavyopewa maelekezo na chama chao, tunavunja kanuni ambazo tumejadili na kukubaliana tuongozwe na dhamira na hoja na si matakwa ya vyama,” alisema. LIPUMBA, MBOWE, VUAI, MBATIA Jana jioni Bunge liliporejea ilishindikana kupitisha kanuni kufuatia hoja ya Profesa Ibrahim Lipumba (CUF)  kuwa muda wa kusoma usingetosha na kushauri bunge liahirishwe hadi kesho ili wabunge wapate fursa ya kusoma neno licha ya ukweli kuwa wanaiamini sana kamati ya kanuni chini ya Profesa Mahalu.

Hoja ya Lipumba ilingwa mkono kwa msisitizo na Mbowe (Chadema), Vuai Ali Vuai(CCM) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), waliosisitiza kuwa maridhiano na kuelewana ni jambo la umuhimu mkubwa kabla ya kupitishwa kwa kanuni hizo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment