WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, March 8, 2014

Katika hili CCM, CHADEMA wanalidhalilisha Taifa




Kumbukumbu za majadiliano ya Bunge (Hansard), za Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 25-28, 1977, Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Moringe Sokoine, ameelezea vizuri dhana na mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba.

Kwa kuwa taifa letu kwa mara nyingine liko kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya, na kwa kuwa Bunge Maalum tayari limeanza vikao vyake vya kutunga Katiba Mpya hiyo mjini Dodoma, ni muhimu tukumbushane kile alichokisema Sokoine wakati ule wa mchakato wa kutunga Katiba hii ya sasa ya mwaka 1977.

Sokoine anasema: “Katiba ya nchi ndiyo Sheria ya msingi kabisa kwa taifa lolote, na chombo kinachotunga Sheria hiyo, ni lazima kiwe chombo chenye madaraka makubwa kabisa. Kwa hiyo, Bunge hili Maalum lina madaraka kuliko Bunge la kawaida. Bunge hili linaweza kukataa au kukubali mapendekezo haya.

“Lakini Ndugu Spika, katika kutumia madaraka yetu, ni lazima tujue mipaka ya madaraka hayo. Mapendekezo tutakayofikiria hivi sasa yametokana na maagizo ya Chama. Kwa busara yetu, tumeamua, na bila kusita, kwamba Chama kitashika hatamu za uongozi wa nchi. Kwa hiyo, Bunge hili linaweza kabisa kuyakataa ama kuyabadilisha mapendekezo ya Serikali iwapo litaona kuwa yanapinga maagizo ya Chama. Na iwapo mapendekezo yote yanayopendekezwa yanatekeleza maagizo ya Chama, naomba Bunge lisione uzito wa kuyapokea na kuyapitisha bila kusita (Makofi).”

Kwetu sisi katika maneno haya ya Sokoine tunaziona hoja kuu mbili. Kwanza ni madaraka ya Bunge Maalum la Katiba, na pili ni mipaka ya madaraka hayo. Kwamba Bunge Maalum hili lina madaraka kuliko Bunge la kawaida, kwa maana ya Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi. Kwamba pamoja na madaraka makubwa hayo, bado Bunge hili linahitaji kuongozwa na busara ya kujua mipaka yake.

Bunge Maalum la mwaka 1977, mipaka yake ilikomea kwenye mamlaka ya Chama kwa sababu wakati huo Chama, kwa maana ya CCM, kilikuwa kimeshika hatamu za uongozi. Bunge Maalum la sasa, 2014, mipaka yake inakomea kwenye mamlaka ya wananchi kwa sababu wananchi ndio wenye Katiba na ndio wametoa maelekezo kwa Bunge Maalum hilo juu ya Katiba waitakayo.

Pamoja na ukweli huo, tunasikitika kusema hapa kwamba vyama vya CCM na CHADEMA, tayari vinakwenda kinyume na mantiki hiyo ya Sokoine. CCM imeweka msimamo kwa wajumbe wake kung’ang’ania muundo wa Mungano wa Serikali mbili. CHADEMA nao wameweka msimamo na wabunge wake wa kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali tatu.

Vyama hivyo vinataka kujipa madaraka makubwa kuliko madaraka waliyonayo wananchi wao. Badala ya kung’ang’ania mambo ya msingi ambayo wananchi wao wanataka yawemo kwenye Katiba Mpya yao, wao wameng’ang’ania muundo wa Muungano wa Serikali mbili au tatu.

Linapokuja suala la kulipana posho za vikao, vyama hivyo havionyeshi tofauti yoyote, vimeungana na kuwa wamoja. Hapo ndipo wananchi wenye nchi yao na Katiba yao wanapovishangaa vyama viwili hivi viwili na vingine vinavyounga misimamo hiyo, wakati kuna mambo mengi ya msingi ndani ya Rasimu hiyo ya Katiba.

Hivi kweli wajumbe wao na vyama vyao, wanaelewa ni nini maana ya Bunge Maalum la Katiba? Wanaelewa jukumu la Bunge hilo? Wanaelewa Bunge hilo linawajibika kwa nani? Tunadhani, misimamo hiyo ya CCM na CHADEMA, inalidhalilisha taifa hili.

No comments:

Post a Comment