WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, March 22, 2014

Kikwete ‘avuruga’ mjadala


Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma jana. Picha na Michael Jamson 

Rais Jakaya Kikwete jana alibadili upepo wa mchakato mzima wa Katiba baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa Serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa na maneno ya ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba, Rais Kikwete alisema  suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.
Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka Serikali tatu waangalie changamoto zake na kuzitafutia majibu, kwa maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.
Alisema ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo huo una gharama na utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM inaweza kuzimaliza kero za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.
Huku akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP) na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa sababu mbili kubwa  za kupendekeza muundo wa Serikali tatu;
“Sababu ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo matakwa ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar.  Sababu ya pili muundo huo unatoa majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili.”
Aliongeza, “Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo wa Kiswahili wengi wape. Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume kwamba hazionyeshi ukweli huo. Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu siyo yangu.” Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, “Watu wanasema Watanzania waliotoa  maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820 sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu 303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano na wala hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni.”
Alisema hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka Serikali tatu.
“Watu wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67), inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu muungano watu 17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa na asilimia 37.2 na waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8, Serikali ya mkataba asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7” alisema. Alisema taarifa ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia 10.4 ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.
“Watu wanahoji kama Muungano ni jambo linalowakera sana Watanzania ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa hoja. Usahihi wa hoja hii ni upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumzia sababu ya pili ya tume kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku akifafanua kero zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; “Nyinyi ndiyo waamuzi, sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume yenyewe imekiri kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto zake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma.”

Alisema wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa kutafuta majibu mwafaka kuhusu changamoto za muundo wa Serikali tatu kwa sababu maelezo ya tume kuhusu muundo huo hayana majibu.
Aliongeza, “Kupanga ni kuchagua. Wanaounga mkono Serikali mbili wanasema mlolongo wa changamoto ulioanishwa na tume kuhusu Serikali tatu hautapunguza matatizo bali utayaongeza kuliko ilivyo sasa na wanasema changamoto hizo zinatatulika bila kuwepo Serikali ya tatu.”
Alisema kama mfumo wa Serikali tatu ukipita ni lazima Serikali ya tatu ijengewe msingi imara kwa sababu haitakuwa na chanzo cha uhakika cha mapato yake yatakayoiwezesha kusimama yenyewe na haitakuwa na chombo cha kukusanya mapato zaidi ya kutegemea kukusanyiwa mapato na nchi washirika.
“Kama tunataka Serikali ya tatu lazima tuitengenezee misingi ya uhakika. Hivi nani atakudhamini kwa virungu, pingu, magari ya kuwasha, majeshi au bunduki. Serikali hii ya tatu haidhaminiki wala kukopesheka,” alisema huku akitolea mfano jinsi mataifa kama Urusi yalivyoanguka baada ya kujitenga.
Huku akifafanua jinsi kero za muungano zilivyotatuliwa na kamati na tume mbalimbali mpaka kubaki kero sita, Rais Kikwete alisema Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar zimeamua kutumia mchakato wa Katiba  kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana kulikuwa na mambo 11 ya muungano, baadaye kuongezeka hadi mambo 22 na kusisitiza kuwa mambo mengi yaliibuka baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Alisema jambo ambalo  Serikali hizo mbili walikubaliana kuliondoa katika mambo ya Muungano ni suala la gesi asilia na mafuta.
Ammwagia sifa Warioba
Alisema Jaji Warioba wa wajumbe wenzake wa Tume ya Katiba wameandika Rasimu ya Katiba vizuri na kwa weledi wa hali ya juu, na kwamba wametoa maoni ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba tuliyonayo sasa.
“Katiba inayopendekezwa imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tuliokuwa nao na kuweka misingi mizuri kwa huko mbele tuendako,” alisema.
Alisema Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi kina kurasa 106, sura 17, hivyo wajumbe wa Bunge la Katiba wanapaswa kusoma kila kitu na kuelewa na kuamua kwa utashi wao.
“Uamuzi wako siyo uamuzi wa kuambiwa na mwenzako, unaulizwa na wenzako kwenye hilo tusemeje unasema na mimi nimeambiwa, ebo! Umeambiwa, umefundishwa na mimi nasema akili za kuambiwa…” alisema Rais Kikwete.

Mambo mengine
Pia Rais Kikwete aligusia suala la mbunge kupoteza ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi kwa miezi sita mfululizo, kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza.

Alisema anaungana na wote wanasema jambo hilo liangaliwe vizuri na kwamba anashauri kama akiwa kizuizi amepatikana na makosa apelekwe mahakamani.

“Kwa mazoea ya duania ukomo unawekwa kwa wakuu wa nchi, hawaweki ukomo kwa wabunge, Tanzania wanataka kuwa wa kwanza,” alisema Kikwete.

Kuhusu suala la ugonjwa alisema mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wake, hivyo siyo sahihi kumwekea mgonjwa muda maalumu wa kuugua kwake.
Huku akicheka, Rais Kikwete alisema kitendo hicho kitawafanya wabunge kuanza kutembea na dripu katika majimbo yao kabla hawajapona vizuri.

source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment