WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 19, 2014

Samia atamani busara za Kificho kuongoza Bunge

Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samia Hassan Suluhu.
“Uongozi  wa Bunge (Maalumu) la Katiba ni wa muda mfupi kuliko wa wizara nilizokwisha kuziongoza…Ikiwa nimeweza yote hayo, sidhani kama mengine yanayokuja yatanishinda.”
Hiyo ni kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Hassan Suluhu.

Anatoa kauli hiyo, akionyesha uzoefu wake, ambao unampa imani kubwa ya kumudu kazi ya kuliongoza Bunge hilo, ambalo ni la kihistoria hapa nchini.

Samia, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), anasema katika mahojiano maalumu kuwa kamwe hawezi kushindwa kuliongoza Bunge hilo.

Anasema siri kubwa ya kujiamini kwake huko inatokana na uongozi wa Bunge hilo kuwa ni wa muda mfupi tu.

Hiyo ni kwa kulinganisha na muda wa uongozi aliokwisha kuutumia katika kuziongoza wizara kadhaa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibara (SMZ) na zile za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anasema tofauti na muda wa uongozi wa Bunge hilo, muda mrefu tangu mwaka 2000, ameweza kuongoza wizara mbalimbali, ikiwamo Wizara ya Kazi, Jinsia, Maendeleo na Watoto (2000-20025) ya SMZ.

Anataja wizara nyingine, ambayo ameiongoza kuwa ni ya Utalii, Biashara na Uwekezaji (2005-2010) ya SMZ kabla ya wizara anayoiongoza hivi sasa tangu mwaka 2010.

“Uongozi wa Bunge la Katiba ni wa muda mfupi kuliko wa wizara nilizokwisha kuziongoza,” anasema Samia, ambaye ni Mbunge wa Makunduchi (CCM).

Anaongeza: “…Ikiwa nimeweza yote hayo, sidhani kama mengine yanayokuja yatanishinda.”

Samia anasema katika miaka minne aliyokuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alifanikiwa kutatua kero za Muungano kutoka 13 na kubakisha moja.

Anasema aliposhika nafasi hiyo alikuta kuna kero 13 za Muungano.

Kwa mujibu wa Samia, kati ya kero hizo, mbili zimetatuliwa na nyingine mbili zikaongezeka.

Hata hivyo, anasema hizo mbili amefanikiwa kuzitatua zote na sasa imebaki moja ya kiuchumi.

Miongoni mwa kero hizo, ni pamoja na utekelezaji wa haki za binadamu kwa Zanzibar na uwezo wa Zanzibar kujiunga na Merchant Shipping Act ya Jamhuri ya Muungano.

Kero nyingine ni kujiunga na International Maritime Organization (Imo) na Zanzibar kushiriki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Nyingine ni Zanzibar kulipa kodi nje ya nchi, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kulipa kodi mara mbili na kuvua katika ukanda wa uchumi bahari kuu.

Imo pia inayohusu ongezeko la bei ya umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenda Shirika la Umeme Zanzibar (Zesco) na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.

Anawaahidi vijana kuwapa nafasi ili watoe michango yao kwenye katiba.

Anasema amejifunza kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kuwa ni umakini katika Bunge, utulivu na ustahamilivu.

Samia mwenye Shahada ya Uzamili katika masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, anasema ana uzoefu wa miaka 10 kama mwakilishi na miaka minne akiwa mbunge.

Mbali na hayo, anasema kwamba, ameshakuwa waziri katika wizara tatu na anaahidi kufanya kazi katika nafasi ya makamu mwenyekiti wa Bunge hilo kwa uadilifu na uaminifu.

Samia alishinda nafasi ya makamu mwenyekiti wa Bunge hilo kwa kupata kura 390 kati ya kura 523 zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake, Amina Abadallah Amour,  aliyepata kura 126. Kura saba ziliharibika.

Anasema atazitumia busara za aliyekuwa Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho, kuendesha Bunge hilo kwa ufanisi.

Pia anaahidi kushirikiana na mwenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kuhakikisha Watanzania wanapata katiba mpya wanayoitarajia.

Samia alizaliwa Januari 27, 1960. Amekuwa Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, visiwani Zanzibar tangu mwaka 2010.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment