WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 6, 2014

Malumbano kura ya siri, wazi isiwe chanzo cha kuvuruga Katiba Mpya

Katuni
Mjadala mkali umedumu kwa siku kadhaa bungeni mjini Dodoma kuhusiana na namna ya upigaji kura juu ya kupitisha vifungu vya rasimu ya katiba mpya.
Baadhi ya wajumbe wamekuwa wakisisitiza kuwa demokrasia ya kweli itapata nafasi yake ikiwa utaratibu wa kupiga kura miongoni mwao utakuwa wa siri.

Wengine wanapinga aina hiyo ya upigaji kura, wakisema kwamba njia nzuri ni kutekeleza zoezi hilo kwa uwazi ili msimamo wa kila mmoja ujulikane kwa Watanzania.
Mgongano huu wa mawazo kuhusiana na kura ndiyo ulioibua malumbano makali, kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita na hadi kufikia jana jioni.
Kutokana na malumbano hayo, wajumbe wamedhihirisha jambo moja ambalo kimsingi halipaswi kuendelezwa kwani siyo zuri kwa mustakabali mwema wa taifa.
Nalo ni kwamba, mapema kabisa, kabla hata ya kuanza kupitisha vifungu vya rasimu ya katiba, wajumbe wameonyesha kugawanyika kwa kiasi kikubwa.
Hii inaonyesha kuwa baadhi ya wajumbe wamejisahau. Wameacha kufikiria maslahi ya taifa kwa kuangalia uzito wa hoja wanazojadili na badala yake kuruhusu siasa, wakitoa hoja kwa kuzingatia itikadi na imani za vyama na makundi yao.

Hadi kufikia jana jioni, tayari wajumbe walishagawanyika katika makundi makuu hayo mawili, ambayo ni ya wale wanaopendekeza utaratibu wa kupiga kura kwa siri na wengine wanaotaka kura za wazi.
Kadri inavyoonekana, wajumbe wengi walio wafuasi wa chama tawala ndiyo wanaotaka kura za wazi huku wengi wanaotoka upinzani wakisititiza kuwa upigaji kura unapaswa kuwa wa siri.
Siyo nia yetu kutaka kueleza ni upande gani ulio sahihi kati ya pande hizo mbili. Bali, NIPASHE tunadhani kwamba malumbano hayo yenye mwelekeo wa vyama na makundi hayana tija kwa mustakabali wa taifa letu, hasa kama kweli tunataka kupata katiba mpya inayokidhi matakwa ya Watanzania wengi.

Kamwe, hatuamini hata kidogo kuwa maamuzi ya wajumbe katika kukamilisha mchakato huu wa kihistoria yatatokana na msimamo wa vyama vya siasa, makundi au utashi binafsi wa wajumbe.

Bali, kama ilivyowahi kusisitizwa mara kadhaa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ni vyema wajumbe wakaweka mbele maslahi ya taifa.

Tunadhani kwamba, ikiwa kila mjumbe atakuwa akifikiria maslahi ya taifa katika kila jambo ndani ya bunge hilo maalum, ni wazi kuwa uwezekano wa kupungua kwa malumbano utakuwa mkubwa. Maamuzi mengi yataendelea kufanyika kutokana na nguvu ya hoja na wala siyo ushawishi wa kiitikadi au makundi.

Kwa sababu hiyo, malumbano ya aina yoyote yale hayatachukua muda mwingi kwa hoja zisizolenga maslahi ya taifa. Wajumbe watakuwa wakipeana nafasi ya kusikiliza hoja na kuzitolea maamuzi kwa kuzingatia uzito wake tu; na wala siyo kuziunga mkono au kuzipinga kwa kulinganisha misimamo ya vyama na makundi yao.

Ikumbukwe kuwa Watanzania wengi wamekuwa na matumaini makubwa kwa wajumbe wanaoendelea na mchakato huu muhimu wa kupitisha rasimu ya katiba mpya ili mwishowe wakamilishe zoezi hilo kwa kupiga kura. Ustawi wa taifa hili katika kipindi cha sasa na miaka mingi ijayo uko mikononi mwa waheshimiwa hao.

Wakitumia maarifa yao kwa maslahi ya taifa, wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa na fursa nzuri ya kupitisha rasimu ya katiba itakayoendelea kudumisha udugu, mshikamano na ustawi wa taifa.

Hata hivyo, ikiwa wajumbe wataendeleza malumbano kama yaliyotawala kuanzia wiki iliyopita juu ya upigaji kura wa siri au wazi, taifa litaingia katika giza lisilotarajiwa.

Rasilimali fedha na muda iliyowekezwa kwa muda mrefu sasa katika kupitia mchakato wa kuandaa katiba hiyo mpya hadi kufikia bungeni itapotea bure.
Hili siyo jambo jema kwa taifa. Ni msiba utakaowaachia huzuni Watanzania wengi wenye ndoto za kuwa na katiba yenye kuzingatia masuala mengi muhimu kwa ustawi wao na taifa lao.
Kwa kuzingatia yote hayo, NIPASHE tunawasihi wajumbe wa Bunge la Katiba kuwa waepuke kujiingiza katika malumbano marefu kwa sababu tu ya kupigania maslahi ya vyama na makundi yao bali wakubali au kukataa hoja kwa kuzingatia uzito wa hoja. Tanzania kwanza.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment