WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, May 1, 2013

Mbunge ‘mpumbavu’ hatapigiwa kura 2015

BAADHI ya raia wa Ethiopia wamekuwa wakiishi kwa kuzingatia msemo mashuhuri ambao kwa namna fulani umebeba mantiki ya kifalsafa ndani yake.
Wanasema; “When spider webs unite they can entangle a lion.” Kwamba  utando wa buibui unapounganishwa basi huweza kumnasa hata Simba.”
Buibui ni mdudu mdogo na kimsingi, utando wake si imara ikilinganishwa na nguvu za mnyama Simba, lakini bado Waethiopia wanasema utando huo unapotanda vizuri, basi huweza kumnasa huyo Simba. Kwa maana nyingine, unaweza kusema jambo dogo linaweza kusababisha maafa makubwa.
Ni katika muktadha huo huo, tunaweza kuanza kulitazama Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama chombo kinachoashiria au kuthibitisha kupungua kwa kiwango cha kuvumiliana miongoni mwa Watanzania na hata kupungua kwa ustaarabu na staha, miongoni mwa Watanzania. Kwa mfano, tumemsikia bungeni, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi akitamka kuwa Baraza la Mawaziri limejaa wapumbavu!
Si kwamba Mbilinyi ambaye aliwahi kuwa mwanamuziki wa bongoflava alitamka hayo maneno wakati akiimba mashairi au mistari ya bongo flava la hasha, alizungumza akiwa bungeni katika mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Sugu anajitetea ya kwamba maneno upumbavu si matusi lakini hata kama si matusi, ni lazima kila mahali kuna hadhi ya lugha au matamshi yake. Kwa mfano, lugha inayotumika katika vijiwe vya watumiaji wa dawa za kulevya na mihadarati mingine hata kama si matusi, haiwezi kutumika ndani ya Bunge.
Lugha inayotumika kwenye vijiwe mbalimbali vya mitaani (hata kama si lugha za matusi) nazo zina nafasi yake katika maeneo hayo husika.
Lugha ya kuitana wapumbavu, kwa watu walioko katika ngazi ya uongozi wa kitaifa ni sawa na lugha ya kihuni, na pengine inaakisi kiwango cha hadhi ya mtamkaji wa maneno hayo.
Kwa viongozi wa kitaifa kuitana au kutambulishana mbele ya umma (tena kupitia Bunge linalorushwa hewani moja kwa moja nchi nzima), kama ni wapumbavu (hata kama upumbavu si tusi) ni kuashiria shari. Ni kuashiria kutoweka kwa ustaarabu kati ya viongozi husika.
Katika mfumo wa demokrasia ambao bila shaka vyama vyote vya siasa nchini vinautumikia hata kama si kwa dhati, kura za wananchi ndizo, kwa kawaida, huamua nani aongoze nchi. Na waliopewa mamlaka ya kuongoza nchi, ni lazima waunde serikali. Na kwa hiyo basi, mfumo wa dekomrasia kwa wanaouamini kwa dhati katika mfumo huo hawana budi, hasa katika vyombo vya uwakilishi kama Bunge, kushindanisha hoja zao kwa kuzingatia nguvu za hoja husika na si nguvu ya misamiati ya kukera wengine, misamiati au maneno yanayoashiria shari na kimsingi, yanayoweza kusababisha wadogo wakapuuza kuheshimu wakubwa.
Kwa bahati mbaya, Mbunge Mbilinyi hakuwa tayari kuomba radhi bungeni na hata kufuta kauli yake kwa kuwa tu, neno pumbavu au mpumbavu lipo katika biblia.
Kwa kawaida, madhara ya matumizi ya maneno fulani hutegemea sana mazingira maneno hayo yanapotamkwa na msukumo wa utamkaji wa maneno husika.
Inawezekana, tunao mawaziri ambao hawafanyi kazi yao vizuri na kwa kweli nami nakubaliana na hali hii ya kwamba kuna mawaziri ni mzigo tu kwa nchi, ni kama hawapo na hata ukitathmini utendaji wao wa kazi, huoni mabadiliko yoyote katika sekta wanazosimamia.
Lakini hata kama kuna viongozi wa namna hii, haikuwa sahihi kwa mbunge kuwaita wapumbavu, kwa kuzingatia mazingira ya kibunge.  Pengine, kuwaita hivyo inawezekana katika vijiwe vya kuvutia bangi na kwingineko, lakini kwenye chombo rasmi cha uwakilishi wa umma ni kuvuka mipaka.
Tutafakari, inawezekana kabisa katika maisha yake Joseph Mbilinyi amewahi kushuhudia wazazi wake wakiwa wametenda makosa ya hapa na pale, makubwa au madogo kwa sababu mbalimbali, za msingi au zisizo za msingi. Je, mbunge huyo atakuwa tayari kuwatamkia wazazi wake kuwa ni wapumbavu? Je, anaweza kutamka hivyo kuwa wazazi wake au mzazi wake ni mpumbavu kwa sababu tu neno pumbavu si tusi?
Bila shaka, jibu ni rahisi tu kwamba hawezi kuwatamkia hivyo licha ya udhaifu fulani ambao anaweza akawa ameubaini. Kwa nini hawezi? Hawezi kwa sababu neno hilo ingawa si tusi, lakini halibebi ustaarabu kati ya mwana na wazazi wake.
Tutambue ya kuwa, mawaziri ambao wameitwa wapumbavu ni watu wenye familia zao na miongoni mwao ni wachapakazi ingawa pia wapo ambao ni butu katika utendaji kazi.
Lakini si Joseph Mbilinyi pekee, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia naye alitamka bungeni akimweleza mbunge mwenzake kuwa; yeye (Nkamia) hazungumzi na mbwa bali anazungumza na mwenye mbwa.
Bahati nzuri, Nkamia alitambua makosa yake katika kutamka maneno hayo ndani ya ukumbi wa Bunge, akaomba radhi. Inawezekana kwa mfano, kama mtu fulani akatamka maneno hayo kwenye vijiwe vya kuvuta bangi au maeneo mengine yasiyo ya kistaarabu, asingelazimika kuomba radhi na tena kila mmoja katika eneo hilo asingebaini kama ni tatizo kutamka hivyo.Sasa kwa kuzingatia msemo wa Waethiopia, utando wa buibui unaweza kumnasa Simba na kwa hiyo, kauli zenu hizi wabunge wetu zinaweza kuashiria machungu mbele ya safari zenu za kisiasa na hasa katika majukwaa ya kuomba kura siku zijazo.
Tunaweza kutamka maneno ambayo yanaweza kufurahisha baadhi ya mashabiki wetu lakini gharama zake zinaweza kuwa kubwa zaidi ya furaha hiyo ya muda mfupi kutoka kwa mashabiki.
Tusiitane wapumbavu wala mbwa bungeni, jiulizeni, watoto wenu wanaweza kujifunza nini kutokana na kauli zenu hizo?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

source: Raia Mwema:  Godfrey Dilunga

1 comment:

  1. Chukulia suala la wagombea ubunge wa CCM kutoroka midahalo wakati wa kampeni ule mwaka 2010. Sina sababu ya kuminya maneno: huu ulikuwa ni upumbavu. Wakati huu wanatamba Bungeni, lakini mimi sijasahau upumbavu waliofanya.

    Hivi kweli, tunawafundisha nini watoto wetu, endapo hatujihusishi na mijadala na midahalo, ambayo ni njia moja ya kuelimishana? Ilichofanya CCM ni kuwafundisha watoto wetu upumbavu.

    ReplyDelete