WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 9, 2013

Ya Kinana na siasa zetu za reja reja


“ Mamlaka zote msingi wake ni imani, tunawajibika katika kuyatekeleza yaliyo kwenye mamlaka zetu,  na kwamba, mamlaka yatatokana na watu, kwa ajili ya watu, na chemchem zote za fikra ziachwe hai”- Benjamin Disraeli.

Katika  nchi, ustawi wa demokrasia na maendeleo ya kiuchumi huimarika zaidi kwa kuwapo na uhuru wa kifikra. Kwamba kuwapo kwa  tofauti za kifikra si jambo baya, bali ni jema na la muhimu kwa maendeleo ya nchi, kisiasa, kijamii na kiuchumi.  Kwamba siku zote, mawazo na mahitaji ya wananchi yatangulizwe.

Hivyo basi, ustawi wa demokrasia na maendeleo ya kiuchumi  huchangiwa pia na kuwapo kwa  wananchi wenye uwezo wa kutathmini michango itokanayo na wengine katika jamii husika.

Ni muhimu pia kukawapo wanasiasa wenye uwezo wa kutathmini mambo na kuja na hoja zenye mashiko kwa maslahi ya nchi, badala ya hoja zenye kulenga kuibakisha nchi kwenye hali ya kugota kisiasa na kimaendeleo ya kiuchumi.

Kuwapo kwa siasa za vyama vingi ni jambo jema kwa nchi, lakini, kukosekana kwa umakini katika kuendesha siasa za vyama vingi hupelekea kupunguza ladha na maana ya kuwa na siasa za vyama vingi. Maana, vyama vingi ina maana pia ya kuwapo kwa fikra nyingi zenye kutofautiana na hata kufanana, lakini, ni vema zikawa ni zenye kujenga.

Nahofia, kuwa katika wakati tulio nao sasa, pamoja na hoja za msingi zinazoibuliwa kwenye jamii, bado nchi yetu imekumbwa na balaa la kuwapo kwa siasa za reja reja ( retail politics). Ni siasa  zisizo na maslahi kwa nchi.

Ningependa hapa nitoe mfano wa siasa za rejareja zenye kupunguza ladha ya siasa za ushindani wa vyama vingi. Hivi karibuni  Katibu Mkuu wa sasa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana amekuwa akizungumzwa kuhusishwa na kashfa ya kusafirisha pembe za ndovu.

Hakika, haya ya Kinana ni mfano wa siasa zetu za reja reja. Binafsi niliyasoma zamani sana maelezo ya  Kinana mwenyewe juu ya asivyohusika na kashfa hiyo, ingawa ni kweli kuwa pembe hizo za ndovu zilikamatwa zikiwa zimepakiwa kwenye meli ambayo Kinana ana hisa nayo kwenye umiliki.

Inavyoeleweka, si kwa Kinana tu, hata kwa yeyote mwenye kutaka kujua. Kwamba  kwenye taratibu za usafirishaji wa majini kuna Wakala wa Meli ( Shiping Agency) na wenye kuhusika na taratibu za kupakia mizigo kwenye meli kabla haijasafirishwa, (Clearing and Fowarders).

 Hivyo basi, mmiliki wa meli ni mtu mmoja na wenye kukagua na kuipitisha mizigo ni wengine. Mmiliki wa meli anaweza kabisa asijue kilicho ndani ya shehena kwenye meli yake mbali ya kile kilichoandikwa kwenye nyaraka alizokabidhiwa na wahusika wa zoezi la ukaguaji na upakiaji wa shehena ndani ya meli.  Na katika hili, Kinana mwenyewe ameshaweka wazi, kuwa yeye si mtendaji wa shughuli za kila siku za kampuni hiyo ya meli ambayo ana hisa nayo kwenye umiliki.

Hivyo basi, kwa akili ya kawaida tu, binafsi sioni ni kwa namna gani Kinana ahusishwe na kashfa hii. Isitoshe, shauri lenyewe lilishafikishwa mahakamani.  Hivyo, hili si shauri jipya. Vinginevyo, kuwepo ushahidi wa moja kwa moja wenye kumhusisha Kinana na kadhia ili kulifanya kuwa ni shauri jipya.
Kwa sasa hakuna kitu kama hicho. Badala yake, siasa hizi za reja reja ndizo zinazofanya Abdulrahman Kinana pasipo kutendewa haki, ahukumiwe mitaani.

Ndio, katika hili  Abdulrahman Kinana ni mhanga wa siasa za reja reja ambapo, upinzani wa kisiasa, kwa kutumia hoja dhaifu kama hizi au zinazofanana nazo, badala ya kumboboa Kinana kisiasa, itakuwa ni kudhihirisha kiwango cha chini cha ujengaji wa hoja mbele ya watu makini wenye kuchambua mambo kwa mtazamo usiokuwa na upendeleo wala ubaguzi. Na watu hao makini siku hizi ni wengi, hata miongoni mwa watu wa kawaida vijijini.

Na hakika inasikitisha, kuwa jamii yetu imekumbwa na wimbi hili la siasa za reja reja ambazo wenye kuzifanya, yumkini huwa na malengo ya kuwachafua wahusika na hata kuwavunjia hadhi na heshima katika jamii. Si siasa za kistaarabu. Tukiacha haya yakaendelea kushamiri bila kukemewa, basi, ni wengi watakuwa wahanga wa siasa hizi.

Hivyo, ni  vema na ni busara, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa kwanza, sote  tukashiriki kupiga vita siasa hizi za reja reja ambazo, kimsingi, zinachangia kufifisha maana nzima ya ushindani wa kisiasa wenye maana.

Kwamba tuhakikishe kuwa roho ya upinzani na ushindani wa kisiasa haipotei. Maana, ushindani wa kisiasa ni chachu ya kuongeza kasi ya ustawi  wa jamii, kisiasa, kiuchumi na kimaadili. Nahitimisha

source: Raia Mwema  Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment