WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, May 14, 2013

Magufuli aleta mwarobaini foleni Dar

Waziri wa Wizara ya ujenzi, Dk. John Magufuli.
Serikali imetenga fedha katika mwaka wa fedha 2013/2014 zitakazotumika katika kununua kivuko kitakachofanya safari zake kutoka jijini Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa ni miongoni mwa jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.
Bajeti ya Wizara ya Ujenzi inaonyesha kutengwa kwa Sh. milioni 4,484  kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo ununuzi wa kivuko.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Wizara hiyo,  Dk. John Magufuli, alipokuwa akiwasilisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/2014 bungeni jana.

Alisema fedha hizo zitatumika pia kununulia boti ya uokoaji, mashine ya kisasa ya kukatia tiketi kwa kivuko cha Magogoni na vifaa vya karakana ya Tamesa.

Aidha, alisema upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa maegesho ya usafiri wa majini kati ya Dar es Salaam hadi Bagamoyo umetengewa Sh. milioni 215.

“Ujenzi wa vituo vya kusubiria kivuko kati Dar es Salaam hadi Bagamoyo katika maeneo Govenor Jet (Kivukoni), Jangwani Beach na Rungwe Hotel umetengewa Shilingi
milioni 600,” alisema.

Kuhusu msongamano jijini Dar es Salaam, Dk. Magufuli alisema ujenzi wa barabara katika jiji hilo, kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari ulioanza utekelezaji wake katika bajeti ya mwaka 2009/2010 umetengewa Sh. milioni 28,634.

Alisema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya barabara kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.

Akifafanua miongoni mwa miradi iliyotengewa fedha, alisema ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Ubungo Maziwa-External na Tabata dampo hadi Kigogo umetengewa Sh. milioni 3,000.

Alisema Sh. milioni 5,000 zimetengwa kwa ajili ya barabara ya Kimara-Kilungule-External wakati Sh. milioni 6,000 kwa barabara za Mbezi (Morogoro Road)- Malambamawili- Kinyerezi- Banana.

Shilingi milioni  5,000 kwa barabara ya Tegeta-Kibabaoni-Wazo Hill-Goba-Mbezi Morogoro Road.

Sh. milioni 1,000 zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya barabara za juu eneo la Tazara jijini humo.

Kwa upande wa daraja la Kigamboni, Dk. Magufuli alisema mradi wa daraja litakalounganisha Jiji la Dar es Salaam na mji wa Kigamboni katika mwaka huu wa fedha limetengewa Sh. milioni 3,000.

Kadhalika, alisema milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa awamu ya kwanza itakayohusisha ujenzi wa sehemu ya Dar es Salaam hadi Chalinze kwa kiwango cha Expressway.

Alisema kampuni 19 zimejitokeza kuomba kujenga barabara kwa kiwango cha Expressway kutoa Dar es Salaam-Chalinze hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 200. “Maandalizi ya mradi huu utakaotekelezwa kwa ubia baina ya serikali na makampuni binafsi yameanza,” alisema na kuongeza kuwa uchambuzi wa maombi ya kampuni hizo unaendelea.

Kuhusu barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo hadi Msata, Dk. Magufuli alisema Sh. milioni 10,885.24 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Wazo Hill kupitia Bagamoyo hadi Msata.

Alisema mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa Agosti 11 mwaka 2010 kwa gharama ya Sh. milioni 89,610.  Alisema kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami inaendelea lengo likiwa ni kuendelea na usanifu wa barabara ya Bagamoyo-Sadani-Tanga yenye urefu wa kilomita 178 na kuongeza kuwa Sh. milioni 444.14 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa barabara hiyo ya Bagamoyo kupitia Sadani hadi Tanga.

MAKANDARASI 366 WAFUTWA

 Dk. Magufuli alisema hadi kufikia Aprili mwaka huu, Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini ilifuta usajili wa makandarasi 366 walioshindwa kuzingatia sheria na taratibu za ukandarasi.

Alisema bodi hiyo ilifanya ukaguzi katika miradi 2,480 na kati ya hiyo 1,672 sawa na asilimia 67.4 ilionekana kutekelezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za usajili na miradi 808 ambayo ni sawa ni asilimia 32.6 ilikiuka sheria na taratibu hizo. Wizara hiyo  ililiomba Bunge kuidhinishia Sh. 1,226,431,739,000.

KUWAJIBISHA TANROADS
Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Wizara ya Ujenzi kuwawajibisha maofisa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) watakaoshindwa kusimamia ujenzi bora wa barabara na kusababisha fedha nyingi kupotea.

MAONI YA KAMATI
Akisoma taarifa ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Juma Kapuya, alisema taifa litaendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa barabara zilezile kila mwaka kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa ujenzi wa barabara hizo.

Alisema pamoja na kuwapo kwa vituo vingi vya mizani, bado barabara zimekuwa zikitengenezwa matuta na mabonde jambo ambalo linathibitisha kuwa ama ujenzi wa barabara hizo haukuzingatia viwango au magari yenye uzito kuliko uwezo wa barabara huendelea kupita siku hadi siku.

“Endapo barabara zitaendelea kuharibika maofisa wa Tanroads waliopo katika kanda husika wawajibishwe ili wengine wachukue nafasi zao na kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema.

Ikizungumzia hali ya barabara katika jiji la Dar es Salaam, Kamati ilishauri kuwa wakati umefika kwa matatizo ya Dar es Salaam kutatuliwa kwa mkakati maalumu wa kuendeleza na kuboresha miundombinu ya Jiji hilo kwa kujenga barabara zipitazo juu.

Aidha, ilisisitiza uharakishwaji wa kuanzisha usafiri wa boti kutoka Bagamoyo mpaka Feri jijini Dar es Salaam.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment