WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, May 27, 2013

Wanahabari na gharama za ukweli


TAALUMA ya habari inahusiana kwa wanahabari kusema yalo ya ukweli kwa jamii. Na jambo hili lina changamoto zake katika jamii zetu hizi.

Maana, ukweli una sifa na tabia zake. Ni kwa vile, ukweli nao una uhai. Ukweli unaishi. Katika kuishi kwake ukweli hupitia hatua tatu; Kwanza, kukataliwa, kwamba ukweli unapowekwa hadharani mara nyingi hukataliwa.

Pili; gharama, kwamba ukweli una gharama zake. Kwa anayesema ukweli awe tayari pia kulipa gharama za kusema ukweli. Na hapa kuna kisa cha bwana mmoja aliyekuwa na kiu ya kuupata ukweli. Alitembea huku na kule kuusaka ukweli. Na hamu yake ilikuwa kuupata ukweli mzima.

Siku moja katika pitapita zake, bwana yule  akaliona duka limeandikwa nje; “ Hapa tunauza ukweli!|”

Bwana yule akasimama. Akaona dukani kuna bei za ukweli zilizoandikwa. Kuna bei ya robo kilo ya ukweli. Kulikuwa na bei pia ya nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya kilo nzima ya ukweli.
Bwana yule aliyekuwa na kiu ya kuupata ukweli akaulizia bei ya kilo nzima ya ukweli. Mwenye duka akamwuliza kuthibitisha hitaji lake; “E bwana ee, unataka kilo nzima ya ukweli?”

“Ndio” Mwenye duka akamwambia aingie ndani dukani. Humo akamnong’oneza; “Bei ya kilo moja ya ukweli ni uhai wako!”

Basi, bwana yule mwenye kiu ya ukweli alitimua mbio na kuacha vumbi nyuma. Ndio, hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli.

Tatu; ukweli udhihiri, kwamba, hata baada ya kukataliwa, kuwa na gharama, lakini, hatimaye, siku zote, ukweli udhihiri. Yumkini ukweli ukachelewa kufika, lakini, siku zote hufika. Na uhalali wake huanzia pale ulipoanza kukataliwa.

Kazi ya uanahabari inatutaka pia kuwa tayari kulipa gharama za kusema ukweli. Leo ni ukweli, kuwa baadhi ya wanahabari wanatumika zaidi kisiasa badala ya kuwatumikia watu.

Leo utamkuta mwanasiasa anaongozana kwenye mkutano na  wanahabari wake. Imekuwa kawaida siku hizi kwenye mkutano kusikia wanahabari wakitambulishwa rasmi kwa majina na vyombo vyao wanakotoka.

Binafsi nimekulia katika nchi hii. Hakika, mambo hayo hayakuwa yakifanyika huko nyuma. Maana, mwanahabari ni kazi yake kuwa kwenye mikusanyiko na kufanya kazi yake ya uanahabari. Hana haja ya kualikwa au kutambulishwa na mwanasiasa. Isitoshe, jambo hilo la kutambulishwa laweza kumuweka katika mazingira hatarishi katika kazi yake.

Wanahabari tunaojitahidi kusema ukweli tunakabiliwa na changamoto nyingi. Binafsi, leo naweza kukutana na watu wa upande mmoja wa kisiasa na nikaambiwa kuwa niko upande mwingine. Na nikikutana na wa upande mwingine naambiwa niko na wa upande mwingine.

Kuna wanaodhani kuwa haiwezekani kwa mwanahabari kuwa kwenye upande wa umma. Hivyo basi, kuwa kwenye upande wenye kulinda maslahi ya nchi na umma kwa ujumla. Na tunaojitahidi kuwa kwenye kundi hili tumo pia kwenye hatari kubwa kwa watu wenye kutanguliza fikra binafsi na za kimakundi badala ya za kitaifa, hivyo basi, kwa wasiotanguliza yalo na manufaa kwa umma.

Ni ukweli, kuna wenye kuona wanavyopenda kuona. Kuna wenye kusikia wanavyopenda kusikia. Kuna wakati nikiwa Sweden nilizungumza na vijana wanafunzi wa Kisweden kuhusu mgogoro wa Congo DRC. Haraka vijana wale walitaka niwaambie ni upande gani wa kushabikia kati ya Rais Kabila na waasi wanaompinga.

Niliwaambia, kuwa ni muhimu kwanza wakaielewa historia ya Congo kabla ya kuhitimisha ni nani mbaya na nani mzuri. Ndio, tumekuwa wepesi wa kukimbilia kushabikia mambo kuliko kutafakari kwanza.

Kuna siku mtoto wangu wa miaka 12 alinifanya nitafakari sana. Nilimpa asome hoja zangu zilizokuwa zikijibu mashambulizi ya hoja kutoka kwa walionishambulia kwa hila.

Mwanangu yule alisoma kwa makini. Kisha akaniangalia na kunitamkia; “Baba, hoja zako zimesimama vema, lakini nikuulize, je, unaweza kuniambia udhaifu wako katika hoja ulizozijenga?”

Naam, wanadamu mara nyingi tunaona udhaifu wa wenzetu, lakini, hatufikiri juu ya udhaifu wetu ambao tunaowaita maadui zetu nao wanaweza kuutumia katika kujenga hoja zao.

Ndugu zangu wanahabari, mna dhamana kubwa katika kuitumikia jamii yetu. Mjitahidi katika kusimamia kwenye ukweli. Mjitahidi sana pia katika kusoma vitabu ili muweze kujenga uwezo zaidi katika kazi yenu ya kuutumikia umma.

source: Raia: mwema  Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment