WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 23, 2013

Kingunge: Nipo fiti, uchumi huria umeshindwa


Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru
Siku moja baada ya kuzushiwa kifo, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, ameibuka na kusikitika kwa uzushi huo, huku akichambua hali ya mambo ilivyo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, Kingunge ambaye ametumikia awamu nne za utawala wa nchi hii tangu utawala wa Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, alisema kuwa siasa ya ujamaa kwa sasa ndiyo suluhisho kwa ustawi wa uchumi nchini baada ya mfumo wa soko huria kushindwa.

Kingunge ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao walikuwa waumini wakubwa wa siasa ya Ujamaa, alielezea matamanio yake ya kurejeshwa kwa Azimio la Arusha ambalo lilikuwa linaelezea utekelezaji wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea nchini.

Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa amestaafu katika nafasi zote za kiserika na kwenye chama chake, alisema kuwa Azimio la Arusha lilitoa fursa kwa wananchi wengi wakiwamo vijana kupata ajira na kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumu tofauti na ilivyo sasa kupitia uchumi wa kisasa wa soko huria.

Aliongeza kuwa, wakati wa Azimio la Arusha haikuwa rahisi kukuta vijana wakiwa mitaani bila ya kuwa na kazi za kufanya, lakini hivi sasa wimbi la ukosefu wa ajira limekuwa kubwa na kuwaathiri zaidi vijana.

Kuhusu ukuaji wa uchumi, Kingunge alisema uchumi wa soko huria hauwezi kumaliza tatizo la ajira nchini hususani kwa vijana wanaomaliza shule na vyuo.

Baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967, njia zote za uchumi ziliwekwa chini ya umiliki wa dola.

Kupitia Azimio la Arusha, yalianzishwa mashirika ya umma zaidi ya 400 ambayo yalisaidia pamoja na mambo mengine, kutoa ajira kwa wananchi wengi.

Alisema bado anaamini kwamba Azimio la Arusha lilikuwa na maana kubwa kwa Watanzania.

Mzee Kingunge hata baada ya kusambaratika kwa siasa ya Ujamaa duniani mwishoni mwa miaka ya themanini na mwanzoni mwa miaka ya tisini, aliendelea kuwa muumini wa itikadi hiyo iliyoasisiwa nchini na Baba wa Taifa,  Mwalimu Julius Nyerere.

URAIS CCM
Akizungumzia wanachama wa CCM wanaotaka kugombea urais mwaka 2015 kuanza kujitangaza na kupitapita kwa wanachama, alisema hilo siyo kosa ilimradi wasikiuke utaratibu wa chama.

Alisema siyo dhambi kwa wanachama wa CCM kuwa na matarajio ya kushiriki katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, lakini kitu cha msingi cha kuzingatia ni kufuata utaratibu uliowekwa na chama hicho.

“Siyo mara ya kwanza jambo hili kutokea na misingi ya chama chetu inayongoza katika kuchagua na kuchaguana, mimi naamini wanaotaka urais mwaka 2015 watafuata utaratibu,” alisema.

“Mwiko siyo mtu kutaka kugombea, mwiko ni kutofuata utaratibu uliowekwa na chama na hao wanaotaka lazima waheshimu utaratibu wa chama,” alisema Kingunge.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alifanya mkutano na wabunge wote wa chama hicho, na miongoni mwa mambo ambayo yanadaiwa yalijadiliwa ni kutolewa kwa ruksa kwa wanaoutaka urais kupitia chama hicho kujipitisha kwa wanachama alimradi hawavunji kanuni za chama, kama kujenga makundi ya kuhasimiana.

Kingunge alisisitiza kwamba kama Mwenyekiti wa chama amekwisha kusema hayo, hakuna wa kutoa kauli nyingine kwani ndiye msemaji wa chama.

KUZUSHIWA KIFO
Akizungumzia uvumi wa kuwa amefariki dunia ulionezwa juzi katika baadhi ya mitandao ya kijamii, Kingunge alisema suala hilo halikumshitua kwa kuwa anajua kila binadamu ataonja mauti.

Hata hivyo, alisema waliopata shida ni watoto wake, marafiki zake, ndugu wa karibu na jamaa wengine wanaomfahamu ambao alisema walimpigia simu na hata wengine kuangua kilio.

“Kama aliyeeneza uvumi huo alitaka kunipa tabu mimi, basi waliopata tabu ni wanaonifahamu mimi kwa kuwa watoto wangu, ndugu zangu walishtuka kusikia taarifa hizo,” alisema.

Alisema ni mzima wa afya na kwamba juzi aliongea kwa simu na kada mmoja wa CCM ambaye yupo jijini Mwanza na muda mfupi baada ya kukata simu alipigiwa tena na mtu huyo akimpa pole, na baada ya hapo mfululizo wa simu zilianza kumiminika kwake.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment