WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, May 13, 2013

Homa pambano la vigogo


Na Clara Alphonce, Mwananchi Share

Dar es Salaam. Wakati homa ya pambano la watani wa jadi ikizidi kupamba moto, Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu, ameponda majigambo ya wapinzani wao Yanga waliopania kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 katika msimu uliopita.

Simba na Yanga zinafunga pazia la Ligi Kuu Bara Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku vijana hao wa Jangwani wanaojivunia kiwango kilichosimama kwenye mstari, wakitwaa ubingwa mapema.

Timu zote zimekwenda kujichimbia Zanzibar kujiandaa na pambano hilo na zinatarajia kurejea Dar es Salaam siku moja kabla ya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Tofauti na mechi nyingine za ligi zinazozikutanisha timu hizo, safari hii vigogo hao watashuka dimbani kwa lengo la kulinda heshima, kwani tayari bingwa ameshapatikana.

Kauli ya Kocha Kihwelu imekuja kama majibu kwa Wazee wa Yanga, waliodai kuipeleka timu visiwa vya Pemba kama sehemu ya maandalizi ya kweli ili kulipa kisasi cha kufungwa bao hizo msimu uliopita.

Akiibeza kauli hiyo, Kihwelu alisema anakiamini kikosi chake, ambacho sehemu kubwa kinaundwa na wachezaji vijana kina uwezo wa kuifunga Yanga.

“Nachoweza kusema kwamba, Wazee wa Yanga wamepiga kelele hawajui soka lilivyo,” alisema kocha huyo aliyewahi pia kuchezea timu hiyo miaka ya nyuma.

“Wanachosema, wao ni sawa na mvuvi anayekwenda baharini kuvua samaki akimini ni lazima arudi na samaki, wakati siku nyingine anaweza kurudi bila samaki,” alisema Kihwelu.
Kihwelu alisema hakuna uwezekano wa kikosi chake kufungwa kwenye mchezo huo, achilia mbali bao tano ambazo Yanga wamepania kulipa kisasi.

“Tumejipanga kushinda mchezo huu, hatutawapa nafasi Yanga hata kidogo. Vijana wangu wameonyesha kiwango kizuri na nina imani watashinda mchezo huo,” alitamba Kiwhelu.

Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga, alithibitisha jana kikosi chake kwenda kupiga kambi Zanzibar kwa ajili ya mechi hiyo. Kwa kawaida, Simba hupenda kuweka kambi Zanzibar kila wanapojiandaa kucheza na Yanga, huku wapinzani wao hao wakiwa na utamaduni wa kuweka kambi Bagamoyo.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment