WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 9, 2013

Chadema ilivyolegeza msimamo kuhusu mchakato wa Katiba

 
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (kushoto) akizungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndani ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma. Picha na Maktaba 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi  (email the author)

Mchakato wa kuandika Katiba Mpya umepamba moto, huku Tume ikielekea kwenye hatua ya Mabaraza ya Katiba, baadhi wadau wakidai  mabaraza hayo yana kasoro, yamechaguliwa kiitikadi.

Hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitishia kujitoa katika mchakato wa Katiba iwapo madai yake mbalimbali yasingesikilizwa  hadi Aprili 30, 2013.
 

Katika msimamo huo uliokuwa umetolewa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akijadili hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, chama hicho kilitaka:

Mosi, kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe hao wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na Mkutano wa Maendeleo ya Kata (WDC);

Pili, walitaka Serikali ilete mbele ya Bunge Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanya marekebisho ya vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuweka wazi namna wawakilishi wa taasisi hizo watakavyopatikana kutoka kila taasisi na idadi yao kwa kila taasisi;

Pia walitaka vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara, ili kuhakikisha kwamba wajumbe wa Zanzibar ambao hawatakuwa pungufu ya theluthi moja ya wajumbe wote watashiriki katika mijadala inayohusu mambo ya Muungano tu na siyo mambo ya Tanzania Bara yasiyokuwa ya Muungano;

Katika sheria hiyo, pia Chadema walitaka vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalumu la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni viondolewe  ili kumwondolea Rais uwezo wa kubadilisha uamuzi uliopitishwa na Bunge Maalumu;

Walitaka pia vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni ili kurekebisha hali ya sasa ambayo Katiba na Sheria za Uchaguzi hazitambui uwepo wa kura za maoni na utaratibu wa namna ya kuiratibu, kuisimamia na kuiendesha;

Hata hivyo, madai hayo hayakutekelezwa hadi ilipofika siku ya mwisho ya tishio, hali iliyokilazimu chama hicho kubadili msomamo kupitia maoni ya kambi hiyo kuhusu bajeti ya

Wizara ya Sheria na Katiba iliyowasilishwa na msemaji wake, Tundu Lissu.
 

“Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hayajatimizwa hadi tunatoa maoni haya. Mwenyekiti wa Tume (ya Katiba), Jaji Joseph Warioba amesema kwamba uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ambayo Tume inakiri ulivurugwa na mivutano ya kisiasa na kidini, hautarudiwa na Mabaraza hayo yataendelea,” anasema Lissu.

Hata hivyo,  kwa upande wa Serikali, Waziri Mkuu aliahidi  wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu  kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.

Ahadi hiyo ya Waziri Mkuu inaelezwa kuwa ndiyo imewalainisha Chadema hadi wakaacha kujitoa katika mchakato huo.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetafakari sana ahadi hii ya Waziri Mkuu. Pamoja na kwamba ni ahadi ya maneno tu, kama ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete kwamba marekebisho yote yanayohitajika katika Sheria hiyo yatakamilika hadi kufikia Novemba 2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona ni vyema iipe muda Serikali wa kuleta marekebisho tajwa ndani ya Mkutano huu wa Bunge la Bajeti,” anasema Lissu

Hata hivyo, Lissu anatoa sharti jipya: “Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, basi Chadema itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha Watanzania kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni”.
Lissu ambaye ni mwanasheria anaonya kwa kutumia mifano ya Kenya na Zimbabwe ambako rasimu za katiba zilikataliwa na uchaguzi zilizofuata zikafanyika chini ya Katiba za zamani, hali iliyozua machafuko.

“...Kenya, kwanza Serikali ya KANU chini ya Rais Daniel arap Moi, na baadaye Serikali ya NARC chini ya Rais Mwai Kibaki, zilijaribu kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya ya Kenya kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ambayo ilipopelekwa kwenye kura ya maoni mwaka 2005 ilikataliwa na wananchi wa Kenya...baadaye Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 2007 kwa mujibu wa Katiba ya zamani ya Kenya ya mwaka 1969. Matokeo ya uchaguzi huo chini ya Katiba ya zamani yaliingiza Kenya katika machafuko.

source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment