WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, May 11, 2013

Viongozi wa dini waitaka Serikali kukomesha vurugu za kidini


Majeneza yaliyowekwa miili ya marehemu wa waliokufa katika shambulio la bumu Jumapili iliyopita kwenye misa ya  uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Parokia ya Olasiti, Jimbo Kuu la Arusham, majeneza hayo yalikuwa ndani ya Kanisa hilo wakati wa misa ya kuwaombea kabla ya kuzikwa katika viwanjani hapo.  Picha na Filbert Rweyemamu 

Arusha. Watu watatu, waliofariki katika shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, mkoani Arusha wamezikwa jana na mamia ya watu, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kuliko kawaida na viongozi wa dini na Serikali kutoa kauli nzito.

Marehemu hao, ni  Regina Loning’o Laizer (45), James Gabriel(16) na  Patricia Joachim Assey(9) walizikwa katika eneo la kanisa hilo Katoliki, mazishi yaliyohudhuriwa na maaskofu wanane wa majimbo tofauti ya Kanisa Katoliki, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Askofu Alex Malasusa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na kisiasa.

Kauli za viongozi

Katika ibada hiyo ya viongozi mbalimbali wa kidini, walitoa salama zao akiwamo Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyeitaka Serikali kutumia msamiati wa mwenye macho haambiwi tazama na kukomesha mpasuko wa kidini aliosema unalitafuna taifa.
Askofu huyo alisema kuwa miongo mitatu sasa, Serikali imekaa kimya, ikishuhudia mafundisho na mihadhara ya kidini inayochochea na kuhamasisha uhasama kati ya Ukristo na Uislamu, bila kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.

“Matukio mbalimbali yanayoashiria uhasama wa kidini yanayotokea nchini. Kuna mihadhara, CD, DVD, machapisho na mafundisho yanayotishia maisha na usalama wa viongozi wa kanisa na waumini wao, ambayo yamefuatiwa na uchomomaji wa makanisa,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.

Alitaja mfano wa kongamano la Januari 15, mwaka juzi iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubillee jijini Dar es Salaam kuwa moja ya mikutano iliyojaribu kuchochea chuki ya kidini kati ya Waislamu na Wakristo kwa kudai kuwa Serikali ya Tanzania inaongozwa kwa mfumo Kikristo ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Askofu huyo alisema kwamba katika kongamano hilo, washiriki waliaminishwa kuwa Serikali inatoa fedha za ruzuku kujenga shule na taasisi za kanisa kutokana na kuwapo mkataba maalumu kati ya kanisa na Serikali, jambo ambalo siyo kweli.

“Kinachosikitisha zaidi ni kwamba Serikali haikukanusha madai na uchochezi huo, licha ya mambo hayo kufanyika na kusemwa hadharani kwa wahusika kuzunguka nchi nzima kueneza chuki na uchochezi huo,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.

Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dk Alex Malasusa alisema kuwa tukio la Arusha ni la kikatili na aibu kwa taifa akiwataka wenye dhamana ya ulinzi na usalama kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo akionya kuwa wasipofanya hivyo watahukumiwa kwa kosa la kukaa kimya mambo yakiharibika mikononi mwao.
“Wote wenye jukumu la kulinda na kuitunza amani waifanye kazi hiyo bila uoga. Wasipofanya hivyo iko siku watahukumiwa,” alisema Dk Malasusa

Mwakilishi wa Muungano wa Madhehebu ya Kikristo mkoani Arusha, Askofu Stanley Hotay aliwataka viongozi wa kisiasa kuepuka kutumia jukwaa la dini kutimiza malengo ya kisiasa, akionya kuwa makanisa hayana itikadi, bali waumini ndiyo wenye itikadi mbalimbali.

“Sote tuliomo ndani ya jahazi lazima tuwakemee na kuwadhibiti vichaa wanaojaribu kutoboa jahazi letu kwani tusipofanya hivyo maji yatajaa ndani, chombo kitazama na sote tutaangamia,” alisema Askofu Hotay.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu, ilioongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyetoa wito kwa waumini wa kanisa hilo, kutolipiza kisasi, akisema kuwa waliohusika  ni watu wasiofuata dini.

“Tusilipize uovu kwa uovu, yapaswa kushinda  uovu kwa wema…; Tuache kunyoosheana kidole kutokana na tukio hili,” alisema Kardinali Pengo.

Pengo ambaye hivi karibuni, alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa shambulio hilo halina uhusiano na masuala ya kidini hasa kutokana na taarifa za uhakika alizopewa akisema waliotekeleza shambulio hilo ni waovu wenye nia ya kuligawa taifa na kuliingiza katika migogoro ya kidini.
Viongozi wa kisiasa waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia  na wabunge kadhaa.

Salamu za Serikali
Akitoa salamu za Serikali katika ibada hiyo ya mazishi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa pole kwa tukio hilo akaeleza kuwa yoyote anayedhani kuua muumini mmoja, Askofu au Mufti ataua Ukristo au Uislamu,  hajui kuwa hiyo haitawezekana.

Pinda alisema Serikali imetoa Sh100 milioni ikiwa ni rambirambi zake akiongeza kuwa dini za Kikristo na Kiislamu  zina historia ndefu duniani.

“Itakuwa ni kujidanganya kuwa ukiua kiongozi wa dini leo utaifuta dini hiyo, kwani kwa kuamini hivyo hiyo ni ndoto,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu, alisema kwamba Serikali imeagiza vyombo vyote vya usalama nchini, vifanye kazi usiku na mchana kuhakikisha amani na utulivu unaendelezwa nchini.
Aliwataka Watanzania kuwa watulivu, hasa watakaposikia kamatakamata inaendelea na kueleza kuwa lengo la hatua hiyo ni kulinda amani ya nchi.

Ulinzi waimarishwa
Ulinzi uliimarishwa eneo lote kuzunguka kanisa hilo, barabara za kuingia Parokia hiyo na katikati ya Jiji la Arusha. Maofisa wa Polisi na Usalama kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam na Maofisa Usalama wa Taifa kutoka maeneo mbalimbali waliimarisha ulinzi.

Askari wenye silaha za moto na mabomu, waliranda juu ya kanisa hilo kwa kupeana zamu, huku baadhi wakiwa na miwani na kuona mbali. Maeneo mengine askari wanafunzi wa Chuo cha Polisi Moshi, walikuwa wameimarisha ulinzi na kuwapekua waliowatilia shaka

source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment