WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, May 24, 2013

Pembe ni kama kucha, zikikatwa zitaota!

Picture
Moja ya maeneo yaliyokubwa na vurugu Mtwara, Mei 2013
Uchunguzi wa wanazuoni umebaini kuwa mara nyingi binadamu anaweza kuficha tabia yake au kusema kile anachokifikilia ila ni agharabu kufanya hivyo hasa pale anaposhindwa kudhibiti hisia zake iwe ni furaha, msongo wa mawazo au hata gadhabu, Kauli ya mtu uonyesha taswira ya tabia ya mtu mwenyewe.

Hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye anaweza kushabikia maafa yaliyotokea Mtwara kwa kupoteza ndugu zetu pamoja na mali, ila Mwenye busara lazima ajiulize ni kwanini Watanzania wapenda amani wamefikia hatua ya kujikusanya kwa mamia kuhami kile ambacho wanafikiri ni haki yao na sasa wana dhulumiwa?

Sakata hili limetuma salamu vilevile kwa wanahabari, kitendo cha wanahabari kuwa miongoni mwa walengwa kutokana na kazia hiyo inatoa tafsiri ya wananchi kuanza kuchoshwa na wanataaluma wenye kucheza na hisia za watu kuwa siku zao nazo zinahesabika.

Naungana na Magazeti pendwa yote yaliyo onyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa nafasi kwenye kurasa zao za mbele kuweka tahariri ambazo zilikuwa na lengo la kuleta maelewano baina ya pande mbili za watawala na 
watawaliwa hususana wa Mtwara siku ya Ijumaa Mei 24, 2013. Ingawa nachelea kusema kauli hizo zimekuwa za upande mmoja tu.

Nachukuwa nafasi hii kuwahasa wanahabari kuwa Uzalendo halisi ni kuwa na nia ya dhati kutoa changamoto kwa serikali hasa wakati ambapo haijatimiza majukumu yake.

Nakumbuka maneno ya Muungwana mmoja aliye julikana kama Theodore Roosevelt pale alipo nukuliwa akisema “Maana ya Uzalendo ni kusimamia yale yote yenye masilahi ya nchi, lakini siyo kumuunga mkono rais au kiongozi yeyeto wa serikali.”

Watawala wanapaswa wakubaliane na hali hii kwa kuketi chini na kuitafutia ufumbuzi. Kwanini haya yanayotokea sasa na si wakati mwingine wowote tangu nchi hii ipate Uhuru wake zaidi ya miaka 50 iliyopita? Kila Mtanzania kwa sasa anashuhudia matukio yasiyo ya kawaida ambayo hatukuwahi kuyashuhudia wala kuyatarajia kutokea hapa kwetu.

Hali ni tofauti kwa viongozi wetu ambao kila uchweo hawaachi kubembeleza kwa wananchi kuwa kuuliza “hamuoni tunayofanya” na kuwa watu wanalaumu tu lakini hawatoi pongezi kwa “mazuri mengi waliofanya”. Imefika mahali watawala wanawashanga watawaliwa kama ambavyo watawaliwa wanavyo washanga watawala.

Tukio la Mtwara siyo la bahati mbaya, wala tusijidanganye kwa kusema limechochewa, na kuwapa wananchi majina kama ya wahuni au kufika mbali kwa kuwaita vibaka.

Tunahitaji muda wa kutafakari na kukubali kuwa watanzania wa sasa siyo wa miaka hiyo na wamepoteza imani na watawala ambao wemekwenda mbali hata kuthubutu kuwa fananisha na chura kwa kujiaminisha kuwa kelele zao kamwe haziwezi zuia bomba la gesi kwenda Dar.

Watawala wetu wamebakia kutumainia vitisho, dharau na matumizi ya nguvu. Wameshindwa kabisa kujenga hoja – kwa mfano kwenye hili suala la gesi.

Hawana ushawishi wa hoja na badala yake hata kauli zao wanazotoa zimejaa dharau (contempt) na matokeo yake watu nao wanawadharau! Wanafikiri vitisho na kejeli zinajibu hoja.

Najuwa wengi wataniita mchochezi, lakini jaribu kufikilia dharau ambayo imeonyeshwa waziwazi na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Mhongo, nahii siyo mara moja. Jumanne ya tarehe 21 Mei 2013 aliwafananisha Wanamtwara na chura.

Alhamisi tarehe 23, Mei 2013 katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani DW mchana  alinukuliwa akisema kwamba katika sakata hili wananchi wanadanganywa na kutumiwa kwani wao hawana uwezo wa kupiga hesabu ya faida au hasara ya usafirishwaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Kwa maneno machache anawaona wananchi wa Mtwara kama Mazuzu wasiyokuwa na uwezo wa kujifanyia maamuzi, kwa fikra zake kupiga hesabu ndogo kama hiyo ni lazima uwe ni Profesa.

Ni wazi tuna tatizo! Viongozi wetu wamekosa ushawishi (are out of touch) kabisa!

Napingana na hoja zinazosema kuwa watu wa Mtwara au watanzania wengine popote pale wanahitaji kuelimishwa. Viongozi ndio wanatakiwa warudi kwa wananchi ili wananchi wawafundishe ni nini cha kufanya.

Ni lini huyu Profesa alikutana na wananchi wa Mtwara, akaongea nao na kujiridhisha kuwa hawana huo uwezo anao uongelea? Kwanini huyu Profesa anarudia kebehi zile zile?

Watawala wetu wanaona zaidi hili la ‘Uchochezi, uhuni na kuwaita wana mtwara vibaka’ kuliko kiini hasa cha tatizo? Kwanini tusijifunze kutatua matatizo kwa kushughulika na kiini badala ya kungagana na Viashiria (symptoms) kila siku?

Inashindwa kuingia akilini pale viongozi wetu wanaposhindwa kwa makusudi kushughulikia tatizo linalojulikana wazi na kuanza kutafuta mchawi!

Amiri Jeshi wetu mkuu akiwa kwenye mkutano wa Dodoma huenda kwa kushauriwa vibaya alitaharuki na kunukuliwa akisema “atawasaka wachochezi popote walipo na hata kama wanapembe basi watazikata”.

Sina nia ya kupingana na kauli ya rais wangu bali namkumbusha kuwa pembe ni kama kucha ukizikata uwa zina tabia ya kuota hivyo utakuwa bado ujatatua tatizo.

Kauli ya Amiri Jeshi wetu mkuu ilifwatiwa na kupelekwa kwa askari wa JWTZ Mtwara.

Ufahamu wangu mdogo unanituma kujuwa matumizi ya vijana wetu wa JWTZ utumika wakati wa hali ya hatari au kulinda mipaka yetu, Ila siku za hivi karibuni tumeshuhudia matumizi ya jeshi hili katika mambo ya kisiasa.

Taarifa za awali zinadai zaidi ya wanajeshi 300 tayari wako Mtwara, ukiniuliza kufanya nini sina jibu la moja kwa moja!

Je! vikosi vya kutuliza ghasia vya polisi vimezidiwa nguvu na wananchi wasiyokuwa na silaha mpaka kuliingiza jeshi kufanya kazi za polisi!

Naomba ifahamike kuwa vijana wa JWTZ mafunzo yao siyo kwa ajiri ya kulinda amani maeneo ya raia ndiyo maana sijashanga shutuma ambazo tayari zimeanza kutolewa za uvunjwaji wa haki za binadamu dhidi yao.

Nakumbusha tu, Sudan ya Kusini ilizaliwa baada ya Sudan kudharau madai ya Muda Mrefu ya Sudan ya Kusini. Elimu na Hekima, huzaa Maelewano na Upendo na Ustawi wa Jamii yenye Amani ya Kweli. Elimu na Sheria visivyo na Hekima , huzaa viongozi Viziwi,Vibubu na Vipofu wa Fikra na matokeo yake hupoteza Amani, Wananchi wasio sikilizwa maoni yao, huona bora kuwa kama Sudan ya Kusini.

Suluhu ya jambo si matumizi ya nguvu na kubeza. Suluhu ya jambo ni kutumia hekima na busara. Suluhu ya jambo ni kusikiliza na kujua hoja zinazopelekea wananchi kupinga jambo hili. Suluhu ya jambo hili ni kufanya utafiti wa kina kujua kiini na kushughulikia tatizo hilo kikamilifu.

Bila kujua kiini, tatizo hili halitaisha wala kuondoka.

Mwisho, napenda kutoa pole kwa familia za wale waliofiwa, walioumia na kuharibiwa mali zao.

Tanzania imekuwa ni nchi ya amani na utulivu, sote tuna wajibu wa kulinda amani hii na kuidumisha.


---
Imenukuliwa kutoka Community.co.tz

No comments:

Post a Comment