WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, May 6, 2013

Profesa Baregu amgomea Slaa

  • Ni kuhusu tishio la kujitoa mchakato wa Katiba
  • Amwambia Dk Slaa nchi kwanza, CHADEMA baadaye
"If I'm told to choose between my party and my country, I will choose my country"

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Mwesiga Baregu, amekataa kata kata wito wa chama chake wa kumtaka ajitoe ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku yeye akiweka msimamo wake wazi kwamba Tanzania ni mhimu zaidi kwake kuliko chama chake hicho.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa Profesa Baregu, zinasema Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa, alimwita msomi huyo ambaye ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akimtaka ajitoe ndani ya Tume hiyo kwa sababu za kisiasa kwa madai kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeuteka mchakato huo.

Profesa Baregu anaelezwa kumjibu Dk Slaa kwa kutumia maneno ya Kiingereza, akisema: “If I told to choose between my country and my party (CHADEMA), I will choose my country,” akiwa na maana kwamba kama angetakiwa kuchagua kimoja kati ya nchi yake na chama chake cha CHADEMA, angechagua nchi yake kwanza.  

Akizungumza na Raia Mwema juzi Jumatatu jijini Dar es Salaam, Profesa Baregu amekiri kutoa msimamo huo Katibu Mkuu wake, Dk Slaa, pamoja na chama chake cha CHADEMA, akisema viongozi wenzake hao wanapaswa kujishauri mara mbili mbili kabla ya kuchukua uamuzi huo wa kujitoa ikizingatiwa kwamba tangu mwanzo chama hicho ndicho kilichoasisi suala zima la Tanzania kuwa na Katiba Mpya tofauti na hii ya sasa.

Itakumbukwa kwamba CHADEMA, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, wakati akiwasilisha hotuba mbadala ya kambi rasmi ya upinzani kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, ilitangaza kujitoa katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba, akitaja sababu kadhaa, zikiwamo za mchakato mzima huo kutekwa na CCM na lakini pia kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawana weledi wa kutosha kufanya kazi hiyo.

“Ni kweli, niliitwa na Katibu Mkuu (Dk Slaa), akaniambia Kamati Kuu ya chama chetu imeazimia kwamba chama hakiridhishwi na mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya, na kwa hiyo akaniambia chama kimeagiza nijitoe ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Akaniambia Kamati Kuu imeamua mambo mawili; kwanza kijitoe na pili, kikishakujitoa kianzishe kampeni ya nchi nzima kuwahamasisha wananchi nao wasusie mchakato huo,” anasema Profesa Baregu katika mahojiano maalum na Raia Mwema.

Anasema aliomba kujulishwa rasmi maamuzi hayo ya CC kwa maandishi, ili ajue atachukua uamuzi gani lakini hadi anafanya mahojiano na Raia Mwema hakuwa amepata majibu, huku akisema kwamba kwa maoni yake kama kweli yalikua ni mamuzi ya kikao, basi Kamati Kuu itakua ilifanya makosa kufikia uamuzi wa kujitoa bila kumshirikisha.

“Kwanini? Mimi tangu mwanzo kabisa sikuona kama suala hili la kuandikwa kwa Katiba mpya ni suala la mapambano kwa sababu kubwa moja kwamba CHADEMA ndiyo mwasisi wa mabadiliko haya ya Katiba. Mimi nilikuwa Meneja wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010 na nilishiriki kuandika Ilani ya uchaguzi, na hili la kutaka Katiba mpya lilikuwemo ndani ya Ilani yetu.

“Wakati ule wenzetu (CCM) waliweka msimamo wao wakisema hakuna sababu ya kuwa na Katiba mpya, iliyopo inatosha, lakini baadaye Serikali ikaona ipo haja ya kuwa na Katiba mpya inayokidhi mahitaji ya sasa na yajayo. Muswada ukapelekwa bungeni, wabunge wa upinzani wakasusa na kutoka nje. CHADEMA tukapewa fursa ya kwenda Ikulu kuonana na Rais kwa siku mbili mfululizo na karibu mapendekezo yetu yote yakakubaliwa.

“Muswada ukarudishwa bungeni upya, sheria ikafanyiwa marekebisho na kukubaliwa na wabunge wa kambi ya upinzani. Sasa leo hii, wabunge wale wale waliokubali, wanataka kukataa mchakato wa Katiba unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria waliyoipitisha wao wenyewe…kwa maoni yangu, hadi sasa sijaona matatizo ya mchakato, yawe ya maandishi au ya malengo ya kisheria. Kama ningekuwa nimeona tatizo, nisingekuwamo humu, ningejitoa. Tunatengeneza Katiba ya Watanzania wote, si Katiba ya chama fulani.

“Lakini pia, CHADEMA tulipokutana na Rais (Jakaya Kikwete), alitushauri na tukakubaliana naye, twende hatua kwa hatua. Itungwe sheria yenyewe kwanza, halafu iundwe Tume, baada ya hapo mambo mengine yaendelee kujadiliwa... tangu wakati huo hadi sasa nadhani sisi kama Tume tunafanya vizuri ikilinganishwa na wenzetu huko nje walioandika upya Katiba yao.

“Mchakato unaofuata sasa ni wa kuundwa kwa Bunge Maalumu la Katiba, hatua hii nayo wananchi wametakiwa wajiandae kutoa maoni yao juu ya muundo wa Bunge hilo. Ushauri wangu kwa CHADEMA, naomba chama chetu kikae mkao wa kujenga nchi yetu, na si mkao wa kuibomoa. Kama chama tukae na Watanzania kujenga Katiba yetu mpya kwa ajili ya Watanzania na Tanzania yetu hii kwa sababu fursa hii haitakuja tena karibuni labda baada ya miaka 50 ijayo…kuzira, kujitoa, nasema Watanzania hawatatuelewa.”

Akifafanua msimamo wake alioutoa kwa Dk Slaa kwamba kama angeambiwa achague kati ya nchi yake na chama chake, angechagua nchi kwanza, Profesa Barugu anasema: “Ndiyo, chama kinaundwa na kinapita, lakini Tanzania kama nchi itaendelea kuwepo daima. Ushauri wangu kwa CHADEMA ni kwamba kwa kuwa sisi tulishajiweka katika kusimamia mchakato huu wa kuwa na Katiba mpya, tusijiharibie kwa kuvuruga mchakato huu.”

Akizungumzia kauli ya Mbowe katika hotuba yake bungeni kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba haina watu weledi, Profesa Baregu anasema: “Sisemi katika hili CHADEMA imekurupuka, nasema ijishauri upya. Sijui ni weledi wa aina gani wanaousema, lakini naamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imejaa watu weledi watupu, imejaa watu waadilifu na wasiokuwa na matope yoyote…ndiyo maana tangu iundwe, hakuna Mtanzania yeyote ambaye ameiita Tume hii kwamba ni genge jingine la mafisadi.

“Sitaki kuwasemea wajumbe wenzangu juu ya weledi wao, lakini mimi mwenyewe tu mbali na elimu yangu, lakini pia nimetumika katika Tume ya Mo Ibrahim inayotathimini utawala bora wa marais wa Afrika kwa muhula mmoja. Mtu huwezi kuwa katika Tume hiyo kama huna weledi wa kutosha.”

Dk Slaa alipotafutwa jana Jumanne, ili pamoja na mambo mengine, aelezee hatua hiyo ya Profesa Baregu kukataa kujiuzulu akiweka wazi kwamba hadi sasa hajaona tatizo lolote kubwa ndani ya Tume hiyo linaloweza kumshawishi akubaliane na msimamo huo wa chama chake, na msisitizo wake huo wa kuweka maslahi ya nchi kwanza mbele kuliko ya chama chake, alisema: “Saa hizi niko kwenye kikao, pole baba!”

Moja ya eneo linalolalamikiwa na CHADEMA katika mchakato huo wa Mabadiliko ya Katiba hadi kutishia kujitoa katika mchakato mzima huo, ni pamoja na uundwaji wa mabaraza ya kata, ikielezwa kwamba wajumbe wengi wa mabaraza hayo ni makada na viongozi wa CCM, na hivyo kuhofu kuwa Katiba hiyo mpya inaweza kukibeba zaidi chama hicho Tawala.  

Hata hivyo, akitoa msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mbele ya waandishi wa vyombo mbalimbali nchini kuhusiana na mabaraza hayo ya Katiba ngazi ya kata, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alivitupia lawama baadhi ya vyama vya siasa na makundi ya dini kujifungamanisha na uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza hayo.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Warioba alisema Tume yake italazimika kuyaondoa mawazo yote hasi yanayokinzana na misingi ya kitaifa yaliyotolewa na wananchi na makundi mengine ya kijamii ili kuhakikisha kwamba nchi inakuwa na Katiba Mpya inayokidhi maslahi ya wananchi wenyewe na maslahi ya taifa pia.

source: Raia Mwema :  Mayage S. Mayage

No comments:

Post a Comment