WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, May 17, 2013

Shamsi Nahodha na kauli za viongozi


MAJUZI hapa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alitoa kauli yenye hekima na busara nyingi juu ya umuhimu wa viongozi kuchunga kauli zao.
Nahodha alialikwa kwenye kusanyiko la viongozi wa kidini lilioandaliwa na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kujadili, pamoja na mambo mengine, juu ya hali inayojitokeza sasa kwenye jamii yetu. Hali ya misuguano ya kidini.

Waziri Nahodha alisema kwamba yanayotamkwa na viongozi, hayaishii pale yanaposemwa tu. Hutafsiriwa kwa maana iliyokusudiwa au hata ile ambayo haikukusudiwa. Hivyo, umuhimu wa kuchunga kauli. Na hakika, hapa duniani kuna mifano ya viongozi, ambao kupitia kauli zao, ama zimewajenga au zimewabomoa kisiasa.

Siku zote, historia ni mwalimu mzuri. Ili tuweze kutafsiri na kuyaelewa yanayotokea sasa na kuyaelewa yatakayotokea kesho, tuna lazima ya kuangalia na kutafsiri kilichotokea jana. Na hii ni moja ya maana ya kusoma na kutafsiri alama za nyakati.

Katika hili la kauli, hapa kwetu Tanzania kuna kisa cha Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Mwaka 1985. Mzee John Malecela alikuwa bado na ujana wa kisiasa. John Malecela, katika uchaguzi ule wa mwaka 1985, ndiye alikuwa waziri pekee katika baraza la mawaziri lililovunjwa ambaye hakurudi bungeni. Alikataliwa na wapiga kura wake. Hakurudi bungeni. Kwanini?

Kwa mujibu wa maandiko ya wasomi watafiti, ma-Bwana Mvungi na Amos Mhina (Searching for a people M. P?), anguko la John Malecela lilitokana na kukosa uzoefu na mahusiano mazuri na wapiga kura katika ngazi za chini. Huyu alikuwa John Malecela ambaye ndugu yake Job Lusinde ndiye alikuwa mbunge aliyemtangulia jimbo la Dodoma Mjini. Malecela alibwagwa na Injinia asiye na uzoefu wa kisiasa, aliitwa Mazengo Yohana.

Hata hivyo, katika hili la mahusiano na watu, watafiti wale katika maandiko yao kwenye kitabu kiitwacho: Tanzania, Democracy In Transition, kwa mtazamo wangu, wameshindwa kubainisha sababu nyingine iliyochangia kuharakisha anguko la John Malecela wa wakati huo. Hili linahusiana pia na mahusiano kati ya John Malecela wa wakati huo na wapiga kura wake.

Na hapa inahusu kauli ya John Malecela wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi. Katikati ya kilio cha watumiaji wa njia ya reli ya kati (TRC) juu ya huduma mbaya za Shirika la Reli miaka ile ya 1980, Mzee huyu alipata kukaririwa akitamka kuwa hakukuwa na tatizo la huduma mbaya, na kwamba wenye kufikiri hivyo, “they can go to hell!.” Kwamba wanaoliona tatizo, wanaweza kwenda kuzimu.

Katika sanaa ya mawasiliano, tunaamini kuwa sentesi moja inayotamkwa na mwanasiasa, yaweza kumjenga au kumbomoa kabisa kisiasa. Kwa John Malecela, kauli yake ile ataishi asiisahau, maana, pamoja na kuwa tulikuwa katika mfumo wa chama kimoja, redio moja ya taifa na magazeti matatu, bado wananchi waliweza kufikisha shutuma zao kwa Malecela juu ya kauli yake ile.

Na kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliofuata wa mwaka 1985, ilikuwa ni kwa wapiga kura wa Dodoma Mjini kushindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la kisiasa la John Malecela. Walifanya hivyo kwa niaba ya Watanzania wengine, na hususan watumiaji wa reli ya kati. Malecela aliangushwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Hakupata ubunge na hivyo hakuweza kuwa Waziri.

Na hakika, Malecela alijifunza, na hata aliporudi tena kwenye ulingo wa kisiasa, John Malecela, hata hii leo, amekuwa ni makini sana katika kuchagua maneno anapowasiliana na umma.
Nahofia, kwa hali tunayokwenda nayo sasa, kuwa yaliyomkuta Mzee wetu John Malecela miaka zaidi ya 20 iliyopita, huenda yatakuja kuwafika baadhi ya wanasiasa wetu wa sasa, na wengine ni mawaziri wenye dhamana.

Yatakuja pia kuwafika baadhi ya wabunge, ambao, wakiwa bungeni, kauli zao zisizo makini, wanajisahau kuwa kuna wengi wenye kuwasikiliza.

Kwanini? Wapiga kura wa leo ni wenye uelewa zaidi kuliko wale wa 1985. Wapiga kura wa leo si tu wanakumbuka na kufuatilia matendo ya wabunge wao, na hususan ahadi walizotoa ambazo hazikutimizwa, bali wanakumbuka, na wataendelea kuzikumbuka pia, baadhi ya kauli za kejeli kwa wapiga kura kutoka kwa baadhi ya wabunge na mawaziri.

Na mara nyingi kuna kosa kubwa linalofanywa na wanaotafiti hali ya kisiasa, na hasa kuelekea uchaguzi mkuu. Wengi wa watafiti wanalenga zaidi katika kuchambua mienendo ya wagombea na kampeni zao. Watafiti hawa wamesahau kutafiti mienendo ya wapiga kura ambao kimsingi ndio wenye uchaguzi na maamuzi ya nani awe kiongozi wao.

Moja ya hulka za mpiga kura, ni kujaribu kukumbuka kauli za nyuma za wagombea. Hivyo, kama alivyobainisha Waziri Vuai Shamsi Nahodha kwamba upo umuhimu mkubwa kwa viongozi kuwa makini kwenye kauli zao! Nahitimisha.

source: Raia Mwema:  Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment