WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 9, 2013

Serikali itekeleze haraka Azimio la Bunge

 

Bunge jana kwa kauli moja lilitoa azimio la kuitaka Serikali na vyombo vyake vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya viashiria vya aina zote za uvunjifu wa amani unaojitokeza nchini.
 
Hatua hiyo ya Bunge inafuatia matukio kadhaa yaliyotokea katika siku za hivi karibuni na kutishia amani kwa misingi ya dini kama kushambuliwa na kuuawa kwa viongozi wa dini, kuchomwa moto nyumba za ibada na chokochoko za watu wachache zinazopandikiza chuki miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya dini.
 
Jumapili iliyopita mtu asiyejulikana alirusha bomu wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi ya Olasiti, jijini Arusha na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine zaidi ya 60. Hadi sasa watu waliokufa ni watatu baada ya majeruhi wawili kufariki hospitalini.
 
Tukio hilo la Arusha limelitikisa taifa, huku Serikali ikionekana kushindwa kupata jibu kuhusu lengo la watu waliofanya kitendo hicho cha kigaidi. Fadhaa hiyo ya Serikali inaeleweka, hasa tukitilia maanani kwamba wakati bomu hilo likilipuka, alikuwapo Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo akiwa na mwenyeji wake, Askofu Josephat Lebulu wa Jimbo Katoliki la Arusha.
 
Hivyo, Serikali ingekuwa katika wakati mgumu iwapo viongozi hao wa Kanisa Katoliki wangedhurika au kuuawa katika shambulio hilo. Pia taswira ya nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa ingechafuka. Taarifa zisizo rasmi zinasema Balozi huyo wa Vatican ndiye aliyekuwa mlengwa wa shambulio hilo, ingawa sio viongozi wa Serikali wala Kanisa Katoliki waliokuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
 
Ndio maana Bunge limetafakari hali hiyo na kuona umuhimu wa kutoa azimio la kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka. Pamoja na kwamba sio jukumu la Bunge kuiambia Serikali hatua za kuchukua, azimio lake lililotolewa jana mjini Dodoma halikuacha shaka yoyote kwamba Serikali lazima ianze utekelezaji wake haraka kadri inavyowezekana.
 
Bunge limetaka uchunguzi wa kina ufanyike na kuwatia nguvuni wahusika wote wa tukio hilo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili kuwapa wananchi matumaini ya kujumuika na kuabudu kwa uhuru pasipo kuwa na hofu ya usalama wao. Tunaambiwa kwamba tayari baadhi ya watu wamekamatwa.
 
Hata hivyo, tungependa kutoa tahadhari kwa Serikali kuhusu utekelezaji wa Azimio la Bunge, kwani kutokana na mazingira tuliyomo hivi sasa inawezekana kabisa Azimio la Bunge likapotoshwa makusudi na kupewa tafsiri ya kisiasa. Lazima Serikali na vyombo vya dola vitambue kwamba azimio hilo la Bunge halina maana ya kutangaza hali ya hatari wala kufuta Katiba ya nchi, kwa maana ya kuondoa haki za kiraia, kufuta shughuli za kisiasa na kuendesha nchi kwa amri na udikteta.
 
Kwa maana hiyo, shughuli za kisiasa lazima ziendelee bungeni na nje ya Bunge kwa vyama vya siasa kushindana kwa hoja na vyama vya upinzani vikiendeleza mikakati ya kukiondoa chama tawala madarakani. Hizo ndizo siasa za ushindani na Serikali lazima iikubali hali hiyo. Hata hivyo, vitendo vya kugawa wananchi kwa misingi ya dini, siasa na kabila vipigwe vita na kamwe visivumiliwe. Hayo ndio madhumuni ya Azimio la Bunge lililotolewa jana.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment