WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, June 28, 2013

Zuma ana siri nzito ya Mandela


 


Johannesburg. Rais Jacob Zuma anaaminika kuwa na siri nzito ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela baada ya kufuta safari ya kwenda Maputo, Msumbiji alikokuwa akahudhurie mkutano wa marais wa nchi wanachama wa Ushirikiano wa Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Zuma alivunja safari hiyo baada ya kumtembelea Mandela hospitalini na kumwona afya yake ikiwa imedhoofika, huku akiendelea kusaidiwa kupumua kwa mashine.

Hatua ya Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kuahirisha safari yake ya Maputo, tayari kumeibua sintofahamu zaidi kuhusu hatima ya afya ya Mandela.

Msemaji wa Rais Zuma, Mac Maharaj alisema kuendelea kuzorota kwa afya ya Mandela ni sababu ya kufutwa kwa safari hiyo.

Hata hivyo, Maharaj akizungumza kwa simu na gazeti hili jana alikataa katakata kuzungumzia undani wa afya ya Mandela, akasema jukumu hilo ni la familia yake na kwamba Ikulu inasaidia tu katika masuala ya jumla yanayohusu afya ya kiongozi huyo.

Familia ya Mandela
Wakati familia ya aliyekuwa mpigania amani na ubaguzi nchini Afrika Kusini, Nelson Mandela wakipeleka mashine ya kuchimbia kaburi katika makaburi ya kifamilia yaliyopo eneo la Qunu, kwa mara ya kwanza, kiongozi huyo amefumbua macho na kurejewa na fahamu.

Taarifa iliyotolewa jana jioni na Ikulu ya Afrika Kusini inasema Rais Zuma alimtembelea Mandela hospitalini mapema jana ambako alipewa taarifa kwamba anaendelea vizuri. “Bado yuko mahututi lakini imara,” ilisema taarifa ya Ikulu na kuongeza:

“Ana nafuu zaidi leo kuliko nilivyomwona jana (juzi) usiku. Timu ya madaktari inaendelea kumtibu.”
Hata hivyo taarifa hiyo ilimnukuu Rais Zuma akilalamikia kile alichosema kuwa ni vyombo vya habari kutoheshimu faragha ya mgonjwa.

Kauli hiyo ya Zuma ilitolewa muda mfupi tangu binti yake Mandela alipovikosoa vyombo vya habari vya nje ya Afrika Kusini, kwamba vinafanya kazi ya kuripoti tukio la ugonjwa wa Mandela katika misingi ya ubaguzi wa rangi.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha SABC jana mchana, Makaziwe alisema kitendo cha vyombo vya Magharibi kuweka kambi nje ya Hospitali ya Medi Clinic alikolazwa baba yake ni kushindwa kuheshimu desturi za Kiafrika.

Mashine yapelekwa makaburini
Mashine hiyo ilipelekwa juzi katika makaburi hayo ambapo ndipo wanapozikwa ndugu wa familia ya mzee Mandela. Hatua hiyo imekuja baada ya mkutano wa pili wa wanandugu wa karibu na Mandela uliofanyika juzi kwenye mji wa Qunu, kabla ya baadaye kufanya mkutano mwingine kati ya wanaukoo wa Mandela na maofisa wa Serikali waliokuwa wakizungumza mambo ya siri.

Mandela amelazwa katika Hospitali ya Moyo ya Medi-Clinic na hali yake ni ya kukatisha matumaini.
Mbali na hali yake hiyo, Shirika la Habari la Afrika Kusini la CBS jana liliripoti pia kuwa, ini na figo za Mandela zinafanya kazi chini ya asilimia 50.

Taarifa zaidi zinasema, kwa sasa maisha ya Nelson Mandela yapo mikononi mwa familia yake ambao ndio wanaoweza kusema aondolewe mashine ya kumsaidia kupumua ama la.

Miongoni mwao ni pamoja na Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala, Lindiwi Sisulu na kiongozi wa Kikabila Phathekile Holomisa, ambaye alisema kwa sasa kiongozi huyo wa zamani anateseka, hivyo kinachotakiwa ni uamuzi wa familia kuzima mashine ya kumsaidia kupumua.

“Kwa sasa Mandela hafurahii chochote kile, kinachoendelea katika ulimwengu wetu, sasa kwa nini familia isiamue tu kumwondolea hii mashine inayomsaidia kupumua?” alisema.

Tayari kanisa lililopo ndani ya kambi moja ya jeshi mjini Pretoria lilisema kwamba litaandaa mwili wa kiongozi huyo atakapofariki dunia, huku mtoto mkubwa wa Mandela, Makaziwe Mandela akisema lolote linaweza kutokea kuanzia sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Pretoria, Makaziwe alisema: “Hali aliyokuwa nayo baba, kwa kweli tunasubiri tu lolote kutokea.”

Naye mjukuu wake Ndileka Mandela alisema, kwamba kutokana na hali ya babu yake huyo wanasubiri lolote lile, wakati mjukuu wake mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Zoleka alisema kwamba hali ya babu yake hairidhishi na inaiweka familia katika wakati mgumu.

Wakazi wamzungumzia
Baadhi ya wakazi wa Johannesburg wanasema Zuma ana “siri nzito” kuhusu hatima ya afya ya Mandela (94), ambaye amelazwa katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo, Med Clinic mjini Pretoria ambako mamia ya watu wamekuwa wakifika kwa ajili ya kumwombea na kumtakia afya njema.

Hatua ya Rais Zuma pia ilisababisha kuongezeka idadi ya watu waliojitokeza kwenda kwenye makazi ya kiongozi huyo yaliyopo eneo la Houghton, Mtaa wa Laan 12 jijini Johannesburg tofauti na juzi, kiasi kwamba polisi walilazimika kufunga baadhi ya barabara kuzuia uingiaji huo isipokuwa kwa waandishi wa habari na wakazi wa eneo hilo pekee.

Mzee aliyejitambulisha kuwa rafiki wa karibu wa Mandela, Pathekile Holomisa, aliliambia gazeti hili kuwa: “Kweli tunapita katika kipindi kigumu, muda umefika kwa Madiba kuwa katika hali aliyonayo, kwa bahati mbaya sisi hatuna tunachoweza kufanya.”

“Tunaambiwa kwamba anasaidiwa na mashine kupumua, katika hatua hii Mungu pekee ndiye anayeweza kutuvusha, pengine Zuma ana siri ya afya yake,”alisema Holomisa ambaye alikuwa akilengwa na machozi.

Mkazi mwingine wa Johannesburg, Bono Boya aliliambia gazeti hili kuwa shauku waliyonayo wananchi wengi wa Afrika Kusini ni kumwona Mandela akitimiza umri wa miaka 95 ifikapo Julai 18 mwaka huu.

“Tumeambiwa anapumua kwa mashine, Serikali iziache mashine ziendelee kufanya kazi hadi mwezi ujao, tunatamani afikishe miaka 95 ili tusherehekee siku ya Mandela pamoja naye, baada ya hapo basi wazitoe maana ni kweli kwamba umri wake ni mkubwa sasa,”alisema Boya.

Mtanzania anayeishi Johannesburg, Almasi Maliki aliliambia gazeti hili kuwa: “Hapa South (Afrika Kusini) Mandela ni kama Mungu, ni mtu anayekubalika kwa Wazungu na Waswahili (Waafrika) kwa hiyo akifa tu, kila kitu hapa kitasimama.

Mashada, nyimbo zatawala
Polisi wa Afrika Kusini walilazimika kuondoa baadhi ya mashada ya maua yaliyotapakaa nje ya Hospitali ya Moyo ya Medi-Clinic.

Watu mbalimbali wamekuwa wakiweka mashada ya maua, maputo na kadi za kumtakia nafuu Madiba.
Pia nyimbo za kumwombea Mandela zilitawala katika hospitali hiyo iliyopo eneo la Pretoria, ambapo hata Zuma naye alijitokeza kuimba.

Miongoni mwa ujumbe uliokuwa umetawala katika maua hayo na kadi yalisomeka: “Tunakuombea kwa Mungu...tunakupenda...Mungu akubariki Mandela.”

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment