WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, June 15, 2013

Tume ya Warioba haikuchukua maoni ya wananchi?




WAKATI Tume ya Mabadiliko ya Katiba (maarufu Tume ya Warioba) inaundwa, wapo watu walioamini maoni yao yatachukuliwa na tume hiyo, hususan kama maoni hayo yatakuwa ni ya wengi.

Watu waliamini hivyo kwa sababu waliambiwa tume hiyo ni ya “kukusanya maoni” ilhali kiuhalisia tume hiyo ilikuwa ni ya ‘kusikiliza’ tu maoni lakini ikiwa haina mfumo wenye kuilazimisha tume kuchukua maoni ya wananchi wengi.

Kimsingi muda wote ambao wananchi waliutumia kutoa maoni, Tume ilikuwa inawasikiliza tu lakini yenyewe ikiwa ni uamuzi wa mwisho wa ‘maoni gani’ ni muhimu na yapi yanafaa kuingizwa kwenye Katiba.

Watu hawa wengi waliotoa maoni yao katika sehemu mbalimbali za nchi yetu walifanya hivyo wakiamini kuwa wanaweza kuishawishi tume kuchukua maoni yao. Watu hawa wengi walikwishasahu kuwa Tume ya Warioba kimsingi ni tume ya kusikiliza maoni tu na kutoa mapendekezo.

Kwa kawaida mapendekezo yanayotolewa na tume yanapaswa kuwa yale yenye kuakisi matakwa ya wengi. Tume ya Warioba hata hivyo, haikutakiwa kutoa mapendekezo yake kutokana na kuona matakwa ya wengi. Iliundwa kusikiliza tu maoni na kutoa mapendekezo yake bila kujali maoni ya wananchi yalikuwaje.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa tume ya maoni Tanzania kutokujali maoni ya wananchi wengi na badala yake kutoa mapendekezo kinyume cha maoni ya wananchi hao. Wengi wetu tunakumbuka tume ya Jaji Nyalali iliyopita na kuwauliza wananchi kama turudi kwenye mfumo wa vyama vingi au tuendelee kuwa katika chama kimoja.

Kwa wanaokumbuka tume ile baada ya kufanya kazi yake ilikuta kuwa wananchi waliotoa maoni asilimia 80 walitaka tuendelee kuwa chini ya chama kimoja huku asilimia 20 tu walitaka tuingie kwenye vyama vingi. Waliotaka chama kimoja wengi walitaka demokrasia yake iboreshwe na kusimamiwa vizuri zaidi. Hata hivyo, tume katika hekima yake na ‘ugenius’ wake (ikiwa imejaa wasomi mahiri wa sheria) ikaamua ‘kupendekeza’ kuwa Tanzania iingie kwenye mfumo wa vyama vingi.

Kimsingi tume ile ilienda kinyume kabisa cha matakwa ya wananchi. Mara nyingi umesikia watu wakinukuu Katiba na kusema kuwa “madaraka ya kutawala yatatoka kwa wananchi”. Ukisikiliza vizuri unaweza ukafikiria inasemwa “madaraka ya kutawala yatatoka kwa wananchi wasomi”.

Kilichotokea ni kuwa mfumo wa vyama vingi uliingizwa tena nchini si kwa sababu wananchi wengi waliutaka bali kwa sababu kundi la wasomi waliamini kuwa ndio njia pekee ya kuboresha demokrasia. Ulipofika uchaguzi wa 1995, CCM ikashinda kiti cha urais kwa asilimia 61.8; uchaguzi wa 2000 CCM ikashinda urais kwa asilimia 71.7; mwaka 2005 CCM ikashinda kwa asilimia 80.2 na mwaka 2010 CCM ikashinda 62.8.

Na ukiangalia kwenye viti vya ubunge bado CCM inashikilia karibu asilimia 80 hivi. Je, inawezekana matokeo haya yanaakisi matakwa ya wananchi ya kutaka nchi iwe kwenye chama kimoja? Je, kwa kupendekeza mfumo wa vyama vingi kinyume cha matakwa ya wananchi Tume ndio imewapa wananchi, yote yanayotokea leo katika siasa?

Kwamba pamoja na kutawala kwake vibaya, ufisadi na sera mbovu zilizoshindwa bado CCM inapendwa na wananchi wengi? Kama hili ni kweli na likaendelea kuwa kweli kwa chaguzi kadhaa zijazo siyo kwamba CCM itaendelea kushinda?

Fikiria uchaguzi mdogo ujao wiki hii. Ukisikiliza lugha za kisiasa na mwitikio wa wananchi unaweza ukaamini kuwa CCM haiwezi kushinda hata kura moja. Lakini kama tulivyoona sehemu mbalimbali nchini CCM bado ina wapenzi wengi sana. Je, wapo watakaoshangaa wakisikia kuwa baadhi ya viti vya udiwani vitakavyogombaniwa vikaendelea kuwa CCM au kunyang’anywa kutoka upinzani? Mimi siwezi kushangaa.

Ninachozungumzia hata hivyo ni hili la Tume ya Warioba kuweka mapendekezo kwenye rasimu yake ya Katiba huku ikiweka wazi kuwa ilichopendekeza siyo maoni ya wananchi bali maoni ya tume yenyewe. Kwa watu waliopata kumsikiliza Warioba wakati wa uzinduzi (sijui kwa nini watu wanazindua rasimu!) alizungumza na kutuonesha kuwa yeye na wenzake ndio walikuwa na maoni bora zaidi kuliko ya wananchi. Naomba nirejee baadhi ya kauli zake mbele ya Makamu wa Rais.

Kuhusu haki za binadamu wananchi walitaka haki hizi ziimarishwe na kusiwe na vikwazo visivyo vya lazima. Tume imependekeza mabadiliko katika baadhi ya haki za binadamu kwa madhumuni ya kuziimarisha. Moja ya mabadiliko hayo ni kuhusu uhuru wa mwananchi kushiriki shughuli za umma. Tume inapendekeza kwamba vikwazo vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.

Swali: Kuna mtu anajua ni asilimia ngapi ya wananchi walitaka wagombea huru waruhusiwe katika nafasi zote kama tume ilivyopendekeza?

Tume pia, inapendekeza haki mpya ziingizwe kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi, haki ya mtoto, haki za watu wenye ulemavu, haki za wanawake, haki za wazee, haki za makundi madogo katika jamii, haki ya elimu na kujifunza, haki ya kupata habari, haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari na kadhalika.

Swali: Tume inapata wapi madaraka ya “kutengeneza” haki mpya? Hili limenishangaza kwa sababu tume imejaa wasomi na watu ambao kwa kila kipimo wanapaswa kujua zaidi. Lakini katika ‘ugenius’ wao huo ndugu zetu wameamua kutengeneza ‘haki’ mpya? Je, ni wananchi waliotaka hizi ‘haki’ mpya ziingizwe? Na Katiba haiingizii haki ‘mpya’ inatakiwa ‘kutambua’ uwepo wa haki hizo. Kwa mfano, haki ya kuishi haitolewi na Katiba bali Katiba inatambua tu.

Mgombea wa nafasi ya Rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa.

Swali: Haya ndio matakwa ya wananchi au ndio maoni ya Tume? Kama ni maoni ya Tume wananchi wao walitaka nini?
Angalia na hili;

Kuhusu Bunge kutakuwa na wabunge wa aina mbili. Kutakuwa na wabunge wa kuchaguliwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye ulemavu. Kila Jimbo la Uchaguzi litakuwa na wabunge wawili mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.

Hoja: Nina uhakika kuna ‘magenius’ waliokaa kwenye Tume wakaona kuwa hili ni wazo bora kabisa! Sasa najiuliza, hivi ni kweli wananchi wengi waliotoa maoni walitaka kila jimbo ‘LAZIMA’ liwe na mbunge mwanamke na mwanamume? Hivi kuwa kwao watu wa jinsia moja ama tofauti, kunahakikishia vipi kuwa watakuwa ni wawakilishi wazuri wa wananchi? Au wanataka kuwa na takwimu tu zinazoonesha ‘gender parity’?

Kama lengo ni huo usawa wa kijinsia kwa nini waishie kwenye wabunge tu? Kila kata iwe na diwani mwanamke na mwanamume; kila kijiji kiwe na viongozi wanawake na wanaume; na kwenda mbali zaidi ‘magenius’ wetu wangeweka kuwa ni lazima Rais wa Muungano ateue mgombea mwenza wa jinsi tofauti – hii itaonesha usawa. Lakini wasiishie hapo; Majaji ni lazima wateuliwa kwa kuangalia jinsi zao, na teuzi nyingine zote!

Lakini pia itabidi tuhoji kwa nini ‘jinsi’ (ama jinsia wengi wanavyopenda kuita) ndio iwe kigezo kikubwa hivyo? Kwa nini wasiangalie na dini au rangi ya watu? Au hata makabila yao? Si lengo ni kuonesha usawa? Kwani usawa wa watu uko katika jinsia zao au katika utu wao?

Nina hoja nyingi sana ninapoangalia rasimu hii. Hitimisho langu ni rahisi kulielewa tu. Rasimu hii imetoka kwa Tume na haikutoka kwa wananchi. Sasa, nina uhakika kuna watu wanasema wanaponisoma – sasa kama ina mambo mazuri hivi ambayo tumekuwa tukiyalalamikia hata kama hayakutolewa na wananchi si ni bora kweli kweli na wote tuikubali rasimu hii? Kwamba, kama wasomi wameona mawazo yao ni mazuri sana na yanafaa kwa Taifa zima, kwa nini tusikubali tu?

Jibu langu ni hili katika swali: Kama Katiba inaakisi mawazo ya wajumbe wa tume na wasomi walioulizwa, je bado tunaweza kusema ni Katiba kutoka kwa wananchi? Je, ni kweli kama mawazo ya wananchi hayakuchukuliwa kwa kiwango kinachoonesha ukuu wao (supremacy of the people) bado Katiba itakuwa ni ya wananchi? Lakini swali kubwa ni hili; kama mfumo wa kuandika Katiba mpya ya wananchi hauwahakikishii wananchi hao kuwa mawazo yao yatazingatiwa, kweli wananchi wana sababu ya kukubali Katiba hiyo?

Jibu langu ni hapana. Sijui la kwako.
Kama kuna mengine katika rasimu hii nitaendelea na mada hii wiki ijayo, In shaa Allah

Source ;www.raiamwema.co.tz: Lula wa Ndali Mwananzela

No comments:

Post a Comment