WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, June 12, 2013

Rasimu yawagawa wabunge Zanzibar


Sanya Dodoma. Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa hivi kwa ajili ya kujadiliwa imeibua mgawanyiko baina ya wabunge wa Zanzibar.

Licha ya wengi wao awali kuonekana wakisimama kidete kudai Serikali tatu, sasa wameanza kurudi nyuma, Hawazitaki tena.

Sasa wameanza kuibua sababu na hoja za kuipinga, wakionyesha hofu ya Zanzibar kushindwa kujiendesha kiuchumi, endapo uamuzi wa Serikali tatu utapitishwa na kuwa sehemu ya Katiba.

Ajabu, eti sasa wanataka ziendelee mbili kama ilivyo sasa,  wakieleza kuwa kuanzishwa Serikali tatu ni kuuweka Muungano kitanzini.

Wanasema Muungano hauwezi kuendelea kuwa na uhai iwapo Tanzania bara itakuwa na Serikali yake.
Mmoja aliyeonyesha wasiwasi wake bila kumung’unya maneno ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Maua Daftari ambaye anasema mfumo huo ukipita itakuwa hasara kubwa kwa Wazanzibari.

Daftari ambaye amewahi kushika mara kadhaa nafasi za unaibu waziri katika Serikali ya Muungano, anasema ni vyema kwa Wazanzibari kupima faida na hasara kwanza kabla kuamua kuwa na Serikali Tatu.
“Kwa mtazamo wangu, kwa Zanzibar bado sana kusimama kwa miguu yake na wakati huo kuchangia katika Serikali ya Muungano….ingawa huenda kukawa na faida, lakini ninachokiona  kwa upande wangu, hasara ni kubwa zaidi,” anasema Daftari.

Anasema Wazanzibari wanapaswa kujiuliza, je, wamejiandaa kiasi gani kiuchumi, na akasema ni ukweli wa wazi kuwa Serikali ya Muungano inasaidia sana Zanzibar kama nchi.

“Tutake tusitake Serikali ya Muungano inatusaidia sana sisi Wazanzibari…ni vizuri tungepima zaidi, mfano sisi Wapemba tupo kila mahali huku bara, ukiangalia mahoteli, teksi nyingi ni za wapemba, na wanafanya biashara bila shida, hofu yangu ikija Serikali ya Tanzania Bara, tutasalimika? Hawatatwambia uzeni vitu vyenu muondoke?” anasema  na kuweka anaglizo: “Hayo ni mawazo yangu lakini.”

Anasema wasiwasi wake mkubwa ni kuwa baada ya kuwa na Serikali tatu, Wapemba nao wataibuka na kudai Serikali yao na kuwa sio tatu tena, bali itakuwa Serikali nne.

“Naona hofu kubwa mbele, naanza kuyakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa mawazo ya kugawanyika yataleta Uunguja na Upemba….ni vyema Wazanzibari tukatumia busara kubwa katika suala hili,” anaonya Daftari.

Akifafanua zaidi, mbunge huyo anasema Zanzibar haiwezi kufurukuta katika mfumo huo kwa kuwa haitaweza kuendesha Serikali yake na wakati huo huo ikamudu kuchangia Muungano, hasa kutokana na ukweli kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaitegemea Tanzania Bara.

Daftari anazibebesha lawama Serikali zote mbili –Muungano na Zanzibar kwa kushindwa kushughulikia kero za Muungano, akisema “kupuuza na kutokuzishughulikiwa mapema kunaweza kusababisha madhara makubwa yatakayosababisha amani na mshikamano wa Watanzania kubaki historia.

Naye Rajab Mbarouk Mohamed, Mbunge wa Ole (CUF) anasema kila anapoiangalia rasimu ya Katiba anaona urahisi na uwezekano wa kumalizika kwa Muungano kwa ukaribu zaidi.

Anasema ni vigumu kuwa na Serikali Tatu na Muungano kuendelea kuwa imara.

Anasema kuwepo na Serikali Tatu maana yake ni kuwa kila upande utaangalia maslahi ya upande wake, na Muungano kufuata baadaye, hali anayosema hiyo pekee ni dalili ya wazi ya kukosekana kwa Muungano imara kama uliopo.

Anaongeza kwamba kwa mtazamo wake Serikali ya Muungano imepewa madaraka makubwa, hali inayoweza kusababisha kero za Muungano kuendelea kuwapo, na kushauri kuwa zinatakiwa kutazamwa sasa.

“Zile kero za Muungano ndizo zinazotutafuna, hazijawahi kushughulikiwa, na haya ndio matunda yake.

“Hata ukiangalia hiyo rasimu imerudi kule kule, mambo yaliyotangazwa kusimamiwa na Muungano kwa faida ya pande mbili bado yanaweza kuzua sintofahamu,” anasema.

Anasema mambo kama umiliki wa rasilimali, umiliki wa fedha, wizara ya mambo ya nje na ukusanyaji wa kodi ni miongoni mwa vitu vitakavyoikwamisha Serikali ya Zanzibar kutokana na alichokiita wasiwasi kuwa Serikali hiyo haitakuwa na uwezo wa kiuchumi wa kuchangia katika Serikali Kuu.

Anasema wasiwasi wake mwingine ni ile nguvu itakayopewa kila Serikali, kuwa hatashangaa Zanzibar itakapoamua kuwa na pesa yenye sura ya viongozi wake.

Hata hivyo, anasema haamini huo ndio uamuzi wa mwisho wa wananchi wa Tanzania na kusema anasubiri hatua zinazofuata kuelekea kwenye Katiba mpya,  ambazo ndio zitatoa majibu sahihi.
Anasema Bunge la Katiba pamoja na Mabaraza yaliyoundwa ndiyo yenye jukumu la kuja na aina ya Katiba inayofaa.

Kwa upande wake mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya (CUF) anasema haoni wasiwasi wowote wa kuwepo na Serikali tatu kama ambavyo haoni hatari yoyote ya kuvunjika kwa Muungano.

Sanya anasema Serikali tatu ndio suluhisho la malalamiko ya wananchi wa pande zote mbili na kwamba zitaiwezesha Zanzibar kuwa yenye kuwanufaisha zaidi Wazanzibari.

Anasema wasiwasi wa wengi ni katika suala la ulinzi, uchumi na uwekezaji na kusema hoja hizo ni dhaifu na hazina msingi wowote.

Anasema mambo hayo yatashughulikiwa kwa uadilifu na kujali misingi ya utaifa pasipo kuwaathiri watu wa upande mwingine wa Muungano.

“Watu wamekuwa na mitazamo hasi kuhusu uimara wa uchumi wa Zanzibar. Hata mtoto hazaliwi na kutembea, huanza kwa kubebwa, kushikwa mkono na mwisho kutembea polepole mpaka anapoweza kutembea kwa kasi kama wengine,” anasema Sanya bila kufafanua.

Sanya anawataka wenye wasiwasi kutoa nafasi kwa mchakato kuendelea na sio kujaribu kuukwamisha.

source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment