WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, June 27, 2013

Ya Arusha na tuendako kama taifa
MWAKA 1976 nilikuwa mtoto wa miaka kumi tu. Hata hivyo, nilikuwa na uelewa wa kujua baadhi ya mambo, likiwemo tukio la kule Soweto, Afrika Kusini, yalipotokea mauaji makubwa, ya kutisha na ya kusikitisha ya watoto wengi wa shule. Ilikuwa ni Juni 16, 1976.

Mauaji yale yamepelekea Juni 16 kufanywa kuwa Siku ya Mtoto wa Afrika. Mwaka 1976 sikuweza kufikiri kuwa tukio kama lile la Soweto lingeweza kutokea katika nchi niliyozaliwa. Juzi hapa, siku moja kabla ya Juni 16, tumepokea habari ya mauaji ya kutisha kwenye viwanja vya Soweto, Arusha.

Kuna watoto wamekufa pia. Na picha za watoto waliojeruhiwa, tumeziona magazetini na kwenye runinga. Kama alivyotamka AGP Said Mwema, kilichotokea Arusha kinaashiria vitendo vya ugaidi. Hivyo basi, vilaaniwe na wote wenye mapenzi mema na nchi yetu.
Huu ni wakati pia wa kushikamana kama Watanzania, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na kiimani. Maana, hapa tulipo ni vigumu pia kujua hasa, kama taifa, adui wetu ni nani na anatoka wapi! Tuviachie na tuvipe ushirikiano vyombo vya mamlaka ili vifanye uchunguzi wa kina juu ya kilichotokea Arusha. Vifanye hivyo ili vije na ukweli wa kilichotokea, na hivyo kutupunguzia hofu ya ugaidi kwa raia wa nchi hii na hata wageni wa kutoka mataifa ya nje.

Nchi yetu hii imekuwa na sifa ya kuwa na amani na utulivu. Hakuna shaka yoyote kwamba sisi Watanzania kwa ujumla wetu, ni watu wenye kupenda amani. Tusikubali wachache wapandikize mbegu za chuki miongoni mwetu, na hata kufikia hatua ya kuvuruga amani yetu. Kutufanya tuishi kwa hofu na hata kuhofia kukusanyika kwa pamoja kwenye sherehe zetu za harusi na nyinginezo.

Wanadamu kwa kawaida, ni viumbe wenye kutegemeana. Nimepata kuandika kuhusu Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre aliyepata kusema: “Hell is the other people.” Kwamba jehanam ni wale wengine. Anataka pia tukubaliane kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.
Kwa hakika kabisa, tofauti ya mwanadamu na mnyama iko kwenye kufikiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndiyo maana ng’ombe anaweza kumpanda mama yake. Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.

Kwa hiyo, mwanadamu kwenye mambo ya msingi, hapaswi kabisa kuongozwa na hisia, ikiwamo ushabiki. Anapaswa kufikiri, na zaidi kufikiri kwa bidii. Vinginevyo, ni ukweli kuwa kijamii, mwanadamu anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye uhusiano wa kirafiki na kiadui na wenzake.

Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama ilivyo kwa wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha, mashamba, mapenzi na hata kivuli cha mti. Ndiyo, unaweza kabisa kuwakuta wanadamu wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa kivulini.

Wanaweza kugombana hadi akatokea mwendawazimu atakayekuja kuukata na huo mti wenyewe. Wanadamu hao watabaki wakitazamana juani. Mara nyingi, migogoro husababishwa na kugombania kisichotosha. Hivyo, lililo la msingi ni kutambua kuwa wanadamu tunategemeana.

Kwamba panapo kushindania jambo, mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza hekima na busara. Kwenye mgogoro wowote ule, mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya pekee katika kufikia muafaka, na si vurugu au mapigano.

Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta amani, panakosekana mazungumzo, basi, ina maana ya uwepo wa mazingira ya kuvunjika kwa amani. Wanadamu sisi tumekuwa wepesi sana wa kunyosheana vidole na hata kuhukumiana pasipo kudadisi ili kuujua ukweli.

Na hapa nawaletea leo kisa cha wanandoa waliokaa miaka mingi bila kupata mtoto. Wakaamua wamfuge paka nyumbani. Naye paka huyo wakampenda sana kama mtoto wa kumzaa. Paka naye aliwapenda sana bwana na bibi nyumbani.

Ikatokea mke yule akapata mimba na hata kuzaa salama mtoto. Ikawa kama miujiza. Furaha nyumbani ikaongezeka. Siku moja bwana na bibi walimwacha mtoto wao amelala kitandani. Nao wakaenda zao kuwasabahi jamaa na marafiki.

Walipokaribia nyumba yao wakati wakirudi nyumbani, wakashtuka sana. Walimwona paka wao nje ya mlango akiwa na kipande cha nyama mdomoni. Sura yake ilitapakaa damu pia. Wote wawili wakachukua muchi wa kutwangia nafaka.

Kwa hasira wakamtwanga paka yule kichwani. Alikufa papo hapo! Walipoingia chumbani, wakamkuta mtoto wao amelala salama kitandani. Kando kuna nyoka mkubwa aina ya chatu. Nyoka amekufa baada ya kujeruhiwa kwenye mapambano na paka. ‘Hell is the other people!’ Jehanam ni wale wengine. Lakini hata pepo yaweza pia kuwa ni ya wale wengine. Nahitimisha.

No comments:

Post a Comment