WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, June 20, 2013

KWA MWENDO HUU WA SIASA ZA TANZANIA ULIOJAA VURUGU WANANCHI TUNAJIFUNZA NINI? 

  • Ni kweli kwa sasa vyama vyetu vikuu CCM, CHADEMA na CUF vimeamua kuendelea kuona kuwa ni jambo la kawaida kwa damu ya wananchi wasio na hatia inaendelea kumwagika kwa sababu tu ya ushindani wa siasa?


  •  Je wanao kufa katika matukio haya ya vurugu ni viongozi au wananchi ambao hawana hatia? 

  • Kuna siri gani kubwa inayoendelea ndani ya vyama vya siasa kushabikia vurugu na sio amani


Kauli kama 


  • “CCM wamepanga njama ya kulipua bomu kwenye mkutano wa CHADEMA ili wananchi waogope kuhudhulia mikutano ya chadema”.  • “CHADEMA wamejilipua wenyewe ili kutafuta umaarufu na huruma ya wapiga kura pamoja na kuipaka matope serikali ya CCM pamoja na jeshi lake”.   • Nashindwa kuelewa je siasa ni sera au malumbano yanayoishia kuvunja amani?


Zitto Kabwe aliwahi kusema kuwa “sisi kama watu ambao tumepewa wajibi na wananchi wa kuitunza nchi hii na kuipeleka  pamoja tumejikuta tukiingia katika kutoa kauli, maneno na vitendo ambavyo ni “irresponsible” vinavyopelekea kugawanya nchi; na yanayotokea sasa ni matumizi ya nyufa hizo.”
 
Kwa matukio haya ambayo yameisha tokea na yanayoendelea kutokea; Leo hii ni Tanzania gani tunaijenga ni Tanzania yenye mshikamamo wa  kujenga utaifa, utanzania ambao utakuwepo siku zote hata kama watanzania wote waliopo sasa wata toweka.

Nafikir tatizo la viongozi wa siasa huwa hawaoni utashi wa kuleta mazungumzo yenye tija kwa Taifa bali wanachoona wao nini kifanyike ili kukifanya chama kishinde; lakini kama tutaendelea kuleta vurugu ambazo zinasababisha vurugu na watu kuuwawa mwisho wa siku hakutakuwa na chama na wananchi wa kuwaeleza hizi  propaganda za kisiasa kwani tutakapo ukaribisha ukimbizi ndani ya nchi yetu ndio utakuwa mwisho wa siasa hizi za amani na matokeo yake yatakuwa ukimbizi. Hebu tuwaangalie jirani zetu ambao nchi zao zilihusika katika vurugu na hatimaye vita za wenyewe kwa wenyewe wameishia wapi?

Ni chanzo cha vurugu na hatimaye umwagaji wa damu; mimi naona ni kauli za viongozi wa vyama pale ambapo wanaweka busara nyuma na masilahi binafsi mbele; unaweza kuwapima kwa kauli zao ndizo zinazoashiria vurugu inasikitisha sana.

Nakubaliana na kauli ambayo iliwahi kutolewa na mwanazuoni mmoja aliyesema kuwa “Siasa zilizo gubikwa na umamluki ndiyo zinazo yumbisha taifa kupitia propaganda ndani ya vyama vya siasa.”

Taifa hili kwa miaka 50 ya uhuru, tumeweza kuishi kama ndugu,  kwa amani na maelewano makubwa; kwa nini leo hali imebadilika ghafla je hii ndio demokrasia tunayoipenda ya vurugu?

 
Mwandishi wa raia mwema aliwahi kuandika kuwa “hakuna chombo au taasisi inayoweza kuitisha Serikali iliyowekwa madarakani na wananchi” kwa mtazamo wangu hata kama utakuwa huipendi kwa vile imewekwa na wananchi walio wengi basi inatakiwa iheshimiwe tukiamua kuleta vurugu tujue kuwa mwisho wa siku vurugu hizo zitamgusa kila mtu. Amani inatafutwa kwa muda mrefu, lakini fujo hazina muda. LAKINI Kwa upande mwingine vyombo vya ulinzi na usalama lazima vitumie busara zaidi katika kukabiri vurugu; ikiwezekana kwa vile wana mbinu zote za kulinda amani ikiwezekana waepuke umwagaji wa damu pasipo na ulazima wa kufanya hivyo;

Wananchi tujiulize je kama taifa wananchi tumaini letu ni lini dhidi ya viongozi wetu wa siasa? Jibu ni moja tu watupeleke kwenye nchi yenye neema na amani kwa watu wote bila kujali itikadi, hali yao kiuchumi, kisasa, kidini .

 
Lakini hivi sasa tunaona mbio za vyama vyetu vya siasa ni fikara ya kuwa madarakani, je madaraka haya yana siri gani mpaka wako tayari kupoteza maisha ya wapiga kura wao.

Niliwahi andika huko nyuma kuwa wanasiasasa tukiwaendekeza sana wanaweza kutufanya tusiendelee;tukumbuke kuwa maendeleo yetu kwanza yatatokana na sisi wenyewe, juhudi zetu na misimamo yetu;  tukiangalia kwa ujumla wanasiasa  wanpoteza muda mwingi katika propaganda na sio kutuelimisha ili tuweze kujua kwa undani matatizo na mahitaji yetu yanatokana na nini na tutaweza vipi kuyaondoa.

Wanasiasa wetu ndio wapiga majungu namba moja; aaa siasa zetu zimejaa majungu, chuki tusipoangalia sisi wananchi tutaendelea kuwa wajinga; tusifanye ujinga kuwa ni sehemu ya utamaduni wa siasa za Tanzania

Kwa takibrani miaka kumi sasa sioni dira katika siasa zetu zaidi ya vurugu; tufahamu kuwa Uongozi ni uwezo wa kuota dira na kuhamasisha maono na matarajio yaliyoko mbele na kuwafanya watu kusimamia na kuuboresha mfumo kwa moyo wao wote huku wakiamini na kushiriki kuyafikia matumaini yao ya kufikia maono yanayotolewa na uongozi kupitia mfumo uliowekwa.

Kiongozi tunaemtaka tunataka asimamie maono ya kule tunakotaka kwenda na hata kama ana maono yake basi kwa kipindi tunachompa dhamana awe na uwezo wa kuweka misingi ya kufuatilia maono ya kule tunakotaka kwenda.Je viongozi wa sasa wana mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani, kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kila mtu hasa wale wananchi wa vijiji ambao ndio wapiga kura namba moja?

 

Vurugu za Mtwara, Dar es salaam Zanzibar Arusha Mbeya Mwanza na kadhalika ni kipimo tosha kuwa bado tunahitaji wanasiasa wawajibikaji  na ambao wako tayari kutumia muda wao mwingi katika kuhubiri amani kwani bila amani kwa kweli hakuna kitu kinaitwa maendeleo, tunawaomba wajipange vizuri na kuja na sera mbadala ambazo zitawawezesha kujipanga vizuri kuliongoza taifa hili.

Wananchi tunatakiwa tuamke na tusiwape nafasi wanasiasa kutufanya sisi kuwa  daraja lao la wao kuweza kutimiza malengo yao bila sisi kujitambua kwa haraka; matokeo yake ni sisi ambao ndio tunapigwa, tunauwawa na tunaendelea kuwa masikini.

MUNGU IBARIKI TANZANIA


No comments:

Post a Comment