WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, June 24, 2013

Uchumi wetu na harusi za kufa mtu! ( MWANANCHI JUMAPILI)

8 ddacc

Na Maggid Mjengwa,

NAHOFIA, kuwa Watanzania tumejikita kwenye ndoto ya utajiri wa gesi na mafuta na kusahau kilimo chetu.  Hivyo, ni hatari kwa uchumi wetu.

Tunafikiria utajiri wa gesi na mafuta kana kwamba katika dunia hii ni sisi tu Watanzania ndio wenye utajiri wa akiba ya  gesi na mafuta. Hatujui, kuwa katika dunia hii kuna nchi zilizo akiba hizo za mafuta na gesi lakini bado uchumi wao hauwafanyi watu wao wawe ni wenye neema tu.  Nao wanafikiria pia kwenye vyanzo vingine vya kuinua uchumi wao ikiwamo kilimo.

Naam, Mwanafalsafa David Hume alipata kusema; “Mbegu  yako imekomaa leo, yangu itakomaa kesho. Ni jambo la manufaa kwetu sote kama  nitalima pamoja nawe leo, na wewe unisaidie kulima kesho. Siwezi kuwa na urafiki nawe

kama naona kuwa hujengi urafiki nami. Msimu utapita, nasi tusipoaminiana na kushirikiana, basi, sote tutakula hasara.” – David Hume.

 Kuna wakati nilisafiri kwenda Finland. Kule nilishangazwa sana kuona matrekta mengi yamepangana kwenye shamba moja. Nilimwuliza mwenyeji wangu; kulikoni?

Nilijibiwa kuwa huo ni utamaduni wa wakulima wa nchi ile. Kila mwaka huwa na mashindano ya kulima kwa matekta. Wakulima wa eneo moja  huenda kwenye shamba  la mwenzao na kufanya mashindano hayo; wanaangalia ni nani amewazidi wenzake katika kunyosha mistari, kulima kwa kasi, na kadhalika.

Ni katika nchi ile ya Finland nikaelewa, kuwa utamaduni huo ulianza tangu zama za kilimo cha kutumia farasi. Matrekta yalipoingia katika kilimo, ilitokea kwa mkulima mmoja akamwuliza mwenzake; “Je, trekta lako ni sawa na nguvu za farasi wangapi? Ni katika mazingira hayo, hata  kipimo cha nguvu za farasi kikaanza kutumika; horse power, ina maana ya nguvu ya farasi, inatumika hata leo katika kupima nguvu za mashine mbalimbali.

Nitazungumzia umuhimu wa mtaji wa kijamii ( social capital) na ari ya kiraia ( civil courage) ili kuweza kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kuinua uchumi wa nchi. Ili jamii na nchi kwa ujumla iendelee kiuchumi inahitaji kuwa na mtaji huu muhimu. Kukua kwa ushirikiano wa kijamii katika shughuli mbalimbali, iwe za huzuni au sherehe, ni mfano wa kuwapo kwa msingi mzuri wa mtaji wa kijamii.

Dhana hii ya mtaji wa kijamii na ari ya kiraia huenda ni  ngeni kwa baadhi yetu. Hata hivyo, ni kitu ambacho tunakishuhudia kila kukicha. Tunaona vikundi mbalimbali vya kijamii vikiongezeka. Leo tuna mifano ya jumuiya za kuzikana, tuna jumuiya za kukopeshana na nyingine nyingi.

Tuchukue mfano huu wa jumuiya zenye kushirikiana katika sherehe, mathalan, harusi. Siku hizi ukitembelea kumbi za starehe si ajabu ukakutana na watu walio katika kikao cha kamati ya maandalizi ya harusi.  Ni kamati hizi zenye kupanga mikakati ya kufanikisha harusi.  Wakati mwingine hupanga hata kile kinachoitwa “harusi ya kufa mtu!”.

Kamati ya maandalizi ya harusi itakutana hata mara mbili kwa mwezi. Na mara nyingi hukutana kwenye kumbi za starehe baada ya saa za kazi.  Kamati itapanga mikakati ya kufanikisha harusi huku wajumbe wengine wa kamati wakinywa bia. Na hata wakifanikisha harusi, watakutana tena kama kamati maalumu kwa “kuvunja” kamati. Watakula, watakunywa, watasaza. Fungu la kufanya hayo hupangwa pia kwenye bajeti ya harusi!

Wakati wenzetu kule Finland wanashindana katika shughuli za maendeleo, sisi, pamoja na umasikini wetu, bado  tunashindana kwenye kufanya harusi za anasa kubwa! Tunatumia mamilioni ya shilingi kufanya harusi za “kufa watu” wakati kuna watu nchi hii wanaokufa kwa umasikini. Wanakufa kwa vile barabara za kutoka vijijini kwao hadi ziliko hospitali za wilaya hazipitiki! Kuna watu wanakufa kwa kukosa fedha za kununulia madawa kwa magonjwa yao. Mjadala huu utaendelea...

No comments:

Post a Comment