WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, June 23, 2013

Haturuhusiwi kufanya mambo hivi tufanyavyo




WIKI hii nitakamilisha (kwa muda) mjadala unaohusu matukio yaliyoikumba sekta ya elimu hivi karibuni, lakini wakati wote najua kwamba masuala ya elimu siku zote yataibuka katika safu hii kwani hayaishi na kwa jinsi tunavyoyashughulikia yanaelekea yataendelea kujitokeza kwa ukali zaidi.

Ni kweli kwamba sakata la hivi karibuni la sehemu moja ya utawala kutangaza kwamba watoto wa shule wameshindwa vibaya na sehemu nyingine kuamua kubadilisha taratibu za kupima matokeo ili washinde ni dalili za ugonjwa na sio ugonjwa wenyewe.

Ugonjwa wetu ni mkubwa kuliko tunachokiona na tunachokizungumza kwa jazba na sauti kali, na huu ni ugonjwa ambao anayetaka kuufuatilia kwa makini ataugundua katika kila medani ya maisha yetu. Iwe ni elimu, au kilimo, au viwanda, au afya, au maendeleo vijijini, au hata michezo, tumekuwa ni watu wa kutafuta urahisi wa majibu katika hali ngumu.

Kwa kufanya mabadiliko katika utaratibu wa kupima matokeo watawala wetu wanataka tuamini (na wao nadhani wanaamini) kwamba elimu yetu haina tatizo, ni elimu bora kabisa, na kwa hiyo hatuna sababu ya kuhamanika wala kuchukua hatua zozote za dharura. Hawa ndio akina Pangloss niliowahi kuwasuta katika safu hii.

Sote tunajua, hata kama baadhi yetu wangependa kujifanya wamesahau, kwamba tafiti mbalimbali zimetuonyesha kwamba watoto wetu katika shule nyingi hawafundishwi (na hawajifunzi) kwa kiwango kinachotakiwa, na kwamba wengi wao wamekutwa wakiwa nyuma kwa miaka mitano au sita ya darasa walimokutwa.
Sasa tunashangaa nini tunapoambiwa kwamba watoto wa aina hiyo, wanapofika hatua ya kutahiniwa, wanafanya vibaya? Tungetakiwa tushangae kama tungeambiwa kwamba wamefaulu. Wanaoshangaa kwa haki ni wale wazazi wanaokwenda shuleni kuwaaambia walimu wa watoto wao kwamba haiwerzekani kwamba watoto wao wamepasi kwa sababu wao (wazazi) wanajua kwamba watoto hao hawajui kitu na hawawezi kufaulu.

Tumeambiwa mara kadhaa kwamba anayeficha ugonjwa ataumbuliwa na kilio, lakini tumeamua kuwa mabingwa wa kuficha magonjwa yetu, tena magonjwa ya hatari kama hili la ujinga. Kwa hatua za “fasta-fasta” zilizochukuliwa majuzi, hili la elimu ni kama limekwisha, tutalisahau hadi utakapotokea mlipuko mwingine. Na utakapotokea tutachukua hatua nyingine za “fasta-fasta” huku tukijua (au tukitakiwa kujua) kwamba “fasta-fasta” ya awali haikutusaidia.

Tumekuwa watu wa hivyo; hatuna mustakabali wa pamoja kwa sababu kila mmoja wetu anajijengea mustakabali wake, yeye na familia yake. Inaelekea sote tunaelewa umuhimu wa elimu bora kwa watoto wetu, na ndiyo maana kwamba tunawekeza fedha nyingi katika kuwasomesha katika shule tunazoziona kama shule bora, mara nyingi kwa sababu watoto wakienda huko wanafanywa kuzungumza kimombo kuliko wazazi wao, na kwetu hiyo ndiyo elimu!

Tatizo ni kwamba ni wachache wetu wanaoweza kumudu shule hizo za gharama kubwa, na watoto walio wengi wanaendelea kusoma katika shule ambazo siyo tu haziwafanyi wazungumze ung’eng’e bali hawana lolote wanalojifunza, hata kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kiwango cha msingi tu. Na hawa ndio Watanzania wa kesho!

Nilikwishakulisema hili, lakini nitalirejea, wakati hawa wazungumzaji wa ung’eng’e wasiojua kitu watakapofika madarakani wakichukua nafasi za wazazi wao waliowasomesha ung’eng’ewa kuwasaidia kuzidi kuiuza nchi, wenzao wasiosoma ung’eng’e wala kitu kingine chochote watawagomea, na kutatokea vita. Kutakuwa na matabaka yasiyovumilika na katika hali kama hiyo hapatakalika.

Ni kweli kwamba wengi wa watawala wanapochukua uamuzi wa kijinga kama huu wa kubadilisha vipimo vya mitihani wanawapeleka watoto wao kusoma katika shule ambazo wazazi wa kawaida hawazimudu. Kwa maana hiyo hawa ni wazazi wasio kuwa na uchungu na shule wanazoziamulia. Kwa nini wajali wakati watoto wao wanasoma kwingine?

Hebu tuambizane tena: hakuna jambo muhimu kwa watoto wetu kama elimu bora katika kuwafanya wawe binadamu bora na raia wema. Mifano inajionyesha yenyewe. Watoto wa matajiri na wakuu wa serikali na watoto wa masikini na ambao wazazi wao hawakuwa na vyeo serikalini wamejikuta wote ni sawa kwa sababu walisoma shule zinazofanana na walipata elimu inayofanana.

Huo ulikuwa ni wakati ambapo wazazi waliokuwa serikalini walifanya muamuzi wa wa kuzifanya shule za umma zitoe elimu iliyokuwa bora kwa kiasi kilichowezekana, na watoto wao walisoma katika shule hizo.

Huu ulikuwa ni wakati ambapo wazazi wenye uwezo, au vyeo serikalini, waliwaondoa watoto wao kutoka shule binafsi na kuwaingiza katika shule za umma kwa sababu walikuwa na imani na shule za umma kuliko shule binafsi.

Kwa jinsi hii watoto walio wengi wa Taifa hili walikuzwa katika mazingira ya udugu. Leo hii hili halipo tena, na huko tuendako, kama si kesho ni kesho kutwa, gharama zake zitakuwa kubwa mno.
Ningependa kutoa ushauri kwamba tuache mtindo wa kupaukia masuala, tuachane na mtindo wa kuendesha kila kitu kwa dharura. Kama ninavyosema kila mara, hakuna mahali pengine tunakokwenda, kwani hapa ni kwetu, tumefika, na tunatakiwa tujenge maskani yetu ya kudumu hapa.

Kama hiyo ni kweli, tunatakiwa tuketi chini kama Taifa la watu wenye akili, tutafakari suala la elimu kwa mapana na marefu, historia yetu katika medani hii; tuangalie tulipokosea ni wapi na nini tulitakiwa tufanye; tuwaangalie wenzetu waliofanikiwa na tujifunze kutoka kwao.

Jambo la kwanza la kuwekeza katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu katika medani ya elimu ni tafakuri pevu, na wala si fedha. Umakini, fedha zitahitajika, lakini jambo la kwanza, jambo la msingi, jambo la awali kabisa, ni fikra zitakazotuelekeza jinsi ya kuenenda na jinsi ya kuwekeza fedha zetu kwa busara.

Tukiishakuelewana ni nini tunataka kufanya, ndipo tutakapoweza kuangalia rasilimali kiasi gani tuwekeze katika elimu ya watoto wa Taifa hili. Tunaweza kukopa kwa niaba yao, na hawatakuwa na kinyongo wakija kujua kwamba madeni wanayotakiwa kuyalipa ni fedha zilizowapa elimu sawa na watoto wa Korea na Singapore.
Tunaweza kuzithamanisha rasilimali zetu na utajiri tunaoambiwa kwamba tunao, kama ni dhahabu, gesi, mafuta, misitu na utajiri mwingine na sehemu maridhawa ya fedha zinazotokana na rasilimali hizo ikawekezwa katika elimu ya watoto wetu.

Yapo mambo mengi ambayo tunaweza kufanya, mambo ambayo tunatakiwa kuyafanya, ili kulinusuru Taifa hili dhidi ya janga la ujinga. Jambo moja ambalo najua kwa hakika hatutakiwi kulifanya ni kuendelea jinsi tunavyofanya mambo yetu, hovyo hovyo.

No comments:

Post a Comment