WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, June 2, 2013

Tumetoka Mbali; Je, Unaijua Historia Ya Daladala?

4 e8c83

Ndugu zangu,
Jana nikiwa viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa niliweza pia kuongea na baadhi ya wasomi wa Chuo hicho wakati tukiangalia mpira.

Mmoja wao alikuwa Mwalimu Mgaya aliyeniambia kuwa anakwenda kuwa mwalimu wa historia.Hapo tukaingia kwenye mada ya Daladala. Nikamwuliza kama anaijua historia ya Daladala. Hapana, hajawahi kuisoma au kusikia mahali popote. Kwake yeye Daladala ni Daladala.

Basi, akashangaa sana nilipomsimulia, kuwa asili ya Daladala ni jina tulilolitohoa kutoka sarafu ya Marekani, yaani, Dola. Nakumbuka kwenye miaka ya 80 mwanzoni , na katikati ya shida kubwa ya usafiri Dar, nauli za usafiri wa vibasi vidogo vidogo ikaongezeka na kufikia shilingi tano kwa safari. Ndipo hapo tuliweza kumsikia konda akiita; " Kariakoo Dala ..dala..dala... dala!"

Maana, shilingi tano yetu iliyokuwa nzito kidogo hata kuishika na yenye pembe sita ilikuwa na thamani sawa na dola moja ya Marekani. Ndipo hapo, shilingi tano yetu ikabatizwa jina la ' Dala'.
Jana jioni niliongea kwa simu na ndugu yangu  Mrisho Mpoto, nikamwuuzia wazo, kuwa siku moja tukutane tulijenge wazo la kuwa na kitu kwa jamii  kitakachotufanya tuzungumzie tulikotoka kwa nia njema ya kukumbushana historia yetu. Jambo hilo lingeenda sambamba na uzinduzi wa Mpango wa Usafiri wa Mabasi yaendayo kwa Kasi jijini Dar.

Maana, kuna mengi ya kutafakari kuhusiana na uchumi na jamii yetu. Tujiulize; wakati wasafiri wa daladala enzi hizo walikuwa ni watu wa kipato cha chini na hata cha kati, je , wasafiri wa daladala wa leo ni watu wa aina gani?Je, anayepanda daladala leo anatazamwa vipi; ni mtu asiye na uwezo kifedha au anaweza kuwa ni mtu  anayeona kuliacha gari lake nyumbani na kupanda dala dala amefanya mawili; amebana matumizi na kuelekeza fedha zake kwingine na hata kutunza mazingira. Maana, magari mengi mijini yanachafua mazingira.Je, ni kwa nini uchumi wetu wakati huo ulikuwa na nguvu kutuwezesha kubatiza sarafu zetu kwa fedha za kigeni kama dala kwa shilingi tano. Wengine waliita gwala.

Tuliweza pia kuibatiza noti ya shilingi 20 kwa kuiita ' Paundi' ikiwa na maana, thamani ya paundi moja ya Uingereza wakati huo ilikuwa ni sawa na shilingi 20 za Tanzania.  Ni kwenye miaka ya 80.Je, rasilimali zetu ikiwamo gesi na mafuta vinaweza kuturudisha kwenda kuwa ' Taifa Kubwa' kama tulivyokuwa wakati fulani. Maana, nakumbuka nikiwa mdogo nilisikia redioni  taarifa ya habari ikisema kuwa  ' Tanzania imetoa msaada wa magunia ( Sikumbuki idadi) ya kunde na maharage kwa nchi ya India kutokana na mafuriko yaliyowakumba. Nilisikia pia Tanzania ikitoa msaada wa chakula kwa nchi ya Msumbiji na kwingineko zilizokumbwa na maafa.

Je, tunaweza kurudia kuwa ' Taifa Kubwa' kiuchumi kama tutaendelea kuruhusu karibu kila nchi kubwa kiuchumi kuwa na benki zao hapa kwetu? Maana siku hizi hapa kwetu kuna benki za Wahindi mpaka Wapakistani! Je, na sisi tuna mabenki kwao?

Na tafsiri ya benki hizo si ina maana  pia kuwa nchi hizo zimeamua kujenga ' Vihenge' vyao kwetu kuhifadhia wanavyovuna hapa kwetu na kusafirisha kwenda kula kwao.

Na tuendelee kujadili daladala na uchumi wetu...!
Picha hiyo juu niliilipiga mwaka 1988 pale Posta ya Zamani. Huo ulikuwa ni usafiri tulioutumia ennzi hizo, maarufu kama ' Chai- Maharage'. Ni moja ya picha zangu za zamani sana zilizo kwenye Maktaba yangu.
Maggid,
Iringa.
0754 678 252

No comments:

Post a Comment