WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, June 15, 2013

Katiba mpya na aibu yetu
MWAKA 1990, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa anastaafu uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), katika ukumbi wa Diamond Jubilee alitamka yafuatayo: "Wananchi wenye shida za kweli hutapatapa mno siku hizi kutafuta msaada,”

Akaendelea; “Na sasa tumefikia hali ya hovyo kabisa kwamba Rais wa nchi yetu analazimika kutatua matatizo madogo madogo katika sehemu mbalimbali za nchi, kusaidia raia mmoja mmoja. Hali hii ni hali ya aibu kwetu wote, na inadhihirisha tu jinsi vyombo vya serikali vinavyofanya kazi vibaya. Iko faida kubwa inayotokana na kazi anazofanya Rais wetu, lakini ni kupoteza muda na nguvu za Rais wetu anazozihitaji kutimiza majukumu yake maalumu ambayo ni magumu na yanadai muda wake wote."

Zaidi ya miaka 20 sasa imepita tangu Mwalimu alipotamka hayo ya aibu na hali imezidi kuwa ngumu. Hakuna ubishi kwamba uongozi duni umechangia wananchi “kutapatapa mno” kiasi cha kuelekea kuchanganyikiwa. Mwalimu mwenyewe kwa bahati mbaya ana sehemu ya mchango wake kwa kuwaacha madarakani watu wengi dhaifu kiuongozi.

Popote duniani, uongozi duni unajidhihirisha mara nyingi kwa viongozi kupenda waonekane wanachapa kazi kwa kushugulikia matatizo madogo. Kuna mifano mingi ya viongozi kuwa miungu-watu; kwamba wakikutana na wananchi kazi iwe moja tu, wapigiwe magoti na si kuhojiwa kuhusu mambo magumu.
Lakini haya matatizo yetu yaliyofikia kwenye sura ya aibu, si tu viongozi wa nchi wakulaumiwa, bali hata wa vyama vya upinzani na jamii kwa ujumla.

Kuna tatizo kubwa la watu kuwa na kumbukumbu fupi. Sijui ni wangapi wanakumbuka wakati Mwalimu Nyerere anachaguliwa kuiongoza nchi, ilijulikana wazi kiasi gani cha mshahara alichokuwa akipokea. Na ilipotokea vurugu za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye miaka ya 1960, ambao pamoja na mambo mengine walidai viongozi wa nchi wana mishahara mikubwa, Mwalimu alikiri na kupunguza mshahara wake.

Ukiondoa suala la itakidi yake ya kisoshalisti, naamini tuliweza kufahamu mshahara wa Mwalimu, si tu kutokana na uadilifu wake, bali pia alitambua athari za wananchi kujenga fikra kwamba Rais ana vyanzo vingi vya mapato.

Kutokana na msingi huo mzuri wa uwazi kwenye mshahara aliotuachia Mwalimu, cha ajabu, suala la mshahara wa Rais na mawaziri kwa muda mrefu sasa ni siri. Nimejitahidi kuwauliza waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini juu ya hili, majibu yao ni ya kuchanganya.

Viongozi wengi serikalini wanajibu mshahara, kwa mfano wa Rais si kitu, kwamba ana marupurupu mengi. Nimewauliza pia baadhi ya viongozi wa upinzani waliowahi kugombea urais nikiamini haiwezekani mtu kuwania nafasi yoyote bila kujua atalipwaje.

Cha ajabu, wote niliowahoji hawajui mshahara wa Rais hadi mmoja alithubutu kuniambia; “Jinsi mimi ninavyowashangaa viongozi wa serikali kushindwa kutaja mshahara wa Rais, basi na wao wananishangaa kutokana na nchi yetu tunavyoijua.”

Swali nililojiuliza ni je, hawa watu wanatania? Yaani mtu kweli unagombea nafasi ya uongozi wa nchi bila kufahamu utapokea mshahara kiasi gani? Hata katika kazi yoyote ile, haiwezekani mtu ukaambiwa tu usijali kuhusu mshahara, mambo mengine yote ni mazuri mno.

Mshahara una nafasi yake muhimu katika kujenga nidhamu ya kila siku. Matokeo ya kupuuza suala hili ni sawa na kukaribisha viongozi kula nchi kama "mchwa".

Unakuta mgombea wa urais anajua akifanikiwa tu kukamata uongozi basi ameula.

Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo, mgombea mmoja wa urais aliwahi kutamka maneno ambayo kwa sasa naona ni kama almasi kutoka kwenye ulingo wa siasa.

Alitamka: "Siingi kwenye harakati hizi kwa lengo la kujipatia utajiri. Mapato ya Rais hayawezi yakamtajirisha mtu na wala sina ndoto za kujipatia utajiri. Nilivyo navyo vinaniridhisha."

Hii kauli inatuambia kwamba raia wa Tanzania tunamwajiri kiongozi wa nchi na tunaelewa vema mazingira ya kazi zake. Hatupaswi kutegemea afanye mambo ya kukurupuka nje ya mapato yake ya kila mwezi.

Kama Rais hana uchungu na mshahara wake, ambao unaweza kutumika kwa mfano, kwa ajili ya kulipia ada za elimu ya wanafamilia, ndugu na jamaa, kama si kukaribisha ufujaji wa pesa, ni nini? Na isitoshe halipi hata kodi kama raia namba moja wa nchi.

Katika Marekani, imefikia Rais halipiwi kila kitu hovyo hovyo. Inabidi achangie sehemu ya gharama ya chakula kila mwezi nyumbani kwake. Ndio maana kuna usemi kwao "there is no such thing as a free lunch".

Haiwezekani kiongozi akawa tu anakula na familia yake na wapambe kwa pesa za walipa kodi. Naamini raia wa Tanzania wanapaswa sasa kuwa makini na maisha ya Rais wao. Nisingependa kusikia maneno ya kipuuzi kutoka kwa raia kama 'ooh Rais hata hapokei mshahara au mshahara kama anapokea basi umetulia tu benki.

Mara hapokei zaidi ya milioni 20 au anapokea milioni tatu. Kama ni milioni tatu, Waziri analipwa nini?' 

Vile vile, mwandishi mmoja wa habari, kutokana na maswali yangu kwake, alisema "mshahara wa mtu yeyote unapaswa kuwa siri", halafu tena "ukiandika mshahara wa Rais bila shaka utamchonganisha na wananchi wake."

Jambo la pili linalopaswa kutazamwa kutokana na kutia aibu kwa nchi inayojisifu kwa amani ni jinsi viongozi wanavyosumbua raia na misafara yao mikubwa kana kwamba kuna hatari ya kuuawa. Mbona wakati wa Nyerere hakukuwa na fujo kama sasa barabarani, pamoja na majukumu mazito yaliyomkabili ndani na nje ya nchi.
Kuna hadithi kwamba kipindi cha Nyerere, kuna gari la kawaida ambalo liligongana na gari la msafara kutokana na kinachoonekana kutokufahamu kuna kiongozi anapita. Sasa tunashuhudia usumbufu wa misafara mikubwa, hata kwa mke wa Rais, Spika wa Bunge na marais wastaafu.

Hivi kweli kama ni usalama, walinzi wachache makini hawatoshi kwenye foleni za mjini? Na sasa tunakutana mara nyingi na watu wanaoongozwa na pikipiki ambao hawajulikani kiasi cha swali kuulizwa bungeni kwamba ni nani hasa anapaswa kuongozwa kwa msafara?

Tumeanza pia kuona polisi wa usalama barabarani wakipoteza maisha wakiwa wanaongoza misafara ya viongozi. Hii yote ni aibu kwa taifa.

Nadhani wakati umefika kwa Watanzania kujifunza na kuwaeleza viongozi watarajiwa ambao hawajaonyesha kukerwa na mbwembwe za viongozi kwamba, tuige mfano wa Botswana.

Botswana kweli ni nchi ya amani kiasi cha mtu kuweza kushindwa kujua Rais ametembelea eneo fulani kama hospitali. Nieleze mfano, kuna hadithi ya daktari mmoja wa Kitanzania nchini Botswana, ambaye alikuwa anahangaika kuitambua sura ya Rais wa Botswana alipotembelea hospitali alikokuwa anafanya kazi na kisha huyo Rais kuamua kujitambulisha.

Tujiulize hii kweli inaweza kutokea hapa Tanzania? Nakumbuka ile hadithi ya Rais wa nchi moja ya jirani aliyetembelea hospitali ya wagonjwa wa akili. Mapema tu, akiwa anazungumza na mgonjwa mmojawapo, naye Rais aliulizwa kama ni yeye tu aliyesindikizwa na magari mengi hivyo na watu waliobeba silahi nyingi. Baada ya kujibiwa ndiyo, yule mgonjwa wa akili alitamka, basi wewe kesi yako ni nzito sana.    

La mwisho katika hili la amani, nilipata bahati ya kufika nchi ya Argentina mwaka juzi na kufurahishwa jinsi ambavyo inaruhusiwa kwa mtu yeyote kutembelea eneo fulani la Ikulu ya nchi hiyo, katika mji mkuu wa Buenos Aires, bila kutozwa fedha.

Sehemu hiyo ina picha nyingi za marais na maelezo mengi. Iko wazi hadi saa mbili usiku. Ni ruksa kupiga picha na matokeo yake ni kivutio cha utalii. Askari wapo wanaolinda bila bughudha. Nadhani hata Marekani kuna utaratibu fulani wa kutembelea sehemu ya Ikulu ya Washington DC.

Jambo kama hili katika Tanzania ya amani na utulivu ni kama ndoto. Hata kama wangetoza kiwango kidogo tu cha fedha, mtu yoyote kuingia ndani itakuwa shughuli nzito! Tafakari je, ni kweli hakuna picha nzuri sana za Mwalimu na wageni mbalimbali za kuwavutia wananchi na watalii?

Tungekuwa na umakini katika ubunifu, mapato hayo yangeweza kusaidia kutunza mandhari katika Ikulu au kusaidia kazi nyingine. Kweli walinzi wapo kwa ajili ya kuwatisha watu tu? Tujitahidi kadri tunavyoelekea kwenye Katiba Mpya, tuhakikishe mambo ya aibu tunayashugulikia kikamilifu.
 
Source: www.raiamwema.co.tz: Andrew Bomani

No comments:

Post a Comment