WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, June 9, 2013

Warioba: Serikali ya Muungano haitakopa fedha


,
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi 

Dar es Salaam: Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kama mfumo wa Serikali tatu utakubalika, Serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha.

Amesema hata katika suala la uwakilishi wa nchi Kimataifa, Rais wa Muungano ndiye atakuwa na jukumu hilo na siyo Rais wa Tanzania bara (Tanganyika) au Zanzibar na kwamba Serikali hiyo ndiyo itakuwa na nguvu na itategemewa sana na Serikali nyingine.

Tangu Tume hiyo ilipotoa rasimu ya Katiba, watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao, huku wakionyesha wasiwasi mkubwa juu ya uendeshwaji wa Serikali hizo, kwamba utakuwa wa gharama kubwa kuliko ilivyo sasa.

Katika mahojiano yake na waandishi waandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, Sunday Citizen na Mwanaspoti, Tido Mhando ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL na Theophil Makunga, Meneja wa Uendelezaji wa Biashara wa MCL, Jaji Warioba alitoa ufafanuzi juu ya suala hilo.

Swali: Gharama za uendeshaji wa Serikali hizi utakuwaje, huoni kama Rais wa Muungano atategemea zaidi fedha na msaada kutoka Tanganyika na Zanzibar?

Warioba: Katika Katiba ya sasa mapato ya Muungano yanatokana na vyanzo vitatu, Kodi ya Mapato (income tax), Ushuru wa Forodha (custom duty) pamoja na ushuru wa bidhaa (excise duty).
Kodi ya mapato ndiyo inatoa fedha nyingi sana na inafuatiwa na kodi ya ushuru wa bidhaa na ushuru wa forodha. Kutokana na hesabu tulizopiga, tumeona matumizi katika Serikali ya Muungano yapo katika sehemu mbili, moja ni yale ya Muungano na ya pili ni yale ya Tanganyika ambayo yanachukua fedha nyingi.
Mwaka 2010/2011 mapato ya kodi ya mapato yalikuwa Sh2 trilioni na mapato ya ushuru wa bidhaa yalikuwa Sh1trilioni na mapato ya ushuru wa forodha yalikuwa Sh600 bilioni.

Ni kwamba matumizi ya mambo ya Muungano yalikuwa chini ya Sh1trilioni, ndiyo maana tumechagua ushuru wa bidhaa, kwani tukipata fedha zile zitaweza kumaliza matumizi yote ya Serikali ya Muungano.
Hivyo basi kama tukiendelea na utaratibu huu wa Serikali tatu, ni wazi kwamba Serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha kwa kuwa itakuwa nazo za kutosha, Serikali zitakazokopa ni hizo mbili.
Tulikuwa tukijua wazi kuwa Serikali ya Muungano lazima iwe na chanzo cha uhakika cha fedha, na kwa utaratibu huu Serikali hizo tatu ndizo zitakazokubaliana jinsi ya kukusanya fedha hizo.

Swali: Rais yupi atakuwa na madaraka katika mfumo wa Serikali tatu?
Warioba: Mambo ya Muungano ni machache, lakini yana umuhimu wake, kuna uraia ambao tunatakiwa tuulinde uwe wa nchi moja na ikumbukwe kuwa nchi haiendeshwi na viongozi na taasisi pekee.
Tabia za raia inahusika sana kwani raia wakiwa pamoja hata hizo Serikali mbili haziwezi kwenda zikaanza kufanya mambo yao.

Tukichulia suala la Mambo ya Nje ambalo lina mambo mengi sana, sura ya nchi ipo kwenye Muungano na Rais huyu wa Muungano ndiye atakuwa akikutana na uongozi wa jumuiya nyingine na siyo marais wengine. Kama ni kuiwakilisha nchi, basi yeye ndiye atakuwa mwakilishi mkuu.

Nchi hizi mbili lazima zitegemee Serikali ya Muungano, kwa sababu huwezi kusema una Serikali ya Muungano halafu unakwenda Shirika la Chakula Umoja wa Mataifa (FAO) wanazungumzia Kilimo, halafu wewe unasema Serikali ya Muungano haina madaraka ya kuzungumzia jambo hilo.

Ukifanya hivyo utakuwa umejitenga na dunia. Serikali ya Muungano haitakuwa dhaifu, wanaosema hivyo watakuja kutegemea sana hii Serikali ya Muungano na Rais wa Muungano ndiye atakuwa anaunganisha nchi.
Swali: Kwa nini mlipendekeza Serikali tatu?

Warioba: Upande wa Zanzibar wapo waliotaka Serikali mbili, Serikali ya mkataba na wengine kutaka Serikali tatu ingawa hawakuwa wengi na wachache walitaka Serikali nne.
Kwa Tanzania bara wachache walitaka Serikali ya mkataba na wengi walitaka Serikali moja, mbili na wengine tatu.

Hawa watu wa Tanzania bara walitoa sababu mbalimbali, mfano waliotaka Serikali moja walisema kama tunataka kuendelea muungano ni lazima kuwe na Serikali moja, lakini jambo hilo lilikuwa gumu kulingana na hali halisi.

Waliokuwa wakitaka Serikali mbili walikuwa na sababu nzuri ila tatizo walisema kama zikiendelea Serikali mbili ni lazima kupunguzwe mambo ya Muungano na Zanzibar isiingiliwe katika masuala yake ya uchumi.
Pia tofauti haikuwa kubwa kati ya wale wanaotaka Serikali mbili na waliotaka Serikali ya mkataba.
Ukitaka Serikali ya mkataba ni lazima uvunje Muungano na uwe na Serikali mbili ambazo baadaye zitakaa na kuzungumza aina mpya ya ushirikiano.

Kwa njia hiyo kuvunja Muungano itakuwa rahisi, lakini kuuvunja Muungano kwa lengo la baadaye kukaa na kushirikiana itakuwa ngumu kwa sababu watakaokuwa huru wataleta masharti ambayo yanaweza kuwa magumu kwa wengine, hasara yake ni kwamba Muungano ungevunjika.
Tuliona Serikali mbili zinafaa kwa kuwa zingeleta uchumi wa pamoja sambamba na uchumi mkubwa kubeba uchumi mdogo.
Lakini katika hili Watanganyika walikuwa na madai ya kudai Tanganyika yao tangu mwaka 1991 na hata Zanzibar ilivyoingia katika Jumuiya ya Kimataifa ya nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993, malalamiko haya yaliibuka kwa Watanganyika na kufika hadi mahakamani ila baadaye hoja yao ikazimwa.
Lakini pia liliibuka suala la Zanzibar kuwa na bendera yao, wimbo wa taifa na nembo na hata Katiba yao inaeleza kuwa Zanzibar ni nchi na wanataka uhuru zaidi, hapo Watanganyika walianza kuhoji Tanganyika iko wapi.
Sisi tuliona Muungano utakuwepo kama kutakuwa na dhamira ya Muungano na ndiyo maana tulisisitiza tusiingilie haki za uraia kwa sababu watu wana nguvu ya kuweza kuufanya Muungano ukawa pamoja kuliko hata vyombo vya Serikali.
Watu wenyewe wakianza kubaguana hata kama Muungano una muundo mzuri kiasi gani hautadumu.
Serikali tatu zina changamoto yake na hii haitakuja kumaliza tatizo, tumeona Serikali mbili mvutano wake jinsi ulivyo kati ya Serikali ya Mapinduzi na Serikali ya Muungano, na sasa unaleta Serikali ya Tanganyika ambayo itakuwa na mambo yake.
Ukweli ni kwamba wasipoelewana hawa wawili, Zanzibar na Tanganyika, Muungano utakuwa na matatizo makubwa sana.
Hata kama kutakuwa na Serikali mbili au tatu, kama hakuna dhamira Muungano utavunjika tu, muundo siyo tatizo, kikubwa kinachotakiwa kutazamwa ni dhamira ya viongozi wa nchi mbili.
Tukisema tunavunja Muungano operesheni za sheria tulizonazo zingewatenganisha wananchi, sasa hivi tuna soko la pamoja na kama tungevunja Muungano tungewatenganisha wananchi.
Kuna sheria za ardhi ambazo siyo za muungano, wangapi kutoka bara walioko Zanzibar na Wazanzibari walioko bara wangejikuta wakimbizi na kushindwa kumiliki ardhi, pia tulitazama suala la biashara, matibabu na hata shule.
Tanzania bara mtu wa Zanzibar habaguliwi kwa jambo lolote, na wapo madiwani, wabunge, hivyo kuvunjika kwa Muungano kungeleta ubaguzi wa hali ya juu.

Katika hili la Muungano tuliangalia uzoefu wa nchi kama Ethiopia na Eritrea, Sudan Kusini na hata India na kubaini kuwa kutengana kutaleta ubaguzi kwani nchi hizo zilijikuta zikiingia katika matatizo baada ya kubaini kuwa wageni wanamiliki ardhi na mambo mengine mengi.
Serikali tatu ndiyo suluhisho la kudumisha Muungano kuliko Serikali moja au mbili. Katika kura ya maoni jambo la uwepo wa Serikali tatu linategemea uamuzi wa viongozi.
Wapo viongozi wanaotaka Serikali mbili, tatu na ile ya mkataba, sisi tumependekeza Serikali tatu na kama wakiikubali basi ni lazima wawashawishi wananchi kuwa Serikali hiyo ndiyo inafaa.
Katika hili tunataka mtazamo wa kitaifa, kama kila kundi likishikilia msimamo wake hatutafikia mwafaka hata kidogo. Makundi haya yana nguvu na ndiyo maana sisi tunataka wote washiriki na vyama vikubwa vishiriki na kushauriana ili kuona kama nchi tunaelekea wapi.
Bado gharama zitakuwa kubwa pamoja na jitihada tunazofanya za kuwa na Serikali na Bunge dogo, bado gharama zitakuwa kubwa.
Serikali ya Tanzania bara itabidi ichangie sana katika Muungano. Tuliamua hili kwa kuwa tuliamua kuulinda Muungano, lakini kuhusu gharama kutakuwa na njia nzuri za uchangiaji kutoka kila upande.
Swali: Wapo waliotaka ziwepo Serikali za majimbo, lakini katika rasimu hamkupendekeza uwepo wa Serikali ya aina hiyo, kwa nini?
Warioba: Kuigawa nchi katika majimbo kungekuwa na mvutano wa kidini kati ya Wakristu na Waislamu pamoja na mvutano wa Kanda.
Mfano katika Mkoa wa Shinyanga walitaka jimbo lao na wachague watu wao na mali iliyopo katika mikoa hiyo sehemu kubwa ibaki katika mikoa hiyo hiyo.
Sasa kila mtu akitaka hivyo wananchi wa Dar es Salaam ambako kuna Bandari na asilimia 60 ya mapato ya nchi yanatokana na uwepo wa bandari hiyo, wakitaka kisitoke kitu katika bandari hiyo hali itakuwaje, hata mkoani Lindi wapo waliotaka gesi ibaki katika mkoa huo tu.
Tuliona jambo hili lingeleta ukabila mkubwa na tuliona mikoa mingi kutakuwa na ugomvi, mfano mkoani Dodoma watu walitaka wazawa wa mkoa huo ndiyo wawe na haki ya kwanza kumiliki ardhi, baadaye ndiyo watazamwe watu wengine.
Mawazo yaliyotolewa yalikuwa mengi na kazi ya kuchagua wazo lipi liende na lipi libaki ilikuwa nzito, ila tunashukuru kwamba mambo mengi ya msingi tuliyoyapendekeza hayakupingwa.

Wananchi walitoa mawazo ya msingi na kubwa ni maadili, walisema maadili yameporomoka ndani ya jamii. Katika utawala na katika uongozi wetu na wengine waliona ni zaidi ya ufisadi na kutaka wanaohusika wapigwe risasi.
Ndiyo maana tumeingiza misingi ya taifa na kisha kutia tunu kwamba lazima tuwe na uzalendo, utu na uadilifu.
Tuliona hilo halitoshi na kuona haja ya kuweka maadili ya uongozi na kugusia maadili na miiko ya uongozi na kuweka chombo cha kusimamia hayo.
Swali: Kwa nini mlipendekeza kuwepo kwa mgombea binafsi?
Warioba: Hii ni haki ya msingi; suala la mgombea binafsi lilikuwepo miaka ya nyuma kwamba mtu ana haki na anaweza kujiunga na chama cha siasa na hata kama yuko kwenye chama cha siasa anaweza kutokubaliana na chama hicho.
Jambo hili lilikwenda hadi mahakamani na sasa hivi tumeliweka na tunafikiri matatizo haya yametokana zaidi na vyama vya siasa baada ya wanachama wenyewe kutoridhika jinsi mambo yanavyokwenda ndani ya vyama vyao, ikiwa ni pamoja na jinsi unavyofanyika uteuzi.
Tulibishana sana wakati wa kuchambua suala hil. Wapo waliotaka mgombea binafsi iruhusiwe udiwani tu, wengine walitaka ubunge tu, wengine walitaka iruhusiwe urais tu na wengine walitaka iruhusiwe ngazi zote. Ila tuliona bora tuliache na hali halisi ndiyo itaamua.
Hivi inawezekana mtu akagombea ubunge au urais bila kuwa na mtandao fulani, ni lazima awe na mtandao ili aweze kuwania nafasi hizo.
Katika hili sidhani kama wenye uwezo wa kifedha ndiyo watakuwa na fursa pekee ya kugombea nafasi hizo.
Hata uwe na fedha vipi kwa nafasi ya urais ni kazi bure, ndiyo maana tunasisitiza tuweke msingi mambo yaliyo katika Katiba kuhusu maadili.
Swali: Moja kati ya mapendekezo ya Tume yaliyoleta minong’ono ni kufutwa kwa nafasi ya wabunge wa viti maalumu, kwa nini mmefuta wabunge wa aina hii?
Warioba: Wananchi wengi walisema wabunge wa viti maalumu wanawakilisha wanawake, lakini hawajachaguliwa na wananchi na wengi wapo kwa ajili ya masilahi ya vyama vyao


Tukaona wawe na utaratibu wa kuchaguliwa na wananchi na tumesema kwamba hakuna mtu ambaye atakuwa kiongozi wa kuwakilisha kikundi kimoja.
Ndiyo maana tukasema tunashirikisha wanawake na wanaume katika vyombo vya uamuzi ili wanapokuwa wanatengeneza sera michango itoke katika pande zote, ila katika hilo uongozi unabaki kuwa wa jumuiya nzima.
Tutakapokuja kuzungumzia sheria ya uchaguzi, itaweka wazi kwamba chama kama kinataka kushinda, lazima kichukue wagombea wawili ambao wanakubalika katika vyama hivyo ili kutoshindwa na chama kingine.
Hili lilikuwa ni wazo jingine la kuwafanya wanawake kuwa na uwakilishi unaostahili na waonekane ni viongozi wa jamii.
Swali: Kwa nini mlipendekeza Jaji Mkuu ateuliwe na Rais, hamkuona haja ya kuwa na chombo kingine kwa ajili ya uteuzi wake?
Warioba: Jaji Mkuu ni mmoja katika nafasi yake na pia ni mtawala, hata ukitazama wanaotoa uamuzi katika Mahakama za mwanzo siyo watu wanaoteuliwa na Rais.
Jaji hafanyi uamuzi ni kiongozi kama alivyo Rais, katika nchi yoyote, lazima kuwe na mfumo ili yoyote anayeteuliwa lazima ateuliwe na mtu na hii kazi lazima apewe mkuu wa nchi na siyo kiongozi wa Serikali.
Kama mtu huyu (Jaji Mkuu) atafuata matakwa ya Rais, tukaona tuweke utaratibu kwamba majina ya watu wanaoweza kushika nafasi ya Jaji Mkuu yatatoka katika Tume ya Utumishi wa Mahakama na Rais akishateuua mtu huyo atapelekwa bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa.
Mkiwa na maadili ya kazi hata aliyekuteua akifanya kosa lazima utamweleza ukweli tu.
Swali: Kwa nini Rais hakuondolewa madaraka makubwa?
Warioba: Rais anafanya uteuzi katika vyombo vya juu, wengi waliokuwa wakiteuliwa na Rais tumewaondoa na sasa watateuliwa na Tume.
Hawa wa juu ni muhimu uteuzi wao ubaki mikononi mwa Rais, hata ukitazama mawaziri na naibu mawaziri ambao walikuwa wakiteuliwa na Rais tumeondoa hilo na sasa watapata idhini ya bunge.

Uingereza Waziri Mkuu anateua mawaziri kama wasaidizi wake na hahitaji kibali cha Bunge, lakini hapa kwetu hakuna jambo hilo na tumempunguzia madaraka makubwa.
Rais ni mtu anayechaguliwa na watu wote hivyo lazima apewe madaraka, kwa nini madaraka apewe mtu ambaye hajachaguliwa na wananchi.
Swali: Haiwezi kuwa na mvutano kama Rais akiendelea kuchagua watendaji wa Tume ya Uchaguzi?
Warioba: Tumependekeza Tume iwe huru siyo katika uteuzi tu bali kutazama jinsi inavyofanya kazi, ndiyo maana tukasema sifa za mtu kuingia katika Tume ile lazima ziwekwe kwenye Katiba.
Katika mchujo wa kwanza, tumesema mwanasiasa, wanaharakati na viongozi wa asasi za kiraia wasiingie.
Mchujo wa pili, watakaoomba sifa hizo lazima wapelekwe kwenye Kamati ya Uteuzi ambayo itakuwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri, Majaji Wakuu wa sehemu mbili, Spika wa Bunge, Maspika wa sehemu zote mbili na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, sasa utawaamini watu gani zaidi ya hao katika nchi.
Baada ya hatua hiyo kumalizika, majina yanakwenda kwa Rais kama watu waliopendekezwa na Kamati na Rais atawateua na baadaye kupelekwa kuthibitishwa na Bunge.
Kwa nini wanasema Rais anaweza kuwa na masilahi kuliko wabunge, kama ni hivyo basi tusipeleke kwa Rais wala Bunge.
Yalitolewa mapendekezo kwamba wanasiasa waingie katika Tume, tukaona hilo si sahihi kwasababu Tume hii inahitaji kuwa huru sana, kwa nini tuamini kuwa Bunge linajali masilahi ya wananchi zaidi kuliko Rais wakati wote wanachaguliwa na wananchi, tulitaka chombo ambacho ni huru na tulitazama urais kama taasisi.
Swali: Unafikiri uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 utafanyika tukiwa tumepata Katiba Mpya?
Warioba: Kuwa na Katiba Mpya kutalazimisha sheria fulani zibadilike, ila kwa sababu ya uchaguzi sheria ambayo ni muhimu ikafanyiwa mabadiliko kabla ya uchaguzi ni Sheria ya Uchaguzi.
Sisi tunaamini kama tukimaliza kazi yetu na Bunge maalumu la Katiba likapitisha na kukawa na kura ya maoni na dalili zikiwa nzuri. Tunaweza kufanya mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi kwa muda sahihi kabisa kwa kufanya uchaguzi.


Sheria ya Uchaguzi tuliyonayo ni ya mwaka 1985 ambayo ilifanyiwa marekebisho makubwa mwaka 1984 na mwaka 1985 uchaguzi ukafanyika vizuri kabisa.
Tunafikiri kati ya Januari 2014 na Oktoba 2015 haya mabadiliko yatakuwa yamefanyika katika vifungu vile na Tume ya Uchaguzi inaweza kufanyiwa marekebisho na wanaweza kufanya uchaguzi.
Swali: Unadhani Katiba ya Tanganyika itakuwa ya aina gani?
Warioba: Uundwaji wa Katiba ya Tanganyika hatuoni kama utakuwa na ugumu wowote kwa sababu uandikwaji wa Katiba ya Tanganyika hauhitaji maoni mapya ya wananchi.
Sehemu kubwa ya mawazo haya yaliyoleta na wananchi katika rasimu hii yametokana na maoni ya wananchi wa Tanganyika na siyo Zanzibar ambao wananchi wa huko walijikita zaidi katika suala la Muungano.
Kwa sasa tunarudi kwenye Mabaraza ya Katiba kuna mambo ambayo yatarekebishwa, hata ukichukua sehemu ya kwanza ya Katiba hii mfano miiko ya viongozi, malengo yake, haki za binadamu na misingi ya mihimili ya dola, inaweza kubadilishwa kidogo, ila eneo ambalo ni kubwa ni mfumo wa utawala ambao utahitaji mawazo zaidi.
Hata hivyo, baadhi ya hayo niliyosema mawazo yake ambayo yalitolewa na wananchi tumeyaacha kwa sababu ya kupendekeza Serikali tatu na jambo la utawala lipo katika Muungano.
Swali: Kwa nini mlipendekeza umri wa Rais uwe miaka 40 kama ilivyo sasa?
Wananchi walitaka mgombea urais awe na miaka 30, 35, 40, 45 na 50, hawa waliotaka umri uwe miaka 50 walisema ni vyema Rais akaingia Ikulu akiwa mtu mzima sana na kutawala miaka 10, ili akimaliza muda wake astaafu kabisa.
Tulipoanza kupitia maoni ya makundi, lipo kundi moja lililotaka mtu mwenye miaka 18 agombee katika ngazi zote.
Sisi tulitazama sababu zote na baadaye kutazama hali halisi ya nchi yetu na kisha kufanya utafiti kuona wenzetu wanafanya nini. Kuna nchi nyingi sana kama Afrika Kusini na Marekani zimefanya umri wa kugombea urais uwe miaka 35.
Pamoja na hayo hakuna nchi hata moja katika uchaguzi wa kidiplomasia iliyowahi kumchagua rais ambaye ana umri chini ya miaka 40.

Hiyo maana yake ni kutaka mtu anayeingia katika uongozi akiwa na uzoefu kwa sababu hii ni nafasi ya juu sana na ndiyo maana tukaacha umri huo maana siyo mzee wala siyo kijana.
Umri wa juu wengi walitaka mtu akifikisha miaka 60 asigimbee, wapo waliotaka mwisho wa umri wa kugombea uwe miaka 70, lakini katika hili tulitazama hali halisi kwamba watu wenye umri huo ni nadra kugombea licha ya kuwa wapo viongozi wanaoweza kufikia umri huo wakiwa bado wana uwezo mzuri.
Wengine walitoa mfano wa Mwalimu Julius Nyerere kwamba alitoka madarakani akiwa na umri wa miaka 63, lakini aliweza kufanya kazi kubwa na alikuwa na uwezo mzuri tu.
Tunajua vijana walikuwa wanataka sana umri ushushwe, lakini tulizingatia hayo, katika hili sidhani kama kuna rais ataweza kurudi tena kugombea.
Kuna marais ambao walitawala wakiwa chini ya miaka 35 lakini wengi waliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi, siyo demokrasia.
SWali: Kwa nini katika rasimu hii hamkugusia sana masuala ya ardhi, maliasili,rushwa na udini?
Hii nchi itakuwa ya demokrasia na itakayoongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na utawala wa sheria, kujitegemea na isiyokuwa na dini.
Liliibuka suala la Mahakama ya Kadhi tulizungumza sana na kufanya uchambuzi na kufikia uamuzi kwamba tatizo siyo kuwa na Mahakama ya Kadhi, tatizo ni kuingiza Mahakama hiyo katika Katiba.
Zipo nchi ambazo zilimeingiza Mahakama ya Kadhi katika katiba na zipo nchi ambazo hazijaingiza Mahakama hiyo katika Katiba lakini zina mahakama ya kadhi, na mojawapo ni Zanzibar.
Zanzibar ina mahakama ya kadhi na ipo kisheria, lakini haipo katika Katiba, jambo hilo lipo katika katiba yao kwamba Baraza la Wawakilishi lina madaraka ya kuanzisha mahakama za aina nyingine ambazo zitaendeshwa kufuatana na masharti ya chombo hicho, kwa msingi huo wakatunga sheria ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi.
Tukasema hili siyo suala la Muungano, kwa kuwa Zanzibar wana uzoefu huo tukaona tunaweza kulitumia hili hata hapa, baada ya kuendelea na mvutano huu ambao unaweza kugawa wananchi katika makundi ya Waislamu na Wakristu, hatujaliweka katika Katiba lakini tumetoa ushauri.
Suala la rushwa lilizungumzwa sana na ndiyo maana tumetia msingi wa maadili ambapo katika malengo tumeweka suala la rushwa kupigwa marufuku na tumemesisitiza maadili liwe jambo la msingi katika uongozi.

Swali: Ni mawazo gani mmeyachukua zaidi katika rasimu hii?
Warioba: Kuna maeneo ambayo mawazo yametoka kwa wananchi kwa kiwango kikubwa, mfano ni suala la dira (unataka Tanzania ya aina gani), suala la maadili (unataka maadili ya aina gani).
Wasomi na viongozi walijikita zaidi kwenye madaraka na haki za binadamu, hayo yote ni mazuri, lakini ni lazima kuwe na msingi na hilo ndiyo tunategemea kupata kwenye Mabaraza ya Katiba ambayo yamewakutanisha watu wa kada mbalimbali.
Wananchi watasema wanataka utawala uweje kwenye kijiji, kata, halmashauri.
Swali: Mchakato wa Mabaraza ya Katiba utawazuiaje watu wa kada mbalimbali kutaka maoni yao ndiyo yapewe kipaumbele kuliko ya wananchi?
Warioba: Wakati wa kukusanya maoni ya wananchi tulitaka wananchi wasiingiliwe wala kulishwa maneno ya kusema na jambo hilo lilikuwa likitokea katika maeneo kadhaa, mfano ni kuchaguliwa kwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya ya kutaka uwepo wa Mahakama ya Kadhi.
Watu wa Kahama walikuwa wakizungumzia kilimo cha pamba, shule za kata, masuala ya ufugaji, uvuvi kulikuwa hakuna masuala ya vyama na walikuwa wakizungumzia mambo yao tu.
Hata katika maoni ya wabunge, wengi walikuwa na imani na Bunge, lakini hawakuwa na imani kabisa na wabunge na hilo lilitokea kwa kiwango kikubwa na wengi walikuwa na mambo.
Tuliona tofauti tulivyokutana na wananchi na makundi, kutoka kwa wananchi tuliweza kupata mawazo ya kila aina lakini katika makundi, mengi yalikuwa yakija na mambo yanayowahusu wao tu, vyama vya siasa vilizungumzia sana mambo ya utawala, lakini vitu vingine vya msingi hawakuvisema.
Kutokana na hilo ndiyo maana tuliamua kusisitiza suala la maadili kwa kutoa dira mpya.
Swali: Tume zimeundwa nyingi ikiwemo hii ya Mabadiliko ya Katiba, je, wewe unataka ukumbukwe kwa lipi?
Warioba: Nimelitumikia taifa hili katika mambo mengi sana, kuna mambo unaweza kufanya na kuamini kuwa umelisaidia taifa.

Mimi niliwahi kufanya mambo mengi mojawapo likiwa ni suala la rushwa licha ya kuwa hatukupata mafaniko kwani wengi walikuwa hawaamini kama Tanzania kuna rushwa.
Ukiacha misingi ambayo tunaiweka na kuikazania, ila katika hili la Katiba kama tukiweka kitu ambacho kitaufanya Muungano ukaendelea na kuimarika, hilo ndilo nataka nikumbukwe nalo lakini kama Muungano ukivunjika hilo litaniuzunisha sana.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment