WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, June 26, 2013

Neno La Leo; Kwenye Msafara Wa Gesi Na Mafuta Ya Taa Yamo...!

9 73f50
Ndugu zangu,
Nimepata kuandika, kuwa ni heri kufa na kuacha fikra zinazoishi kuliko kuishi bila kufikiri. Na hakuna njaa mbaya kwenye dunia hii kama njaa ya akili. Kwa mwanadamu, ukiwa na shibe ya akili unaweza kumaliza njaa ya tumbo.
Ninachoandika hapa kinakutaka msomaji sio tu ufikiri, bali ufikiri kwa bidii. Kwenye hoja ya  gesi ya Mtwara na Lindi ambayo kimsingi ni gesi ya Watanzania nauona mkanganyiko wa fikra.
Tulipo sasa ni sawa na mwili uliohangaika kubeba mzigo mkubwa, na kusafiri nao umbali mrefu. Mzigo uko begani. Maungo ya
mwili yamechoka sana. Safari imekaribia mwisho. Mzigo ukifika sokoni utauzwa kwa shilingi elfu mbili tu. Kitakachopatikana kitakuwa ni faida ya mwili mzima.
Ghafla kichwa kinadai mzigo ubebwe kichwani, na si begani. Na faida itakayopatikana sokoni iwe ni ya kichwa tu. Mikono na mabega imegoma kuinua mzigo kuufikisha kichwani. Kichwa kinasema kiko tayari kumlipa mpagazi atakayesaidia kuufikisha mzigo kichwani.

Gharama ya kumlipa mpagazi ni shilingi mia tano tu. Hivyo, kazi yote iliyofanya mwili kuufikisha mzigo mpaka hatua hii ya safari ni ya bure tu. Kwanza mwili ulichoka, maungo yakalegea. Lakini ghafla, mwili umeanza kuchemka, umekuwa mgumu. Naam, mwili umegoma. Unakataa mzigo usifike sokoni.

Je, kichwa kifanye nini?

Jibu, hakuna jinsi. Kichwa kina lazima ya kukaa chini na kufanya mazungumzo na mwili. Kuna lazima ya kupatikana muafaka, kwa mazungumzo. Hasara ya kichwa na mwili kuingia kwenye mgogoro ni hasara ya wote; kichwa na mwili.

Ndugu zangu,
Kuna ishara mbaya naziona mbele yetu. Maana,  hili la gesi ni jambo kubwa na laweza kuwa la hatari pia. Kwenye msafara huu wa hoja ya gesi nayaona mafuta ya taa . Kuna miongoni mwetu, wawe wanasiasa, wanaharakati na hata viongozi wa dini, kwao ya Mtwara na gesi ni ‘ Mtaji katika harakati zao’.
Hata wale Wabunge waliokuwa wakitetea ongezeko la posho zao bungeni nao tumewasikia wakiwashawishi Watanzania wa Mtwara kujitenga na kuunda taifa lao. Kama kweli walikuwa na uchungu na wananchi wa Mtwara na Lindi kwanini hawakugoma kuchukua ongezeko la posho zao bungeni?
Ndugu zangu,
Hii ni nchi yetu. Tunajivunia Tanzania yetu. Kamwe tusizichekee fikra za kihaini za kutaka Watanzania wenzetu wajitenge kutoka kwenye nchi yetu tuliyorithi kutoka kwa mababu zetu. Maana, hatari ya kuzichekea fikra kama hizo ni kupelekea nchi yetu kumegeka vipande vipande.
Kuna haja ya haraka kwa Serikali kutoa elimu kwa umma na ya msingi  juu ya hoja hii ya gesi. Vinginevyo itatoa nafasi kwa wachache wenye dhamira ya kupotosha umma wakaendelea kuifanya kazi hiyo.

Chukulia mfano wa mwanasiasa kijana niliyemsikia kwenye taarifa ya habari ya Star Tv  akitamka; kuwa kama gesi ya Mtwara ikichimbwa na kuuzwa yote, Watanzania milioni 45 , kila mmoja atakuwa akikaa tu, na mwisho wa mwezi analipwa mshahara kwa miaka 200!

Lakini mwanasiasa yule kijana alishindwa kuwaambia Watanzania wangelipwa kiasi gani kwa mwezi. Huu ni upotoshaji mkubwa na wa hatari na ndio maana ya kuhitajika jitihada za makusudi za kutoa elimu juu ya suala hili la gesi.

Hoja ya msingi juu ya gesi ya Watanzania iliyogunduliwa Mtwara na Lindi ni kwenye usimamizi na mgawanyo wa faida itakayopatikana kutokana na rasilimali hiyo ili iwanufaishe Watanzania wote, wakiwemo wana Mtwara na Lindi.
Kuna hoja za msingi pia juu ya mikataba inayoingiwa baina ya wawekezaji na nchi yetu, kama ina maslahi kwa nchi yetu na watu wake au la.

Naam, kwenye msafara huu wa hoja ya gesi kuna mafuta ya taa pia.

Tukiyadharau, yana uwezo wa kusababisha mlipuko mkubwa utakaoangamiza nchi yetu. Tumeshaziona ishara.
Ni   Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,

No comments:

Post a Comment