WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, June 3, 2013

Kuwa na Bunge kama hili, bora tuishi na ombwe


 
 MCL
Na Ndyesu Florian 


Kwa hakika sielewi ni mdudu gani huyu ambaye atakuwa amewaingilia  kiasi cha kuwasumbua vichwani wawakilishi wetu hawa wa wananchi kama maana ya wabunge.
Kwa baadhi ya wabunge hasa wale ambao siku zote ni makini, wanaotimiza wajibu wao ipasavyo, naomba mnivumilie niseme.
Siku zote nimekuwa nikijiuliza na kutafakari, hivi  dawa ya vurumai hizi zote ambazo zimetokea bungeni kule Dodoma ni ipi?
Nimefika mahali nikafikiri  kuwa ingefaa siku moja uongozi wa Bunge uagize wataalamu wa afya wafike mahali hapo, wawapime akili wabunge wetu ili tuone kama wapo wenye kasoro, wasaidiwe.
Mifano ipo mingi ya matukio mengi ambayo yanaonyesha kasoro miongoni mwa wabunge wetu, kiasi cha kumfanya mtu makini ajiulize, kulikoni katika chombo hiki?
Nianzie kidogo kwenye vurumai zilizotokea bungeni mjini Dodoma siku ya Alhamisi, Mei 30, 2013.
Tofauti na nyakati nyingine ambako wahusika walikuwa wabunge wa chama tawala, CCM dhidi ya wale wa upinzani, safari ni baina ya wabunge wa upinzani.
Vurumai hizo ziliwahusisha wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya wale wa CUF wakati ule wa hotuba ya kambi ya upinzani kwenye mjadala wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Ni muda mfupi baada ya kumaliza wajibu wake wa kuwasilisha hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14.
Akiwasilisha hoja za upinzani, Hezekiah Wenje, Mbunge wa Nyamagana (Chadema) akawakera wenzake wa CUF kwa maneno ambayo si vizuri kuyarejea hapa.
Bila subira, wabunge wa CUF wakaanza kujibu mapigo, tena kwa maneno makali, kauli nzito ambazo licha ya Naibu Spika, Job Ndugai kujaribu kuwatuliza haikuwa, ndipo mkutano wa Bunge ukavunjika, Bunge likaahirishwa kwa muda.
Ndugai akalifikisha suala hilo kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo jioni ikatoa karipio kwa pande hizo mbili, jambo ambalo hata hivyo halikusaidia  kumaliza msuguano huo na Bunge likaahirishwa kwa mara ya pili.
Mlolongo huu wa matukio hayo kwa mara nyingine  umetia doa  au chumvi katika kidonda kibichi cha sifa mbaya ambayo chombo  hiki au mhimili huu wa dola tayari umekuwa nayo.
Niseme wazi kwamba siku zote ni uungwana kwa mtu kuomba radhi, ndiyo maana ninakubaliana na hatua ambayo viongozi waandamizi wa vyama hivyo wamechukua.
Kauli za Freeman Mbowe (Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni) kwamba waliwaumiza CUF na yule wa CUF, Rashid Alli Abdallah, mnadhimu wa chama hicho, aliposema kwamba walighafirika kwa lugha isiyofaa, zote zimesikika, sina shaka kwamba zimekubalika.
Hata hivyo, hili la kuomba radhi kwa viongozi hao baada ya vurumai hizo na maji kumwagika, kwa mara nyingine zimetoa picha mbaya kwa chombo hiki. 
Kauli hizi ndizo zinazotuacha wanajamii na hasa wafuatiliaji wa karibu wa mijadala ndani ya Bunge letu tukiwa na maswali mengi ambayo ni zaidi  ya majibu. Yote haya yanatia doa uadilifu wa chombo hiki.
Ninajiuliza, picha hii inayotolewa na wabunge wetu inawafanya Watanzania wakiamini tena chombo hiki?
Wawakilishi wetu hao kila mmoja tangu aingie humo mwaka 2010 anaufahamu vizuri wajibu wake katika kuitumikia jamii?
Zile semina elekezi walizopewa mwaka 2010 baada ya kuchaguliwa  au kuteuliwa kwa viti maalumu au kuteuliwa na Rais,  zimewasaidia kiasi gani.
Ina maana kuwa wamezisahau haraka kanuni hizo zinazosimamia chombo hiki au hata mchezo huo wanaoucheza?
Mbunge wetu anazifahamu vizuri kanuni, taratibu zote, ni kwa kiasi gani anajitahidi katika kuzitimiza au kuziishi?
Pia, wajibu wa spika au kiti chake katika kusimamia kanuni hizi na hata nidhamu katika Bunge unaheshimiwa kwa kiasi gani?
Kama hauheshimiwi, wabunge wetu wote wanataka kutuonyesha kuwa wamekwenda katika jumba hilo la kifahari, lakini bila kujua vizuri wajibu wao?
Ni kweli kwamba mbunge wetu anaweza kufanya chochote kile anacholipenda, tena bila kujali athari zake mbele ya jamii?
Pia, ni picha gani inayotolewa na wabunge wetu mbele ya jamii kila wanapoamua kushambuliana, kutukana au kutoleana maneno makali, kejeli na mambo kama hayo?
Wabunge wetu wamesahau kuwa wanaonekana laivu mbele ya runinga au vyombo vingine ambavyo vinaonyesha mijadala ya Bunge inayoendelea Dodoma?
Maswali machache hayana budi  kujibiwa na wabunge wetu kwa sasa.
Hata hivyo, ninapojaribu kutafuta majibu ya maswali haya ninakwama na matokeo yake ninapokutana na tatizo la msingi la  umakini na uthabiti wa kiti  cha spika.
Ninajiuliza, hivi kweli kiti kinapwaya, nini sababu za kupwaya kwake, ni kanuni au taratibu zote zinazotungwa kusimamia chombo hiki zimeshindikana kutelekezwa au kufuatiliwa?
Huenda ziliandaliwa kanuni hizi bila kujiuliza maswali  ya endapo zinatimiza azma iliyokusudiwa.
Tatizo la msingi ninaloliona ni utoto uliofichwa kwenye ushabiki wa kisiasa uliojengwa na kuendekezwa mno na wabunge wetu. Huo ndiyo unaosababisha vurumai kama hizi za kawaida kule Dodoma, zinazochekewa zikaachwa  zipite.
Wasiwasi wangu ni kuwa wengi wa wabunge wetu hawajitambui kwamba ajira zao hudumu kwa miaka mitano na kwamba mkataba wao na waajiri wao, wapigakura unamalizika baada ya muda huo.
Huenda jukumu la msingi la kutunga sheria ambalo Bunge letu linafanya, pia lile la kuisimamia Serikali halionekani machoni mwa wabunge wetu wengi.
Matokeo yake, kila wanapopata nafasi  basi hulipuka wapendavyo.
Nimshauri Ndugai au uongozi wa Bunge watambue wajibu wao  wasichoke  kwamba wanaandamwa mno na vyombo vya habari kila wanapokunjua makucha, husemwa.
Kama kanuni zipo, hazisimamiwi, hatua hazichukuliwi, ruhusa za wabunge kuacha vikao zimezidi, wengi huonekana mitaani wakiranda, wakihubiri siasa, kufanya mikutano ya hadhara wakati Bunge likiendelea. Kiti cha spika kichukue hatua, siyo kukaa kimya..

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment